Miamba hiyo ambayo ndiyo itakayokutana katika nusu fainali ya kwanza Desemba 21, mwaka huu, imetinga hatua hiyo baada ya Kabwana fc kuwatoa Vijana wa KMT wa Shirati Sota kwa mikwaju ya penalti 2-0, kutokana na dakika 90 za mchezo kumalizika bila kufungana.
Katika robo fainali ya pili Shirati Mji ilitinga hatua ya nusu fainali baada ya kuichakaza Kyariko fc kwa mabao 2-0, yakifungwa na wachezaji wao machachari, Andrea Kisura dakika ya 40 na Chile wa Chile akihitimisha ushindi huo dakika ya 58.
Katika mchezo huo wa robo fainali, mwamuzi Francis Kembo, alimtoa nje mchezaji wa Kyariko, Otwera Otwera dakika ya 85, kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mbaya mchezaji wa Shirati Mji.
Shirati Mji inaonekana kupania kuendeleza kasi yao ya kubeba makombe wilayani Rorya baada ya mwezi uliopita kutwaa ubingwa wa Chege Cup, kwenye michuano iliyoandaliwa na Mbunge wa Rorya, Jafari Wambura Chege.
Mchezo mwingine wa robo fainali ya Umoja Cup 2023, unatarajiwa kupigwa kesho saa 10 alasiri katika Uwanja wa Maji Shirati Sota, ukiwakutanisha wenyeji wa mashindano hayo, Wanamji fc dhidi ya Mafundi fc kutoka Obwere.
Mshindi wa mechi hiyo, hatua ya nusu fainali atakutana na timu itakayoshinda katika robo fainali nyingine itakayopigwa uwajani hapo Alhamisi wiki hii kati ya Walinzi wa Mpakani, Bubombi fc kutoka Kirongwe dhidi ya Gonga fc ya Nyamagaro.
Akizungumza na mwandishi wetu baada ya michezo hiyo ya kwanza ya robo fainali, Mneja Mashindano hayo, Daniel Maina (Obong'o), alisema yamekuwa na ushindani mkali kama vile fainali.
“hatua ya robo fainali sasa ni kama fainali kwa sababu ukipigwa unaondoka," alisema Obong'o na kuongeza:
“Juzi baada ya KMT kutolewa baadhi ya viongozi wao walifanya fujo kuashiria hawakutolewa kihalali, wakati matokeo yalikuwa ni kwa mikwaju ya penalti, kiongozi wao mmoja anayejulikana kwa jina Felix alitishia kuharibu miundombinu ya uwanja, kitu ambacho ni mwiko katika mashindano ya Umoja Cup, hivyo sisi kama kamati ya mashindano tutajua namna ya kulishugulikia hilo."