Mashindano hayo yamezinduliwa leo katika Viwanja vya Leaders Club Jijini Dar es Salaam ambapo wadau mbalimbali wa soka wamehudhuria hafla hiyo.
Timu itakayochaguliwa itacheza mechi ya kirafiki na timu mojawapo ya Ligi Kuu, na kujinyakulia kitita cha sh.milioni 44 na itajulikana kama Timu ya Mabingwa ya Safari Cup yaani Safari Cup Champions.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa Chapa ya Safari Lager, Pamela Kikuli amesema bia ya Safari, ambayo ni ya mabingwa imeamua kuja ya kampeni hii ili kuibua vipaji vipya kabisa vya mpira wa miguu kwani wanaamini kuna vipaji vingi nchini ambavyo havijaibuliwa.
Amesema mashindano hayo yatafanyika katika mikoa minne ambayo ni Mbeya katika uwanja wa (FFU Polisi) Oktoba 7,2023; Arusha (Uwanja wa Ngarenaro) Oktoba 21,2023; Mwanza (Uwanja wa Nyamagana) Novemba 04,2023 na Dar es Salaam (Viwanja vya Kinesi) Novemba 18,2023.
"Vijana wenye umri wa Miaka 18 na zaidi wataitwa kwenye usaili ili washiriki katika mashindano ya mtoano yatakayofanyika ili kuchagua vijana ambao watawakilisha timu ya kila mkoa kati ya mikoa minne iliyochaguliwa," amesema na kuongeza kuwa:
“Baada ya hapo timu zile za mkoa zitatumika kuchagua vijana ambao wataunda timu moja kubwa ya wachezaji 22 ambao watacheza mechi ya kirafiki na timu mojawapo ya Ligi Kuu ambayo itatangazwa hapo baadaye," amesema.
Ameongeza kuwa mchezaji mmoja atapata fursa ya kuchaguliwa na mawakala wa ligi kuu bara ili kuweza kuchezea timu kubwa hapo baadae.
"Mawakala hawa watakua wakifuatilia vipaji vya wachezaji wa Safari Lager Cup Champions ili kuendeleza vipaji vyao katika soka” amesema Kikuli.
Amesema wakati wa mashindano hayo, tungependa kuwaalika wakala wa vilabu mbalimbali vya Ligi Kuu waje kuangalia baadhi ya wachezaji ambao wanaweza kujiunga na timu kubwa za Ligi Kuu.
Kocha Jamhuri Kihwelo, ambaye atakuwa mmoja wa makocha katika kusaka vipaji, pamoja na Sekilojo Chambua aliyewahi kuichezea timu ya Tukuyu Stars ya Mbeya, ambaye pia amecheza Yanga kwa kupindi cha miaka 10.
Makocha hao wawili watashiriki katika kuibua vipaji hivi kwa kuchagua vijana watakaounda timu hizi za mikoa na hatimaye timu ya Safari Lager Cup Champions.
“Tunaipongeza sana bia ya Safari kwa kuona umuhimu huu wa kuibua vipaji miongoni mwa vijana kwani kuna vipaji vingi mno mikoani lakini hakuna wa kuviibua na kuviendeleza,” amesema Kocha Kihwelu.
Naye Kocha Chambua amesema, “Ni heshima kubwa kwetu kupata fursa hii ya kutafuta vipaji mikoani na kuunda timu hii ya Safari Lager Cup Champions.
Ni matumaini yetu kuwa vijana watajitokeza kwa wingi kwenye usaili ili washiriki katika mashindano haya.”
Bia ya Safari Lager imewahi kudhamini mashindano ya Taifa Cup ambayo yalishirikisha mikoa yote ya Tanzania kwa lengo la kuibua vipaji.










