Timu nane zilizofanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ambayo lengo lake mbali na kutoa burudani kwa Wanarorya, ni kuibua vipaji na kujenga umoja na ushirikiano wilayani humo, ni KMT ya Sota itakayocheza na Kabwana fc ya Mkoma, Shirati Mji ya Mkoma itakayocheza na Kyariko ya Raranya.
Nyingine ni wenyeji, Wanamaji FC ya Sota itakayovaana na Mafundi fc, pamoja na Bubombi ya Bukura Mpakani itakayokuwa na shughuli pevu dhidi ya Gonga fc kutoka Nyamongo.
Robo fainali ya kwanza hapo kesho itawakutanisha Vijana wa KMT dhidi ya Kabwana fc wakati ya pili kati ya Shirati Mji Fc na Kyariko Fc ikitarajiwa kuchezwa Alhamisi wiki hii, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Maji Shirati Sota.
Akizungumzia michuano hiyo ya Umoja Cup Rorya 2023, Meneja wa Mashindano, Danile Maina, alisema yamekuwa ya mwendelezo na yanazidi kukua kila mwaka jambo ambalo wanamshukuru mdhamini wao kwa, Peter Owino, kwa juhudi kubwa anazofanya kuhakikisha yanafanyika kila mwaka.
"Mdhamini wetu anajitahidi kuhakikisha kila mwaka mashindano haya hayakwami ili wadau wa soka wilayani Rorya waendelee kupata burudani na vijana waendeleze vipaji vyao", alisema Maina.
Kuhusu kupatikana mshindi aliyestahili kutokana na uwezo wake uwanjani, Maina alisema mashindano hayo yanayodhaminiwa na mdau wa michezo wilayani Rorya, Owino, huchezeshwa na waamuzi makini kutoka mkoani Mara.
Maina alizitaja zawadi zitakazotolewa kwa washindi wa Umoja Cup 2023; mshindi wa kwanza mbali ya medali na kombe ataondoka na Sh. 500,000, wa pili atajinyakulia Sh. 150,000 na seti moja ya jezi, huku wa tatu akizawadiwa seti moja ya jezi na Sh. 50,000 na mshindi wa nne akibeba mpira Sh. 30,000.
"Kocha bora wa mashindano, atazawadiwa 'tracksuit', huku mchezaji bora akiondoka na Sh. 20,000 sawa na mfungaji bora na kipa bora ambaye mbali na kiasi hicho cha fedha atapewa pia zawadi ya 'gloves', wakati mchezaji chipukizi akiondoka na kiatu. Timu yenye nidhamu itazawadiwa 'jozi 15 za 'stocking' (soksi za kuchezea mpira)," alisema.
Timu zilizoshiriki mashindano hayo yalikuwa yakichezwa kwa mfumo wa mtoano (nyumbani na ugenini), kabla ya kutinga hatua ya robo fainali ni Kirengo fc, Wanamaji fc ambao ni wenyeji, KMT fc, Masonga, Bubombi, Victoria, Kirongwe, Donga, Nyahera, Kabwana United, Homeboys, Shirati Mji, Kyariko, Rifa, Wimbi na Mafundi fc ambao ni mabingwa watetezi.