Wagunduzi wanaodhihirisha jinsi plastiki ilivyo mali

26Jul 2023
Christina Mwakangale
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wagunduzi wanaodhihirisha jinsi plastiki ilivyo mali

WAKATI wowote Tanzania inaweza kuanza kujivunia matunda ya ubunifu na ugunduzi unaoendelezwa na kukuzwa na viatamizi (incubators) katika vyuo vikuu kikiwamo cha Dar- Es- Salaam.

 

Ndivyo unavyoweza kusema ukifuatilia baadhi ya kazi za wagunduzi wanaosimamiwa na UDSM na kulelewa na kiatamizi chuoni hapo kama wanavyoeleza wagunduzi wake wanafunzi wa uhandisi, Daud Nzunda na Laetus Buberwa.

Wawili hawa wamebuni namna ya kuzalisha umeme kwa kutumia uji au kimiminika  kinachopatikana baada ya kuyeyusha chupa za plastiki zilizotumika na kutupwa mitaani.

Wakizungumza na Nipashe kwenye maonesho ya Sabasaba, jijini Dar es Salaam wanasema wanazitumia taka hizo ambazo haziyeyuki ardhini wala kuoza kwa urahisi, kuzalisha nishati hiyo, kwa matumizi tofauti, kama kuchaji vifaa vya kielektroniki.

Nzunda, anayesomea uhandisi wa bayoteknolojia ambayo ni taaluma zinazohusisha sayansi na uhandisi kwa kutumia  viumbe hai, seli, tishu na sehemu zao mbalimbali kupata  bidhaa na huduma bora na zenye ufanisi zaidi ili kurahisi maisha ya binadamu.

 

Anasema: "Sisi wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hapa  Sabasaba tumekuja na ubunifu wa mashine inayotengeneza umeme wa matumizi ya nyumbani, lakini gesi ya kupikia ikitumia chupa za plastiki."

 

Anaongeza: "Kwa hiyo badala ya kuweka petroli au dizeli au gesi, tunatumia chupa za plastiki mashine inayozichakata kuzalisha umeme unaotumika nyumbani."

MWANZO WA UBUNIFU

Nzunda anasema wazo la kuunda mashine hiyo linakuja baada ya kubaini tatizo la kupatikana nishati umeme, hasa kwa ambao hawajafikiwa na huduma hiyo. Lakini ni katika kutafuta mbinu ya kutunza mazingira, kwa kuwa chupa za plastiki hutupwa ovyo na kuharibu mfumo wa ekolojia angani, juu na chini ya ardhi pamoja na ndani ya maji.

 

Matumizi makubwa ya plastiki yameleta madhara mengi kwa mazingira, kwanza inachukua muda mrefu kuoza, inachafua mazingira kwa njia nyingi za uzalishaji wa gesi chafu, zichafua maji, kuharibu  maisha  ardhini, athari kwa viumbe hai na hewa inapo kutoa kemikali hatari na sumu ambazo zina madhara kwa afya ya binadamu na viumbe hai pale zinapochomwa.

"Tumetafakari hiyo baada ya kuona kwenye jamii yetu kumekuwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira kutokana na taka za plastiki kusambaa mitaani lakini pamoja na hizo changamoto za umeme. Tumebuni mashine hii ambayo inatengeneza umeme kwa kutumia vitu hivyo ambavyo vinapatikana karibu kila mahali,” anaongeza.

Mashine hiyo, inafanya kazi pale unapochukua chupa za plastiki ukaziwasha moto zinapoyeyuka na kuwa kimiminika, mashine  inakichakata kuzuia kisigande.

 Anaongeza kuwa kisha kinaingizwa kwenye mota ndani ya injini, badala ya kutumia petroli au dizeli kinakuwa ndiyo nguvu ya mashine hiyo.

 

Anafafanua zaidi kwamba, kama injini zinazotumia dizeli au petroli ndivyo mashine hiyo inavyofanya kazi ikitumia uji wa plastiki, kwa ajili ya kutengeneza umeme na pia ni kizito kidogo ikilinganishwa na petroli au dizeli.

 

Nzunda anaeleza uwezo wa mashine hiyo akisema, kwenye injini wameifanyia maboresho ili iendane na mtambo huo. Aidha, ina  uwezo wa kutoa umeme wa kilowati 1.5 au wati 1,500 ambayo inaweza kitumika kuwasha taa, feni, televisheni, redio na televisheni.

 

Mhandisi huyo anabainisha kuwa kama anatokea mwenye kuhitaji mfumo wa umeme mkubwa, mteja huyo wanamtengenezea mashine kulingana na mahitaji yake.

 

Anasema uwezo wa mashine hiyo ni kutoa  volti 24 lakini pia unaweza kuitumia kuendesha vifaa vinavyotumia umeme jua au  sola.

Kadhalika, anasema mashine hiyo inatumia kilo moja ya plastiki na ina uwezo wa kutengeneza umeme ambao utatumika kwa takribani saa sita, uwezo wake ni kubeba kilo15 na kuwa chanzo cha umeme wa saa 90 takribani siku nne.

 

"Kwa hiyo ukiwa na kilo 15 hapo inakuwa na muda mrefu sana. Hii mashine hata kama matumizi ni makubwa utapata nishati ya uhakika. Tumetengeneza itumike pale ambao umeme wa TANESCO a unakatikatika, ukikatika unaitumia mashine au LUKU imemalizika mahine hii inakufaa, au kama kuna mvua umeme wa sola unakwama kwa vile jua halipatikani la kutosha. Mashine hii itakufaa pia," anaeleza Nzunda.

MAJARIBIO

Msomi huyo anasema kwa kuwa mashine hiyo ni ubunifu mpya, lazima kuifanyia zaidi majaribio na kamba wameanzia majaribio chuoni hapo na baadhi yanafanyika nje ya UDSM ili kubaini utendaji kazi wake kiuhalisia na kiufanisi.

 

"Kwa sasa hivi tumeanza majaribio na tunaifanyia kazi maeneo mbalimbali kama vile kwenye migahawa ya chakula chuoni hapa cafeteria, jirani Changanyikeni pia mitaani tunazijaribu River Side Ubungo," anasema Nzunda.