Akizungumza na Nipashe Digital, Robertinho amesema hasa anataka kuona safu yake ya ulinzi inafahamiana na kuzoeana kwa sababu timu ina mashindano mengi na kila mchezaji anatakiwa kutoa mchango.
Robertinho amesema anahitaji safu yake ya ulinzi iongeze umakini kwa sababu lango linatakiwa kuwa salama wakati wote wa mchezo.
Amesema kuna makosa aliyoyabaini katika safu ya ulinzi kwenye michezo iliyopita baada ya kuumia kwa Mkongomani, Henock Inonga, ambaye tayari alikuwa ameshatengeneza uelewano mzuri na Che Fondoh Malone.
“Baada ya kuumia kwa Inonga, nafasi yake anacheza Kennedy (Juma) pamoja na Che Malone, tunaendelea kufanya mabadiliko ya kikosi taratibu ili wachezaji wazidi kuzoeana. Tuna timu bora lakini tunapaswa kucheza kitimu.
Henock alianza kuzoeana kiuchezaji na Che Malone lakini sasa ameumia, tuna Kennedy na Hussein Kazi, wanafanya vizuri lakini wanapaswa kucheza pamoja mara kwa mara ili wawe bora zaidi,” alisema Robertinho.
Ameongeza mabadiliko ya kikosi cha timu hiyo yatafanyika taratibu kwa sababu anaimani ana wachezaji wengi ambao ni wazuri na watakaotoa ushindani kutokana na ubora walionao.
Mbrazil huyo amesema kazi kubwa ambayo anaifanya ni kuimarisha umakini wa kila idara kwa kupata muunganiko ambao utapelekea kila mmoja kuwa tayari kucheza na mwenzake.
Naye Daktari wa Simba, Edwin Kagabo, ameiambia Nipashe Digital kuwa nyota wao, Aubin Kramo, anaendelea vizuri baada ya kupewa mapumziko ya wiki mbili na kesho anatarajia kuanza mazoezi ya ushindani pamoja na wachezaji wenzake.
Kagabo amesema Kramo aliumia goti wakiwa katika maandalizi ya michuano ya Ngao ya Jamii na hakufanikiwa ama kucheza au kufanya mazoezi magumu mpaka sasa ambapo afya yake imeimarika.
“Sasa hivi anaendelea vizuri baada ya kupewa wiki mbili za mapumziko huku akiwa chini ya uangalizi wangu, tunatarajia Ijumaa (kesho), atashiriki katika mazoezi yenye ushindani,” amesema daktari huyo.










