Mafanikio hayo ni kufuatia mpango wa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Serikali ya Marekani (PEPFAR) wa mapambano dhidi ya maambukizi ya Ukimwi kwa kushirikiana na washirika wake ikiwepo Shirika la Walter Reed Army Institute of Research – Department of Defense (WRAIR-DOD).
Mpango huo sasa unatimiza miaka 20 tangu uanze kutekeleza afua mbalimbali za mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa kuwezesha upatikanaji wa dawa za ARV bure, vifaa tiba, elimu ya kujikinga maambukizi ya VVU, magonjwa ya ngono, tohara na elimu kwa vijana rika balehe.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera anasema wamekuwa wanufaika wa PEPFAR katika kutekeleza afua mbalimbali za kupambana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ambazo zimesaidia kupunguza maambukizi.
Anasema licha ya Mkoa wa Mbeya kuwa miongoni mwa mikoa ambayo ina kiwango kikubwa cha maambukizi, ikiwa ni asilimia 9.3, ikilinganishwa na wastani wa kitaifa ambao ni asilimia nne tayari, wanatarajia kiwango hicho kupungua kutokana na juhudi zilizofanyika za kukabiliana na maambukizi hayo.
“Mkoa umefaidika na mradi wa PERFAR, umeboresha huduma za maabara, mafunzo ya wafanyakazi na kuanzisha programu ambazo zinaokoa makundi na vijana rika balehe na wanawake walio kwenye mazingira magumu.
.jpg)
“Hadi sasa Mkoa wa Mbeya unajivunia kufikia malengo ya mapambano ya VVU ambapo kwa sasa tumehakikisha asilimia 95 ya watu wanaoishi Ukimwi wanajua hali zao, asilimia 95 ya waliogundulika wako kwenye matibabu na asilimia 95 ya wale wanaopata matibabu ya kufubaza virusi vya imesaidia kupunguza kasi ya maambukizi katika kufikia malengo ifikapo 2030,” amesema Homera.
Mshauri Mwandamizi wa Kinga kutoka Taasisi ya Utafiti ya Jeshi la Walter Reed - Idara ya Ulinzi (WRAIR-DOD) Ubalozi wa Marekani nchini, Dk. Dk Alick Kayange, anasema wanashirikiana na serikali kuhakikisha huduma za WAVVU zinakuwa endelevu ili kuokoa maisha ya watanzania.
Anasema wanajivunia kuona dawa za kufubaza makali ya Ukimwi zinapatikana kwenye vituo vyote nchini vya kutolea huduma za Afya na kuhakikisha hakuna upungufu ili wananchi waendelee kupata matibabu na kupunguza maambukizi.
“ Wakati PEPFAR inaanza shughuli zake hapa nchini mwaka 2003, watu chini ya 1000 pekee ndio ambao walikua wamemudu gharama za kupata dawa za kufubaza makali ya virusi vya ukimwi kwa sasa tuna watu zaidi ya millioni 1.5 ambao wapo kwenye matibabu na wameokoa uhai wao vilevile vifo vitokanavyo na Ukimwi vimepungua kwa asilimia 76 kutoka watu 120,000 mwaka 2003 hadi watu 29,000 mwaka 2021,” anasema Dk. Kayange.
Ameongeza kuwa hadi sasa, Tanzania imepokea dola za kimarekani sh bilioni 6.6 sawa na trilioni 15 za kitanzania kama msaada wa kutekeleza program mbalimbali za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa miaka 20 sasa.
.jpg)
Msaada huo umesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya VVU ambapo mwaka 2003, serikali ya Marekani ilitangaza mfuko wa misaada ambao lengo lake lilikuwa kudhibiti janga la VVU kwa kuzuia maambukizi mapya na kupunguza kiwango cha vifo katika zaidi ya nchi 50 ikiwamo Tanzania.
Douglas Kisunga(70)mkazi wa Jiji la Mbeya, anasema aligundukia kuwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi tarehe 31 Januari 1993 baada ya kupima katika Hospitali ya Rufani ya Kanda Mbeya baada ya kuugua maradhi mbalimbali kwa muda mrefu.
Anasema baada ya kugundulika maisha yake yalibadilika na kuwa mtu wa hofu kwamba muda wowote anaweza kupoteza maisha lakini baada ya kupata ushauri nasaha aliikubali hali hiyo na kuanza kutumia dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi.
Anasema ni zaidi ya miaka 20 sasa tangu aanze kutumia ARVs na kwamba afya yake ni imara na amekuwa akitoa ushuhuda kwa wananchi wengine ambao wanaficha hali zao ili kujitokeza kupima na kutumia dawa ili kuokoa maisha yao kwa madai kuwa kupata ukimwi sio mwisho wa maisha.
“Nawashukuru sana PEPFAR kwa kufadhili miradi mbalimbali ya Ukimwi hapa nchini, mmetusaidia sasa kuimarisha afya zetu kwa sababu miaka ya nyuma upatikanaji wa dawa ulikuwa mgumu hivyo watu wengi walipoteza maisha, sisi tuliobahati tunashukuru dawa zilianza kupatikana bure mpaka sasa nimekuwa mfano kwa wengine kwani tangu nigundulike nimekuwa mfuasi mzuri wa dawa na afya yangu ni imara,” anasema Kisunga.
Jane Mwakajumba (41) mkazi wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, anasema mwaka 2005 aligundulika kuwa na maambukizi ya Ukimwi, aliamua kupima kutokana na kuugua kwa muda mrefu baada ya kuolewa na mwaka 2003.
Anasema baada ya kupima mume wake ambaye hakuwa na maambukizi alimnyanyapaa na kumfukuza kurudi kwao, ambapo alipata faraja kwa mama yake akimsisitiza kuzingatia ushauri wa daktari kuhusu matumizi sahihi ya dawa.
Anadai ufuasi mzuri wa dawa ulimsaidia na kurejesha afya yake hali iliyosababisha mume wake kuanza kurejesha upendo na kumtaka arudi nyumbani kulea familia bila kujali hali ya maambukizi aliyonayo.
Anaeleza kuwa mume wake alikubali kuendelea kuishi na mkewe na kubeba jukumu la kumkumbusha muda wa kumeza ili kujikinga na maambukizi ya Ukimwi kwake.
“ Baada ya kugundulika kuwa na maambukizi nilimjulisha mume wangu ambaye hakukubaliana na hali hiyo kwani yeye hakuwa mwathirika, nilipata manyanyaso na kuamua kurudi nyumbani kwetu, baada ya muda nilirudi kwenye hali yangu, ndipo mume wangu akaanza kuona wivu akidai nimepata mwanaume mwingine, akanirudisha tukaendelea kuishi wote, huku tukichukua tahadhari na kumlinda yeye asipate maambukizi kwa sasa nafurahia maisha na familia yangu,” anasema Jane.










