Robertinho atamba kupata dawa ya Power Dynamos

14Sep 2023
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Robertinho atamba kupata dawa ya Power Dynamos

ZIKIWA zimebaki siku tatu kabla ya mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika raundi ya kwanza, Kocha wa Simba, Robertinho Oliveira, amesema tayari ameandaa ‘dawa’ kwa ajili ya wapinzani wao, Power Dynamos na watawashangaza wakiwa nyumbani kwao.

Simba itakuwa mgeni wa Power Dynamos Jumamosi kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza kusaka tiketi ya kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Akizungumza na Nipashe, Robertinho alisema wapinzani wao hao wasitegemee kuiona Simba waliyocheza nayo kwenye tamasha la Simba Day Agosti 6, mwaka huu, kwani katika mchezo huo utakaochezwa Jumamosi wiki hii, wataingia uwanjani tofauti.

“Mchezo tuliokutana nao siku ya Simba Day ulikuwa na makusudio tofauti, huu wa Septemba 16, mwaka huu nao ni tofauti, huu ni mchezo wa maamuzi, nimetumia muda kuwasoma wapinzani wetu na tayari mikakati yangu imekaa sawa tunasubiri siku ya mchezo,” alisema Robertinho.

Katika mchezo huo wa kirafiki ambao Power Dynamos walialikwa, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, mabao ya Willy Onana na Fabrice Ngoma.

Alisema utofauti kwenye mchezo wa Jumamosi ijayo utaanzia aina ya wachezaji atakaochagua kuanza katika mchezo na aina ya mfumo atakaoutumia.

“Hautakuwa mchezo mwepesi kwa sababu wapinzani wetu nao wamejiandaa, lakini Simba ni timu kubwa yenye wachezaji wenye uwezo mkubwa na lazima tulionyeshe hili, tutatumia siku hizi chache zilizobaki kumalizia maandalizi yetu ambayo kwa kiasi kikubwa tumefika mbali, tunaomba tu sapoti ya mashabiki wetu,” alisema Robertinho.

Alisema kwa ratiba ilivyo wanatarajia kuondoka nchini kesho kuelekea Zambia tayari kwa mchezo huo na watarejea haraka kujipanga kwa ajili ya mchezo wa marudiano ambao utathibitisha timu itakayofuzu hatua hiyo ya makundi.

Kama Simba itafanikiwa kutinga hatua hiyo itakuwa mara ya tano kwenye michuano hiyo tangu msimu wa 2019-2020.