Ni ajenda ya mafunzo inayoendana na Dira ya Maendeleo Endelevu kuelekea mwaka 2030, Dk. Kimaro akiwa na simulizi zaidi kwamba aliporudi nchini mwaka 2019, akaamua kusafiri maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kilimanjaro na Manyara kufanya utafiti wa utunzaji viumbe hai na mazingira.
Anautaja ni utafiti uliomsaidia kubaini kuna viumbe hai wameanza kutoweka na wengine wapo hatarini, sasa kunahitajika utafiti zaidi kuangalia mahali kuliko hatarini zaidi, wanyama wanatoweka au wameanza kutoweka, kufanyike mkakati mpya wa kuhifadhi viumbe, kulingana na maeneo wanayoishi.
“Wakati nafanya utafiti niligundua kuwa, kumbe kuna vitu ambavyo vinaweza kupotea duniani, kutokana na hali ya mazingira ya tabia nchi na baadae nilikuja na wazo la kuandika kitabu ambacho kitaonyesha viumbehai ambao wapo hatarini kutoweka duniani, lakini kwa kushirikisha watu mbalimbali,” anasema.
Dk. Elibahati Kimaro, anasema utafiti wake katika mkoa Manyara na Kilimanjaro, aligundua kuwapo miti laini inayoweza kupasua miamba na mawe magumu, ikaota na hatimaye kuzalisha msitu.
Anataja utafiti wa Manyara, kwamba kuna aina ya miti wananchi wanaweza kuotesha kwenye maeneo kame, kuwezesha kuwapo uoto wa asili.
Pia, mkoani Kilimanjaro katika kijiji cha Manio, alikokulia anasema kagundua alichokiona miaka ya nyuma, kulikuwapo ndege wengi aina mbalimbali na wanyamapori kama vile mbega na kima.
Anasema, hivi sasa baadhi ya wametoweka mahali hapo. Dk. Kimaro anaendelea: “Wakati nafanya utafiti katika kijiji chetu cha Manio kwanza niliangalia kitu gani kilikuwapo wakati nikiwa mdogo, sasa hivi kuna nini, tofauti ni nini?”
“Hatimaye nikagundua kuwa kuna vitu vingi vimetoweka katika kijiji chetu ikiwamo ndege na wanyamapori,” anafafanua.
Hapo ndipo anafafanua dodosa yake kwamba ikamfanya agundue, si kijijini kwao pekee ndio viumbe wametoweka, bali kwingineko zaidi ya Kilimanjaro na Manyara, kuna shida hiyo.
MATOKEO RIPOTI
Anasema, akatuma matokeo ya utafiti chuoni India alikosoma, ripoti anayoitaja ikawavutia wafadhili wake ambao ni serikali ya India na wakaamua kumfuatilia akiwa nchini Tanzania na mwisho wake wakampatia tuzo ya udaktari wa falsafa wa heshima.
Dk. Kimaro anataja kilichompaisha akagundua miti iliyoweza kupasua miamba na mawe magumu na kuweza kufanya mazingira yakawa mazuri katika eneo hilo katika mkoa wa Manyara.
Hapo mtaaluma huyo anasema, baada ya hapo akaja na wazo la kutengeneza kitabu kinachoonyesha viumbe hai vilivyo hatarini kutoweka duniani, akiwashirikisha wadau mbalimbali.
Ni katika orodha hiyo, anawataja watokao taasisi mbalimbali, wanafunzi vyuo vikuu na vya kati, pia sekondari kutoka nchi mbalimbali, ikiwamo Tanzania.
Rai yake ni kwa Watanzania kutumia fursa za kutafiti au kuandika taarifa za viumbe hai hatarini kutoweka duniani wanakoishi, pia kutoa wazo cha kufanyika, kunusuru na kuhifadhi viumbe hai, sambamba na kurejesha makazi yao endelevu kwa vizazi vijavyo.
“Utafiti huu ni shindano ambalo lipo wazi kwa watu wote ulimwenguni ikiwamo Tanzania, kufanya utafiti. Watu wanaoishi katika maeneo ambayo yapo karibu na misitu, nchi kavu, bahari, maziwa, mito na bonde la ufa wanaweza kushiriki katika shindano hili,” anasema.
Shindano hili limeandaliwa na shirika lisilo la kiserikali linalojulikana kama ‘Kilimanjaro Field and Class of Environment Protection Initiative (KEPI).
Anasema taarifa zote zitakazopatikana kutoka kwa waliofanya utafiti au kuandika ripoti kulingana na maeneo wanakoishi zitatumika kutengeneza kitabu na kinatarajiwa kusambazwa kwenye taasisi za kimataifa zinazohusika na mazingira.
Lengo, ni kujua yanayotokea duniani ili wachukue hatua za kuhifadhi viumbe hai.
Pia, kitabu kinatarajiwa kusambazwa kwenye taasisi za kitafiti na wadau wengine duniani, kiuzwe na fedha zitakazopatikana, zitatumika kugharamia kupanda miti katika maeneo mbalimbali, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuwalinda viumbe hai.
Anasema, ni shindano la utafiti limenza rasmi Aprili 19 mwaka huu na mwisho wa kuwasilisha Juni 2 mwaka huu, kwa kutumia anwani ya baruapepe: kepi202061@yahoo.com au ellykimaro35@gmail.com
“Tumeamua kuja na shindano hili baada ya kugundua kuwapo mabadiliko ya tabia nchi yamesababisha viumbe hai wengi kupata changamoto ya kuishi na kusababisha changamoto kwenye mimea na wanyama,” anasema.
“Ni jukumu letu watu wote ulimwenguni ikiwemo Tanzania kufikiri kuhusu vizazi vijavyo,” anasema, akitaja shindano linalosimamiwa na vyombo vya kimataifa, pia waandamizi ngazi ya vyuo vikuu.










