Wasiowajibika Wizara Kilimo kupelekwa kusoma magazeti

26Jun 2023
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Wasiowajibika Wizara Kilimo kupelekwa kusoma magazeti

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema ugumu uliopo katika mfumo wa kuwafukuza kazi watumishi wa umma ndiyo chanzo cha wengi wao kufanya kazi kimazoea na kushindwa kuwajibika ipasavyo kuisaidia serikali kutatua kero mbalimbali za wananchi.

Amesema atakachofanya kwa watakaoshindwa kutekeleza majukumu, ni kuwapeleka jengo lililopo karibu na Bunge ambako watakuwa wanasoma magazeti na kama serikali itaendelea kuwalipa mishahara, iendelee.

Bashe alitoa kauli hiyo juzi jijini humo alipokuwa akihutubia wajumbe wa mkutano wa 13 wa wadau wa kahawa uliofanyika kwa siku mbili.

Alisema moja ya sababu za serikali kushindwa kufikia azma yake ni watumishi wake kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Hadi umfukuze kazi mtumishi wa umma ni kazi sana, kuna mlolongo mrefu sana, na mimi sina uwezo huo sijapewa mamlaka hayo, ila mimi nitakachofanya kwa mtu yeyote ambaye nitaona anashindwa kutekeleza majukumu yake, kuna jengo lipo pale Fifty Six, nitawapeleka waende kusoma magazeti. Kama serikali itaendelea kuwalipa mishahara, iendelee kuwalipa,” alisema.

Bashe alisema inashangaza kuona mtumishi wa umma anaingia kazini saa mbili asubuhi na kuondoka saa tisa alasiri bila kujali kama amekamilisha kazi zake wakati mkurugenzi wake anakaa ofisi hadi saa tatu usiku.

Kutokana na hali hiyo, aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuwaondoa maofisa kilimo wote waliopo mjini na kuwapeleka vijijini.

“Inabidi waondoeni wote waende vijijini kama ambavyo walivyo walimu, leo hii tumegawa pikipiki lakini bado tunaziona mjini hadi wakati mwingine tunatamani hata tuzikusanye zile pikipiki zetu,”alisema.

Bashe pia aliipongeza Bodi ya Kahawa kwa kufanikisha kuongeza mavuno ya zao la kahawa kwa mwaka hadi kufikia tani 45,000 ikiwa ni kiasi kikubwa kufikiwa tangu Tanzania kupata uhuru.

Alisema ili kuendelea kuimarisha zao hilo, serikali imepanga kuja na mkakati wa kuhamasisha matumizi ya kahawa ya ndani ili kuwa na uhakika wa soko.

“Nchi ya Ethiopia ambao ndiyo wanaongoza kwa uzalishaji wa zao hili Afrika, kinachowasaidia ni matumizi ya ndani. Sisi tunapanga kuhamasisha matumzi ya ndani ili hata soko la nje likiyumba tutaendelea kuwa na uhakika wa kuuza kahawa yetu,” alisema.

Alisema tayari wameshaandika barua kwa vyuo vikuu 15 na viwili kati ya yake vimejibu na kutoa ruhusa ya kuanzisha migahawa ambayo itakuwa inahamasisha matumizi yake vyuoni.

“Kusafirisha kilo moja ya kahawa nje ya nchini ni takribani dola nne lakini kuingiza kilo moja ya kahawa ambayo tayari imeongozwa thamani ni dola takriban 20, hivyo ipo haja na kuwa na soko la uhakika la ndani kwanza,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa (TCB), Primus Kimaryo, alisema zao hilo linazidi kuimarika kila siku kutokana na uwezeshaji mkubwa wanaoupata toka serikalini na kwa wadau wa zao hilo.

Alisema kutokana na mikakati iliyowekwa na bodi hiyo, wanatarajia kufikia uzalishaji wa tani 300,000 wa zao hilo katika msimu wa kilimo wa 2025/26 na kuongeza uzalishaji wa miche milioni 20 ya kahawa kwa mwaka ili kufikia mahitaji ya wakulima.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kahawa nchini (TaCRI), Deusdededit Kilambo, alisema kuna kazi ya kufanya ili Tanzania iingie katika ushindani Afrika na nje ya bara hilo.