Sababu ya vurugu hizo ni mvutano baina ya wafuasi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, na kundi la wanachama na wafuasi wa uongozi wa chama hicho.
Wafuasi wa Prof. Lipumba walitaka aruhusiwe kuingia katika uchaguzi huo na kupigiwa kura kama mgombea wa uenyekiti huku kundi hasimu likiruhusu kiongozi huyo aingie katika ukumbi, lakini likapinga wafuasi wake wasiingie.
Ni tukio ambalo lilionyesha kutishia amani na utulivu katika eneo la mkutano huo, baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura iliyoitishwa kuamua hatma ya Profesa Lipumba.
Vurugu hizo zilimfanya Mwenyekiti wa uchaguzi huo, Julius Mtatiro, kutangaza kuahirisha uchaguzi huo kutokana na watu waliodaiwa kuwa wafuasi wa Prof. Lipumba kuvamia na kuanza kurusha viti, chupa na milingoti.
Sisi tumelichukulia tukio hilo kuwa ni ukosefu wa ustaarabu na uvumilivu miongoni mwa waliohusika.
Tunasema kuwa ni kukosekana kwa ustaarabu na uvumilifu kutokana na kuamuliwa kupiga kura ya kuamua hatma ya Lipumba kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo wa kuwapata mwenyekiti wa taifa wa chama hicho na makamu wenyeviti wawili wa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Wajumbe wa mkutano huo walielekezwa kupiga kura kuamua hatma ya Prof. Lipumba, ambaye Juni 13, mwaka huu aliandika barua ya kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu wa Agosti 5, mwaka jana.
Kutangazwa kwa uamuzi wa kura hizo wa wajumbe 476 kumkataa Pof. Lipumba kwenye nafasi ya uenyekiti na 14 kuunga mkono kurudi kwake, ndiko kulikozua tafrani hiyo.
Hata hatua ya Prof. Lipumba kwenda katika mkutano huo akiongozana na wafuasi wake waliokuwa wamevaa mavazi yenye maneno ya kumuunga mkono, zilionekana kuwa uchokozi wa dhahiri dhidi ya wafuasi wa uongozi wa chama hicho.
Hayo yote yangeweza kuepukika kama wahusika wangeheshimu demokrasia, kuheshimiana, kuvumiliana na kufuata taratibu badala ya kila upande kuuonyesha mwingine ubabe.
Kwa mfano, chama kilitakiwa kuweka wazi mapema ikiwamo kumpatia mhusika taarifa kuwa ajiandae kupigiwa kura na wajumbe, kabla ya uchaguzi kuanza.
Kwa upande wake, Prof. Lipumba angewasiliana na chama chake akiomba kwenda kutoa utetezi wake siku kadhaa kabla ya kufanyika kwa mkutano huo ili kumuidhinisha kuwa mgombea au kumkatalia, badala ya kwenda katika ukumbi wa mkutano akifuatana na makundi ya wafuasi wake wanaomuunga mkono huku wakishinikiza arejeshwe katika nafasi yake ya uenyekiti wa chama.
Hakuna upande tunaoutetea kuhusiana na vurugu hizo, isipokuwa tumeshangazwa tukio hilo kufanywa na chama ambacho ni kikubwa na kilichokomaa.
Tunavihimiza vyama vyote vya siasa kuhakikisha kwamba vinaheshimu demokrasia na kufuata taratibu zake badala ya kufanya uamuzi kutokana na shinikizo kutoka kwa wanachama na wafuasi wenye mihemko.
Licha ya kwamba demokrasia nchini hususani ndani ya vyama vya siasa bado changa, lakini taratibu zifuatwe katika kufanya uamuzi.
Vyama vikifanya uamuzi kwa kufuata mihemuko na shinikizo kutoka kwa wanachama na wafuasi, uamuzi huo hautakuwa wa bisara na utakuwa ni wa kukiuka sheria, kanuni na taratibu.










