Wanamazingira Afrika wanapokutana Kenya kuibua mapya kitisho tabianch

01Sep 2023
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wanamazingira Afrika wanapokutana Kenya kuibua mapya kitisho tabianch

MKUTANO wa hali ya hewa au wa mabadiliko ya tabianchi barani Afrika, unaanza Jumatatu ijayo jijini Nairobi. Likiwa ni jukwaa la  kushughulikia ongezeko la changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na gharama zinazohusiana na tatizo hilo kote duniani lakini pia hasa barani Afrika.

 

Ni mkutano unaotarajiwa kueleza wapi Afrika ilipo na inapokwenda, hatua za haraka zinazohitajika kuchukuliwa ili kupunguza changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa, unaeleza mtandao wa Mtandao wa africaclimate.org.

Septemba 4 hadi 8 ndiyo siku za mkutano huo ambao pia unapewa jina la Africa Climate Week 2023 au Wiki ya Hali ya Hewa barani Afrika.

Ni juma linalotoa fursa kwa watunga sera, watendaji, wafanyabiashara, na mashirika ya kiraia kubadilishana taarifa kuhusu changamoto na ufumbuzi wa masuala ya hali ya hewa, vikwazo vya kukabili na fursa zinazopatikana katika maeneo mbalimbali.

Wiki ya Hali ya Hewa barani Afrika itajielekeza kwenye maeneo manne kwa nia ya kutoa michango inayolenga kupata mambo au ajenda ambazo kanda ya Afrika itafikisha kwenye jukwaa la kimataifa la mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa  kikao cha 28 cha Mkutano wa Nchi Wanachama COP 28 kitakachofanyika kuanzia Novemba hadi Desemba 12, 2023 huko Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mambo ambayo washiriki wa wiki hiyo ya Afrika  watayajadili kwa kina ni pamoja na nishati na viwanda, majiji, miji na makazi mijini. Aidha, suala jingine ni miundombinu, usafirishaji na usafiri.

Kadhalika watajadili ardhi, bahari, vyakula maji,  jamii pamoja na afya, kupata mahitaji muhimu kama maji, chakula, dawa, makazi na mavazi (livelihoods) na uchumi, kwa mujibu wa wa africaclimate.org

MAMBO YALIVYOANZA

Masula ya  tabianchi yamenza kushughulikiwa  takribani miaka 31 iliyopita,  ilikuwa 1992  mkutano wa kwanza wa wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), ukifanyika jijini  Rio de Jenairo nchini Brazil.

Miongoni mwa mashuhuda wa mchakato huo ni Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Misitu na Nyuki nchini, Dk Felician Kilahama, anayesema katika mahojiano kuwa ni miongo mitatu tangu mambo ya mabadiliko ya tabia nchi yalipoanza, lakini halipo la kujivunia kwani hakuna hatua za kuridhisha zilizopigwa.

Anakumbusha kuwa mkutano wa kwanza wa masuala hayo wa Rio uliunda chombo kiitwacho United Nations Framework Convention on Climate Change (UNFCCC).

Jopo hilo la Umoja wa Mataifa la UNFCCC linaundwa na watu mbalimbali wakiwamo wataalamu,wanasayansi mashuhuri,wakuu wa nchi, wasomi , watafiti  na asasi za kiraia wamekuwa wakikutana kila mwaka, waanza kwanza  wataalaam kuandaa masuala ambayo Wakuu wa nchi wataweza kukubaliana na kuyapitisha, ukifanyika kwa wiki mbili kati ya Novemba na Decemba kila mwaka.

 

Wakuu wa nchi kushiriki kikao hicho siku tatu za mwisho na huitwa (High-level Session), wakifanya maamuzi, baada ya kuchakatwa na wataalam mbalimbali wa sayansi na mazingira, anaongeza mtaalamu huyo.

 

Mambo ambayo wakuu wa nchi waliwahi kufanyia maamuzi ni kuundwa kwa mifuko kadhaa ya kushughulikia tabianchi. Moja wapo ni ‘Adaptation Fund’ au mfuko wa uhimilivu, mwingine ni wa fidia ya maafa na ule wa Global Environment Facility (GEF).

 Adaptation Fund husaidia nchi wanachama kuweza kukabiliana na majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi, anaeleza Dk.Kilahama.

Aidha, ni pamoja na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na matatizo kama kilimo cha uhimilivu kutokana na ukame, kuzuia mmomonyoko wa udongo, kukabiliana na mafuriko, kuongeza uwezo wa nchi kuwa na misitu ya kutosha kama mbinu halisi ya kuondoa mlundikano wa gesiukaa hewani   na kuongeza zaidi oksijeni.

BIASHARA YA GESI 

Hapa kuna mkakati wa kuweza kufanya biashara ya gesiukaa (carbon trading), akizungumzia biashara hiyo Dk. Kilahama anasema kwa uzoefu wake, kumekuwa na maneno  ya mengi kukabiliana na matatizo yanayotajwa lakini vitendo hakuna kinachoridhisha hata kidogo.

“Ni siasa zaidi kuliko kuchukua hatua. Kiuhalisia mataifa yaliyoendelea, nchi tajiri ndiyo wazalishaji wa kiasi kikubwa cha gesiukaa ukilinganisha na mataifa yanayoendelea kama Tanzania. Kikwazo kwa mataifa makubwa kuchukua hatua ni "uchumi" viwanda vyao kuweza kurekebisha vyanzo vya nishati ni changamoto kubwa na hawako tayari kuona mapato ya nchi yanashuka sana. Hivyo suala la mabadiliko ya tabia nchi ndani ya miaka 31 iliyopita halijaweza kuzaa matunda na mambo ya kujivunia.” Anasema

Kadhalika, mifuko ipo na fedha wanaweka lakini siyo kama wanavyokubaliana na nchi maskini na zinazoendelea kuweza kupata fedha hizo nayo ni changamoto nyingine. Kuna mikwara mingi na michakato ya kitaalamu ni mirefu kiasi kwamba uwezo wa nchi zenye uchumi unaoinukia ni mdogo, anasema mtaalamu huyo.

Anaongeza: ” Ukiangalia masuala ya kufanya biashara ya gesiukaa, siyo rahisi kama ilivyokuwa ikionekana katika kikao cha Desemba, 2007 kilichofanyika Bali nchini Indonesia. Kikao hicho kilikuwa kimenipa matumaini makubwa na nikaona iwapo mambo yatakuwa kama yalivyozungumzwa, misitu katika nchi za Afrika, itapona maana nilitegemea wananchi watawezeshwa na hatimaye waweze kuitunza misitu ya asili na kupanda miti mingi zaidi katika maeneo yao kwaajili ya kuuza gesiukaa na kupata fedha.”

Anasema kuwa matokeo yake hadi sasa hakuna matumaini makubwa ingawa kuna maelezo kuwa michakato inaendelea, na kwamba wakati anastaafu 2012 hadi sasa (zaidi ya miaka 10) hakujawa na uhakika biashara ya gesi ukaa inakuwaje?

Dkt. Kilahama anasema imekuwa ni kuhangaika na wakati huo kasi ya kutoweka misitu ya asili nchini ikiwa ni kubwa, hali hiyo ni tishio kwa uhai wa mazingira na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Anasema angalau kwa mashamba ya miti Tanzania imejitahidi kupitia Wakala wa Huduma za  Misitu (TFS), lakini kwa misitu ya asili usimamizi wake ni kidogo mno , hata hivyo, kwenye ile ya lindimaji au  misitu hifadhi asilia (nature forest reserves), imekuwa ikilindwa na kuendelezwa kwa msaada wa mfuko wa The Global Environment Facility (GEF) kupitia Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kushirikiana na serikali kupitia TFS, Wizara ya Maliasili na Utalii.

 

AHADI TATA

Katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa wa 2009 au Mkutano wa  Copenhagen, uliofanyika Copenhagen, Denmark ukipewa jina la COP15 mwaka 2009, nchi zilizoendelea ziliahidi kwa pamoja  kuhamasisha kupata dola bilioni 100  ifikapo 2020 kusaidia hatua za hali ya hewa katika nchi zinazoendelea.

 

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa za UN lengo hilo halijafikiwa kama ilivyokuwa imekusudiwa na juhudi zinaendelea. Kama ndivyo hali ilivyo kazi ni ngumu na ufumbuzi huenda ukawa vigumu kupatikana, kwa vile waongeza joto na mabadiliko ya tabianchi hawako tayari kuwajibika.