Kampuni binafsi za ulinzi zatakiwa kuzingatia sheria

05Nov 2023
Vitus Audax
MWANZA
Nipashe Jumapili
Kampuni binafsi za ulinzi zatakiwa kuzingatia sheria

OFISA Polisi Jamii mkoani wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Ramadhani Sarige amewata Wakurugenzi na wamiliki wa kampuni binafsi za ulinzi kufuata sheria kwa kuwasimamia ipasavyo askari wanaowaajiri kufanya kazi hiyo kwa mujibu sheria na taratibu za ulinzi.

ACP Sarige ametoa wito huo wakati wa kikao kazi na uongozi pamoja na wamiliki wa kampuni hizo, ambapo amewataka kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa kutoa mafunzo kwa walinzi ili kuleta uelewa wa pamoja na kuimarisha nidhamu kwa askari hao wakati wanapotekeleza majukumu ya ulinzi.

Naye Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Yesaya Suddy akitoa elimu katika kikao hicho alisema katika jamii si ajabu kukutana na mlinzi anayelinda mali yenye thamani ya zaidi Sh. milioni 500 lakini hajui hata kutumia silaha aliyonayo kwenye lindo kitu ambacho ni hatari kwa usalama wake na mali husika.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ilemela Mrakibu mwandamizi wa Polisi (SSP), Ignatus Kapila amewataka wamiliki kutoa elimu kwa walinzi kwa kushirikiana katika lindo kwani sio jambo jema kuona lindo la jilani linavamiwa na mlinzi jilani anaona kwani ipo siku anaweza kuvamiwa na yeye hivyo ushirikiano ni suala muhimu.

Hata hivyo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana Mrakibu Msaidizi wa Polisi, (SP), Virginia Sodoka amesema wataanza kuchukua hatua kali za kisheria kwa wamiliki wa makampuni binafsi ya ulinzi watakaoendelea kukiuka sheria na taratibu za nchi.

Nao viongozi wa Kampuni binafsi za ulinzi akiwemo Salum Mparo waliahidi kwenda kutekeleza yale yote yaliyoadhimiwa katika kikao hicho ili kuboresha utendaji wa askari wao ikiwa ni pamoja na kuangalia masilahi yao.

"Tumekumbushwa kuhakikisha tunafata taratibu zote za ajira hususan katika kuwalipa walinzi mishahara kwa wakati kwa kufuata viwango vilivyowekwa na serikali, Kuwapa mikataba ya kazi za ulinzi na kupeleka michango yao NSSSF," aliongeza.