Simba, Yanga mambo magumu CAF

04Dec 2023
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Yanga mambo magumu CAF
  • Ingawa kila timu bado ina nafasi, laikini kwa matokeo haya wamejiweka katika.....

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, Simba na Yanga zimejiweka katika mazingira magumu kwenye makundi yao kusonga mbele japo bado wana nafasi ya kufanya hivyo licha ya matokeo ya juzi kwenye michezo yao ya ligi hiyo.

Wakati Simba ikitoka sare bila kufungana na wenyeji wao Jwaneng Galaxy kwenye Uwanja wa Obed Itani Chilume nchini Botswana mechi iliyochezwa mapema, saa 10 jioni, Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Mabingwa Watetezi, Al Ahly ya Misri, mechi ikichezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, saa 1:00 usiku.

Bao la dakika ya 90 lililowekwa wavuni na Kiungo mshambuliaji raia wa Ivory Coast, Pacome Zouzoua, liliiokoa Yanga kupata kipigo cha pili katika Kundi D dhidi ya Mabingwa Watetezi wa michuano hiyo, Al Ahly ya Misri.

Pacome alifunga bao hilo akiwa ndani ya eneo la hatari kwa shuti huku akizingirwa na mabeki wa Al Ahly wakati akipokea pasi ya Kennedy Musonda aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Clement Mzize.

Bao hilo la Pacome lilikuja dakika ya 89 baada ya wageni Al Ahly kutangulia kwa bao la dakika ya 87 la nyota wa Afrika Kusini, Percy Tau.

Tau aliunganisha kwa kichwa mpira uliookolewa kizembe na Bakari Mwamnyeto, huku kipa Diarra akiwa ametoka langoni kutokana na krosi ya Karim Fouad aliyeambaa na mpira wingi ya kushoto kabla ya kupiga krosi hiyo iliyowashinda mabeki wa Yanga.

Yanga ilianza mechi hiyo kwa kasi, ikifanya mashambulizi mfululizo yaliyoiwezesha kupata kona tatu ndani ya dakika kumi za mwanzo, lakini zote ziliondoshwa na mabeki wa Al Ahly.

Mzize nusura aipatie Yanga bao dakika ya tisa kama si kazi kubwa iliyofanywa na kipa Mohamed El Shenawy akiwa amebaki na kipa huyo na mpira mguuni huku akisumbuliwa na mabeki wawili waliokuwa pembeni yake alijikuta akipiga mpira nje huku Stephane Aziz Ki akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga kama angepewa pasi hiyo.

Iliwachukua Al Ahly dakika 13 kufika kwa mara ya kwanza katika lango la Yanga, wakati, Emam Ashour alipowatoka mabeki wa Yanga na kuachia shuti kali lakini kipa Djigui Diarra aliyekaa langoni kwa mara ya kwanza akitoka kwenye majeruhi alilidaka.

Yanga ilipata pigo dakika ya 33 ya mchezo baada ya Joyce Lomalisa kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo na Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi akalazimika kumuingiza Nickson Kibabage kuchukua nafasi yake.

Kwa matokeo ya jana, kwa upande wa Yanga  wapo katika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa kundi D linaloongozwa na Al Ahly wenye pointi nne baada ya ushindi dhidi ya Medeama ya Ghana waliyoifunga mabao 3-0 na sare ya jana dhidi Yanga, CR Belouizdad ya Algeria wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi tatu sawa na Medeama, Yanga wanashika mkia wakiwa na pointi moja.

Jijini Francistown,  Simba itabidi ijilaumu yenyewe kwa kushindwa kutoka bila ushindi kwenye mechi yao ya Kundi B, kwani ilitawala karibuni muda mwingi mwa mchezo, hasa kipindi cha kwanza lakini wachezaji wake walionekana kutokuwa makini kuweka mipira ndani ya nyavu.

Kama Jena Baleke na Saido Ntibazonkiza wangekuwa makini wangeweza kuipatia bao Simba sekunde ya 55 tu baada ya mechi kuanza, kutokana na kazi nzuri ya Kibu Denis aliyemtoka beki wa kushoto Lesego Keredilwe na kumimina majaro ambayo iliwapita mbele yao.

Dakika tatu baadaye, Kibu tena alifanya kazi nzuri baada ya kumtoka tena Keredilwe lakini washambuliaji wa Simba walichelewa kuingia kwenye eneo la hatari na krosi yake nzuri ikaokolewa na mabeki wa Jwaneng.

Beleke alifanya jaribio lingine dakika tano baadaye alipopenyezewa pasi na Willy Onana, lakini wakati anataka kuunganisha kwa mguu wake wa kushoto badala ya kupiga mpira akapiga mguu wa beki wa kati Thabo Lenanyane na kumpa nafasi kipa Goitseone Phoko kuukamata mpira kirahisi.

Kipa huyo alifanya kazi ya ziada dakika ya nane alipodaka mpira wa kichwa kilichopigwa na Sadio Kanoute uliotokana na kona ya Saido.

Dakika moja baadaye ilikuwa zamu ya kipa wa Simba, Ayoub Lakred, alipoiokoa timu yake isifungwe bao kutokana na shambulizi kali la kushtukiza.

Lilikuwa ni shambulizi la kwanza kwa Jwaneng Galaxy likifanywa dakika ya tisa, wakati straika wao hatari Daniel Msendami alipoupata mpira mrefu na kuanza kuwatoka mabeki wa Simba mmoja baada ya mwingine, kabla ya kutaka kuuweka wavuni, lakini Lakred aliruka na kucheza mpira kwa mguu na kuwa kona tasa.

Baleke alipata nafasi nyingine ya kuandika bao dakika ya 24, lakini akiwa ana kwa ana na kipa Phoko, shuti lake lilidakwa.

Kocha, Mualgeria Abdelhak Benchikha aliyekuwa benchi kwa mara ya kwanza akimrithi Mbrazil Roberto Oliveira, alifanya mabadiliko ya wachezaji kipindi cha pili kwa kumtoa Kanoute, Kibu, Saido na Onana, na kuwaingiza Clatous Chama, Mzamiru Yassin, Luis Miquissone na Moses Phiri, lakini bado walishindwa kupata dawa ya kuipenye ngome ya Jwaneng Galaxy na kupata bao.

Nafasi pekee kubwa ambayo wanachama na mashabiki wa Simba wataiota ni ile ya dakika ya 90,  ambapo shuti la mguu wa kushoto la Chama lilikwenda kugonga mlingoti wa pembeni kwa chini na kurudi uwanjani, ukamkuta Baleke ambaye alipiga shuti kubwa juu ya lango.

Kwa matokeo hayo, Simba wanakusanya pointi mbili katika michezo miwili waliyoicheza na sasa wanasubiri mchezo unaofuata dhidi ya  Wydad Casablanca kabla ya kuanza michezo ya marudiano.