Hayo yamebainishwa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara Abdulrahman Kinana, katika maadhimisho ya miaka mitatu ya uongozi wa Dk. Mwinyi.
Kinana amesema Dk. Mwinyi amejituma sana na kujikita katika kuleta maendeleo ya wananchi wa Unguja na Pemba huku akiwaunganisha kuwa kitu kimoja.
Akiyataja mafanikio yaliyopatikana Zanzibar kwa miaka mitatu tangu Rais Dk. Mwinyi alipoingia madarakani, Kinana amesema ni pamoja na kuharakisha maendeleo kwa kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali na miradi ya wananchi ya kiuchumi.
"Pia amewaunganisha wananchi, na kusahau tofauti za itikadi za kisiasa, na watu wote kuwa wamoja," amesema kinana.
Ameongeza kwa kufafanua kwamba, hatua hiyo inatoa matumaini katika kipindi cha miaka miwili iliyobakia kufikia ukamilikaji wa malengo ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025.
"Rais Mwinyi tunakushuru sana, katika kipindi cha miaka mitatu umefanya mambo makubwa, ikiwemo kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, pamoja na kuwaunganisha wananchi na kuimarisha amani na utulivu wa kisiasa," amesema Kinana.










