Wahasibu washindana kuogelea kwenye kongamano lao la mwaka

30Nov 2023
Elizaberth Zaya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wahasibu washindana kuogelea kwenye kongamano lao la mwaka

BODI ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), imeendesha mbio za kilomita tano na 10 pamoja na michezo ya kuogelea kwa washiriki wa kongamamo la Wahasibu mwaka huu linalofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam.

Mbio hizo zimehusisha utoaji wa zawadi mbalimbali kwa washindi wa kwanza mpaka wa tatu wa michezo hiyo.

Akizungumza baada ya  michezo hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Viwango vya Kiuhasibu, Utafiti na Huduma za Ufundi wa NBAA, Angyelile Tende, amesema lengo la kuendesha michezo hiyo ni kuhamasisha washiriki kuchangia fedha kwa ajili ya kwenda kuwasaidia watoto wanaougua magonjwa ya saratani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Amesema washiriki waliojitokeza katika michezo hiyo ni 800 na kwamba lengo lao limekamilika kama walivyopanga.

Kongamano hilo la Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania  linatarajiwa kufungwa kesho.