Kutokana na hali hiyo ambayo inasababisha uharibifu wa mazingira, Serikali imeonya kuwa mtu yeyote atakayekutwa na hatia ya kuvunja sheria kwa kuvamia na kuharibu mazingira, atachukuliwa hatua kali zikiwamo kulipa faini kubwa na kifungo jela.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitoa maelekezo hayo juzi katika mkutano wa kadhara wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa.
Akizungumza na wakazi wa mji mdogo wa Namanyere, Waziri Mkuu alionywa kuwa yeyote atakayekutwa na hatia ya kuvamia na kuharibu mazingira ya msitu wa Mfili ambao ndicho chanzo pekee cha maji wilayani Nkasi, atatozwa faini ya Sh. milioni 70 sambamba na kifungo cha miaka saba jela.
Katika kuhakikisha hilo linatekelezwa, alimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda, kitabu cha sheria zinazoongoza katika kuwachukulia hatua watakaobainika kufanya uharibifu katika chanzo hicho cha maji.
Majaliwa alisema mkuu wa wilaya akishindwa kuwachukulia hatua ikiwamo kuwaondoa wavamizi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria naye atawajibishwa.
Alisema maeneo mengi nchini yanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kutokana na wananchi kuvamia maeneo ya vyanzo vya maji na kufanya shughuli za kibinadamu, hivyo kusababisha vyanzo vya maji kukauka.
Uvamizi wa maeneo ya vyanzo vya maji ikiwamo misitu, mito, mabwawa, mabonde na milima ni tabia iliyoshamiri katika miaka ya karibuni katika maeneo mengi nchini.
Wanaovamia maeneo hayo hawana sababu za msingi wanazozitoa, zaidi ya kisingizio cha uhaba wa ardhi, bila kujali kwamba uvamizi wa maeneo hayo una athari kubwa kwao.
Kwa mfano, siku hizi mvua hazinyeshi kwa wakati na hata zikinyesha zinanyesha kidogo na kuathiri shughuli kadhaa zikiwamo za kilimo. Hizi ni miongoni mwa changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Tatizo la tabianchi ambalo kwa sasa ni tishio kubwa kwa dunia, ni matokeo ya uharibifu wa mazingira ukiwamo uharibifu wa vyanzo vya maji.
Kwa kuwa athari hizo zinamgusa na kumuathiri kila mmoja moja kwa moja, suluhisho ni kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria dhidi ya watu wote watakaothibitika kuvamia maeneo yote ya vyanzo vya maji kwa sababu suala hilo limekuwa likisisitizwa kwa miaka mingi kupitia njia mbalimbali.
Kama alivyosema Waziri Mkuu kuhusu kutolewa kwa adhabu kali dhidi ya watakaobainika kuvamia na kuharibu vyanzo vya maji, adhabu hizo zitekelezwe katika maeneo yote nchini.
Kadhalika, kuna haja ya kufanyika kwa operesheni ya kitaifa ya kuwaondoa kwa nguvu wavamizi wote wanaoishi katika maeneo ya vyanzo vya maji na hifadhi za mazingira kwa ujumla.
Kimsingi, unahitajika uamuzi mgumu wa kukabiliana na uharibifu wa mazingira hususani wa watu kuvamia maeneo ya vyanzo vya maji na kufanya shughuli za kibinadamu kama kilimo, malisho ya mifugo na nyingine.
Mwaka 2006 Serikali ilichukua hatua madhubuti ilipoamua kutekeleza operesheni kubwa ya kuondoa makundi ya mifugo katika eneo la Ihefu, mkoani Mbeya. Uamuzi huo ulifanywa kutokana na kiwango kikubwa cha uharibifu wa mazingira katika eneo hilo ambalo ni chanzo cha maji kwa maeneo mengi na kusababisha kupungua kwa maji katika maeneo kadha likiwamo bwawa la Mtera.
Sisi tunaona kuwa operesheni kama ya Ihefu inapaswa kutekelezwa sasa kutokana na kiwango kikubwa cha uharibifu wa mazingira unaotokana na kasi kubwa ya wananchi kuvamia vyanzo vya maji.










