Fei Toto amelingana idadi hiyo ya mabao na wachezaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki na Maxi Nzengeli pamoja na Mkongomani Jean Baleke wa Simba.
Mzanzibari huyo ambaye alitua Azam FC akitokea Yanga, aliliambia gazeti hili amejipanga kupambana ili kufunga mabao mengi zaidi msimu huu ambapo juzi usiku iliwachapa KMC mabao 5-0.
"Malengo yangu ni kuipambania timu yangu sio kitu kingine, mengine yatajulikana huko huko mbele ya safari," alisema Feisal ambaye mpaka sasa amehusika na mabao 11, akiwa ametoa pasi nne za mabao.
Alisema siri ya kuendelea kuwa katika kiwango cha juu tofauti na ilivyotarajiwa ni kujitunza na kuthamini kipaji chake alichopewa na Mwenyezi Mungu.
"Mimi najisikia vizuri sana, mimi mpira ni kazi yangu, nikienda popote pale na siri ya kuendelea kufanya vizuri ni kujitunza, kuheshimu kipaji na kufuata maelekezo ya walimu, kwa sababu ukifanya vyote hivyo uwezo wako unazidi kuongezeka," alisema Fei Toto.
Alisema hana nia ya kuwania tuzo yoyote msimu huu kwa sababu muhimu kwake ni mafanikio ya timu.