Kijana huyo mkazi wa Mbeya Mjini, amekata tamaa na kuamua kulewa muda wote, ndivyo anavyosimulia maisha yake kwa Nipashe, akisema amekabiliwa na tatizo la kukosa nguvu hizo kwa miaka kadhaa.
Tatizo lake limepata tiba, ni wakati huu wanaume wanaokumbwa na shida hiyo, wanapokutana na usaidizi wa kitaalamu wa kupandikizwa visisimua uume.
Habari njema ilisikika Juni 14 mwaka huu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Dodoma, hapo wataalamu wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji Mfumo wa Mkojo Tanzania (TAUS) na mbobezi kutoka Ufaransa, wanashirikiana kuanzisha teknolojia hiyo.
Dokta Remigius Rugakingira mbobezi wa magonjwa ya mfumo wa mkojo na wanaume (urolojia) wa BMH akizungumzia tatizo hilo, anasema wameamu kuja na suluhisho hilo baada ya kubaini kuna shida miongoni mwa wanaume wakilenga kusaidia ambao uume unakosa nguvu na kuwarejeshea faraja kinababa hao waliokosa watoto.
MAISHA YA JOHN
John mkazi wa Nzovwe mjini Mbeya, anayaona maisha ni magumu kwake, akisema anaishi bila kuwa na mwenza na kwamba hakutarajia pia kupata mtoto.
Anasema alibaini kuwa ana tatizo hilo akiwa na umri wa miaka 20 na kwamba hakikuwa kikwazo kwake kwa kuwa alikuwa mwanafunzi wa kidato cha nne.
"Nilidhani kwamba bado ni mdogo. Maana wakubwa wanatuambia tusome shule kwanza tukimaliza tutayakuta mambo ya kikubwa. Ajabu nimeishi hivyo hadi sasa, uume wangu si kama wa wengine...natamani kuwa na familia ila nawaza kuoa kutakuwa mwanzo wa aibu yangu kuwekwa hadharani," anaeleza John.
Anasema kwake faraja ni kushinda vijiweni kuzungumza na vijana wenzie na ikifika saa 12 jioni huhamishia furaha yake kwenye vilabu vya pombe, akirejea nyumbani kwake ni usiku wa manane.
"Siku yangu naifanya iwe fupi, napiga stori na washkaji mchana ila jioni nahamia kilabuni. Natamani kupata tiba kama ipo. Kwa sababu nimetumia za kienyeji nimeshindwa. Ingawa nimesikia kupitia taarifa za habari, kuna huduma ya kututibu watu kama sisi. Lakini najiuliza nitamudu gharama, sina kazi yenye ujira rasmi, nafanya vibarua hasa kubeba mizigo, kwa siku naingiza Sh. 2,000 hadi 2,500," anasema John.
Kwa mujibu wa tovuti ya ‘edtreatmentindia’, upandikizaji huo nchini India hugharimu Dola za Marekani 6,000 hadi 10,000 huku huduma kama hiyo Uingereza au Marekani ikifikia kati ya Dola 15,000 hadi 25,000.
KILICHOISUKUMA TAUS
Daktari Rugakingira, anasema TAUS, katika mkutano wake wa pili tangu kuanzishwa uliofanyika Dodoma, mwaka huu, moja ya ajenda ilikuwa ni kupata suluhisho kwa wanaume wenye tatizo la nguvu za kiume.
"Tuliona umuhimu wa kuanzishwa huduma hii. Kazi yetu kubwa ni kutibu nguvu za kiume, kuanzisha huduma hii ambayo watu walikuwa wanaipata nje kwa gharama kubwa.
"Huduma hii ipo Afrika katika nchi chache, nasi tumekuwa wa kwanza. Upandikizaji huu usifananishwe na kupandikiza uume wote. Mfano nina mwalimu wangu Afrika Kusini, alishampandikiza mgonjwa uume baada ya mgonjwa aliyekufa ubongo kuamua kutoa uume wake kabla hajafa," anaongeza;
Anasema baada ya hospitali hiyo kuanzisha huduma hiyo, mwitikio na maswali kutoka kwa wanajamii kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, umekuwa mkubwa huku zaidi ya watu 40,000 wakiuliza huduma hiyo.
"Tumebaini wengi wana tatizo na hawana elimu kuhusu nguvu za kiume. Sio kila anayepata shida hiyo suluhisho linakuwa moja, yapo mengi. Na hii huduma ni mojawapo, ingawa kuna dawa na ushauri.
Anasema pamoja na huduma hiyo kufika nchini, zipo changamoto ikiwamo upatikani wa vipandikizi ambavyo hutumika ili kuuongezea uume nguvu,
"Kinachotakiwa ni vifaa na vipandikizi, changamoto itakuwa vifaa na gharama, ila serikali ina wataalamu na itaamua namna ya kupanga gharama ili kuhudumia watu.
Anawaalika wenye changamoto hizo kufika hospitalini na kinamama pia ambao wanapitia shida ya uzazi, lakini hawapati watoto hilo ni suluhisho kwao akisema asilimia 60 hadi 80 wengine wana tatizo la kisaikolojia wakishauriwa wanarudi katika hali zao kama kawaida.
"Iwe chachu kwa wanataaluma wenzetu kukiri kwamba tunaweza, tupende vya kwetu. Lakini inatupa fursa hasa wawekezaji wa viwandani kwa sekta ya afya, wakawa na vifaa yaani vipandikizi, vikipatikana hapa nchini wengi watatibiwa na kuifanya nchi yetu kuwa kituo cha kufanyia utalii wa afya."
Bingwa huyo anasema, upandikizaji huo hutumia saa mbili kwanza huanza kwa ushauri kwa mgonjwa, kabla ya kufanyiwa upasuaji na baada ya hapo mgonjwa huyo huhitajika kufanyiwa ufuatiliaji kwa miezi kadhaa, ili kujua maendeleo yake.
"Najiona vyema kuwa mmoja wa walioanzisha huduma kupandikiza uume, nakumbuka pia nilikuwa katika jopo la waanzilishi wa kupandikiza figo najua wengi wanafanya makubwa kama mimi.
Anaeleza kuwa kwa siku wanaweza kupandikiza wanaume wanne kulingana na uhitaji, wakiangalia pia sifa na vigezo kwa ambaye anaweza kufanyiwa huduma hiyo.
Kiongozi wa TAUS, Dk Lyuba Nyamsogoro, anasema kuwa wamefikia hatua hiyo kutokana na uwepo wa watu wengi wenye matatizo ya nguvu za kiume nchini na Afrika kwa ujumla.
“Mojawapo ya dhumuni la TAUS ni kuendeleza wataalam nchini kwa kushirikiana na wabobezi wengine kutoka nje ili kuiletea Tanzania teknolojia inayopatikana duniani na kutibu wagonjwa wenye matatizo,” anasema Dk Nyamsogoro.
Msemaji wa BMH Jeremiah Mbwambo, anaeleza, kuwa hospitali hiyo inakuwa ya kwanza nchini kufanya upasuaji wa kuweka vipandikizi kwenye uume kwa wagonjwa wenye matatizo ya nguvu za kiume na kwamba serikali inaendelea kufanya uwekezaji kwa kuwawezesha teknolojia za kisasa za matibabu.










