Mabaharia wataka udhibiti uchafuzi Ziwa Victoria 

25Jun 2023
Vitus Audax
MWANZA
Nipashe Jumapili
Mabaharia wataka udhibiti uchafuzi Ziwa Victoria 

MABAHARIA wameiomba serikali kuweka mkazo wa kudhibiti uchafuzi katika Ziwa Victoria unaotokana na taka zinazotiririshwa kupitia Mto Mirongo.

Mabaharia hao walitoa kilio chao katika Maadhimisho ya Wiki ya Mabaharia Duniani kwa serikali jana, wakati wakifanya usafi kwenye mto huo unautiririsha maji yake kwenda Ziwa Victoria.

Licha taka ngumu na nyepesi kuua mazalia ya viumbe hai majini wakiwamo samaki, husababisha pia uharibifu wa mitambo ya vyombo vya usafiri wa majini na kuwaingizia hasara wawekezaji ziwani humo.

Mabaharia hao walisema ili kudhibiti tatizo hilo kuna umuhimu wa serikali kuweka miundombinu ya taka na sheria kali zaidi.

Kaimu Meneja Mafunzo na Utoaji Vyeti kwa Mabaharia, Lameck Sondo, alisema kutokana na taka hizo kuwa tatizo, serikali inatakiwa kutenga bajeti na kuweka vifaa vya utupaji taka katika maeneo mbalimbali yanayozunguka mito inayotiririsha maji yake ziwani ili kupunguza uchafuzi huo.

“Tumebaini uwapo wa taka nyingi zikielekea ziwani na zikifika huko ni hatari kwa vyombo vyetu. Hatua hii itasaidia watu wapate pahala pa kutupa taka zao ili magari ya taka yakipita izichukue," alisema Sondo.

Mkuu wa Uzamiaji na Uokozi Kikosi cha Magendo Zanzibar KMKM, Najima Kalekwa, alisema kuna uhitaji wa kuwekwa kwa sheria ndogo katika maeneo yanayozunguka vyanzo vya maji ili kudhibiti uchafuzi ambao mara nyingi unasababishwa na shughuli za kibinadamu.

“Hali siyo nzuri katika vyanzo vya maji na hali hii inahatarisha zaidi shughuli za kiuchumi ukiwamo usafirishaji. Serikali kupitia sekta ya uhifadhi wa mazingira, inatakiwa kudhibiti uchafuzi huu kwa hali yoyote," alisema.

Kapteni Mande Mangapi, Nahodha wa Vivuko vya Kampuni ya Kamanga vinavyofanya safari zake katika Ziwa Victoria, alisema mara kadhaa wanafanya marekebisho ya vyombo vyao hususani katika maeneo ya propela ambazo husomba taka ngumu zinazosababishwa na uchafuzi ziwani humo.

“Nina imani kuwa hizi sheria ndogondogo zikiwekwa na kufuatiliwa, hakutakuwa na uchafuzi wa aina hii unaosababisha hasara kwa wawekezaji," alisema.

Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Hamidu Said, ambaye pia ni Diwani Kata ya Mirongo, alisema halmashauri hiyo imekuwa ikitenga bajeti kwa ajili ya kufanya usafi katika mito inayotiririsha maji yake Ziwa Victoria, lakini watu wanaendeleza uchafuzi kwa kificho kwenye mito hiyo.

Alisema utupaji taka ovyo siyo tu katika mito na maziwa bali, katika maeneo yote ambayo yamezuiliwa.

Pia, aliwataka wananchi kufuata utaratibu wa kuweka taka hizo katika maeneo yaliyotengwa ili zichukuliwe na magari maalum ya kuzolea taka.