Itakumbukwa marafiki na washirika wa Mwalimu wa awamu ya kwanza ni wale aliokutana nao wakati TANU inaanzishwa hadi uhuru kupatikana, ikiwa ni pamoja na Rashidi Kawawa, Amir Jamal, Pius Msekwa, George Kahama, Paul Bomani na Timothy Apio.
Maswahiba wengine wa kundi la pili ni pamoja na John Malecela, Cleopa Msuya na Benjamin Mkapa ila tofauti ni kuwa Mkapa awali alikuwa mmoja wa wanafunzi bora wa Nyerere wakati akifundisha Pugu Sekondari.
Licha ya makundi haya siyo tofauti sana kiumri, kisiasa yalikuwa na tofauti ya wazi kwani waliokuwapo miaka ya 1950 waliingia madarakani wakiwa vijana zaidi na wale wa baadaye ilibidi wangoje kiasi, kupata nafasi zilizo wazi. Hivyo walianzia katika ngazi za utawala ingawa kimsingi zilikuwa ni za juu, wakaingia serikalini miaka ya 1970.
Mwaka 1977 Mkapa aliingia serikalini akiwa amepitia nafasi tofauti kama msaidizi wa karibu wa Mwalimu hasa katika masuala ya habari, akianzia uhariri Redio Tanzania, gazeti la The Nationalist, Standard ambayo leo ni Daily News. Shirika la Habari -SHIHATA na mwishowe Mwandishi na Msemaji Ikulu.
Alipoingia madarakani mwaka 1995, baadhi ya wachambuzi hasa nchi za nje wakaanza kusema 'mwanahabari aukwaa urais Tanzania,' wakasahihishwa na mwanahabari mkongwe Jenerali Ulimwengu, aliyefanya kazi kwa muda mfupi na Mkapa akiwa bado magazetini.
Anafafanua katika makala 'The East African' kuwa Mkapa hakuwa mwanahabari wa kawaida, 'he was always the boss,' yaani alianzia uanahabari juu kileleni na kubakia huko au kupanda juu zaidi. Hivyo pamoja na kuwa hulka ni hisia za mtu binafsi ni kweli kuwa makada waliotoka vyuo vikuu wakati huo hawakupata muda wa kunyenyekea, walianza moja kwa moja pale juu, kubaki hapo maisha yao yote serikalini.
Moja ya maeneo yaliyomsaidia Mkapa kukua na kufikia ngazi za juu ni umahiri wake wa kuzungumza Kiingereza, uliomwezesha kumwelewa Nyerere kwa kina wakati washirika au aliokuwa anafanyao nao walikuwa wagumu, alilazimika kuanzia katika uwanja mpana zaidi, kwa mfano itikadi ya mapinduzi katika Azimio la Arusha au Mwongozo wa TANU.
Mkapa hakuhitaji kuelezewa kwa kina nini tofauti ya 'uhuru' ambayo ni fikra ya msingi ya Mwalimu, na mapinduzi. Wateule wa Mwalimu katika nafasi ya uwaziri wa mambo ya nje, alipoondoka Oscar Kambona, walikuwa wanakwama hapo, wakijichanganya hasa kwenye hadhara za kimataifa.
Walibakia mawaziri wa nchi kutoka 1967 hadi 1977 alipoingia Mkapa akiwa kama waziri kamili wa Mambo ya Nje.
Kuna kibwagizo kingine kinachoweza kutoa picha ya urais wa Mkapa ulipotokea, kuwa hata wale waliomtangulia serikalini awamu ya kwanza, walishakiri wakati fulani kuwa ndiyo kiongozi wao ila hawakujua kuwa ndicho wanachokifanya.
Hadithi iliyowahi kuelezwa na waliokuwa karibu na watawala nyakati za awamu ya pili zilisema kuwa mwaka 1980, baada ya vita na Iddi Amin wa Uganda halafu kukawa na hali ngumu ya uchumi, kundi la mawaziri likamtaka Mkapa kumweleza Mwalimu umuhimu wa mabadiliko kwani Ujamaa na Kujitegemea ulionekana unaikwamisha nchi.
Mwalimu inasemekana alimshangaa Mkapa kwa kuwasilisha maoni yale, akamuunganisha nayo, akamtoa uwaziri akampeleka ubalozini ng'ambo. Ina maana kuwa mwaka 1995 wakati wa kutafuta mrithi wa Ali Hassan Mwinyi, aliyechukua nchi baada ya Nyerere suala hilo lilikuwa limeshafungwa, kwani mawaziri wa nyakati zile ambao wengi waliingia miaka si chini ya 15 kabla ya hapo walikuwapo katika kundi lililomtuma Mkapa awawakilishe kwa Mwalimu.
Mkapa akakinywea kikombe hicho, akaubeba msalaba wake akaondolewa serikalini, ila akawa amethibitisha ujasiri na uwezo wa kusikiliza wengine, na kutumika hata katika kupeleka ujumbe hatarishi kwa mkuu wa nchi.
Hivyo yale maneno eti Mkapa aliinuliwa tu na Nyerere, ni kijana wake hayatoshi, ni lazima kukumbushia wenzake walivyomtwika uongozi, l980.
Eneo jingine ambalo unaweza kusema linaendana na hilo ni jinsi ambavyo ukaribu wake na Mwalimu na usomi au udiriki wake binafsi ulivyomweka rais huyo mstaafu katika nafasi ya urais.
Waliomfahamu kwa uthubutu wake katika diplomasia na hata kisa hicho cha 1980 walitazamia kuwa amejengeka kiasi cha kufanya maamuzi yake mwenyewe, kile kinachoitwa 'maamuzi magumu.'
Ila waliomfahamu kwa historia pana zaidi ya kuwa mwanafunzi wa Nyerere na msaidizi wake wa karibu muda wote akiwa madarakani waliamini atakuwa mtu sahihi kusimamia maadili, misingi, mafundisho ya Mwalimu kwa jumla.
Ndiyo hapo unapata mihimilii ya uthubutu na vile vile udhaifu wa awamu ya tatu, kuendesha farasi wawili kwa wakati mmoja, kusimamia itikadi ya CCM kwa maeneo mengi, makada na wengi kati ya wasomi wakitaka ajitenge na hulka ya 'soko holela' ya awamu ya pili.
Hilo alilifanya kwa ufanisi kwa kuunda mifumo ya usimamizi wa uchumi na kuteka itikadi ya wafuasi wa Mwalimu alipolikaba koo 'soko holela.'
Isitoshe akawakirimu watawala serikalini kwa kuwaruhusu kupanga walichotaka, kwa mfano kulinganisha mishahara ya wataalamu wa ndani mashirika ya umma na wanaotoka nje, hivyo mkurugenzi mkuu au mtendaji wa mashirika kama TANROADS, Shirika la Maendeleo ya Petroli TPDC, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari kwingine akawa anatazamia Shilingi milioni 12 na baadaye kupanda hadi milioni 40.
Rais wa awamu ya tano ni 'mwanae' wa kisiasa, ndiye John Magufuli, aliyeufumua kwa kiasi si kidogo mtindo huo, licha kutokuwapo na uwazi, na si rahisi kusema ni kwa kiwango hali ya awali imerudi. Japo unaweza kusema kuwa mfumo aliouweka Mkapa ndiyo ulikuwa unawafaa zaidi watawala serikalini ila ukajenga hisia za chuki, watu wakiona wakubwa wanafaidi kupita kiasi, wanaanza kutimkia upinzani kuleta mabadiliko.
Alijitahidi vilevile kuendana na hisia za chama tawala ambacho hakijawahi kufikiria kuachia ngazi za utawala kupitia sanduku la kura, licha ya kuwa uwezekano huo ulikuwa wazi zaidi kwa upande wa Zanzibar, na hali hiyo inaelekea ilifikiwa 1995 halafu 2015.
Nyakati zote mbili kulikuwa na taarifa tata za vyombo vya habari kuhusu ujumlishaji kura na matokeo ya awali, baadhi ya wahariri wakahojiwa kwa kuchapisha au kutangaza kwenye runinga taarifa za uchaguzi za kuokoteza.
Alibaki na hisia za kusononeka kwa mfano baada ya mauaji ya waandamanaji upinzani Zanzibar Januari 2001, ila alibanwa na mfumo, akawa mkali akiulizwa maswali. Alikiri kuteswa na tukio hilo katika kitabu cha kumbukumbu yao maisha yake ila msingi wake asingeweza kuujutia.
Akitangaza kifo cha Mwalimu Oktoba 14, 1999, pamoja na mambo mengine, Rais Mkapa alisema 'baada ya kuondoka Mwalimu, wale tulioachiwa hatamu za uongozi wa nchi, tutaulinda Muungano kwa nguvu zote." Hapakuwa na nafasi ya kufanya kinyume.










