Wakali 10 wa uwiano wa mabao Ulaya

22May 2023
Na Mwandishi Wetu
UINGEREZA
Nipashe
Wakali 10 wa uwiano wa mabao Ulaya

SASA tunakwenda kushuhudia Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Manchester City dhidi ya Inter Milan.

Na linapokuja suala la uwiano wa mabao kwa kila mchezo kati ya wachezaji walio na mabao 30 au zaidi, makala haya inawachambua wachezaji 10 bora zaidi.

10. Neymar (mabao 43) – Uwiano wa 0.53 kwa mchezo

Mwanasoka ghali zaidi katika historia ya mchezo huo aling’ara zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Barcelona na Paris Saint-Germain.

Neymar aliifanya timu hiyo ya Hispania kutwaa ubingwa wa Ulaya msimu wa 2014-15, akifunga mabao 10 katika mechi 12, na saba kati ya hizo akifunga kuanzia kwenye robo fainali na kuendelea.

9. Mohamed Salah (mabao 44) – Uwiano wa 0.56 kwa mchezo

Mohamed Salah alijitambulisha kwenye Ligi ya Mabingwa kule Basel, akifunga nyumbani na ugenini dhidi ya waajiri wake wa wakati huo Chelsea katika hatua ya makundi ya msimu wa 2013-14.

Mmisri huyo sasa amempita Steven Gerrard kama mfungaji bora wa muda wote wa Liverpool katika michuano hiyo ya Ulaya akiwa amefunga mabao 42.

8. Filippo Inzaghi (mabao 46) – Uwiyano wa 0.57 kwa mchezo

Filippo Inzaghi ni mshindi mara mbili wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na alikuwa mfungaji wa pili katika msimu wa 2002-03 akiwa na mabao 10.

Muitaliano huyo pia alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi katika fainali ya mwaka 2007 baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa 2-1 wa AC Milan dhidi ya Liverpool.

7. Karim Benzema (mabao 90) – Uwiano wa 0.59 kwa mchezo

Benzema ndiye mfungaji bora wa nne katika historia ya Ligi ya Mabingwa na alifunga mara 15 katika kampeni ya ushindi ya Real Madrid msimu wa 2021-22.

Mshindi huyo wa Ballon d'Or alianza kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo akiwa na umri wa miaka 17 kule Lyon dhidi ya Rosenborg ambako alifunga bao lake la kwanza.

6. Kylian Mbappe (mabao 40) – Uwiano wa 0.66 kwa mchezo

Kylian Mbappe alijitambulisha kwa mara ya kwanza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Monaco, akifunga mabao sita katika mechi tisa wakati ilipotinga nusu fainali msimu wa 2016-17.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 ameendelea kutamba pale PSG, huku hat-trick yake dhidi ya Barcelona msimu wa 2020-21 ikiwa ni kiwango chake cha kukumbukwa zaidi hadi sasa.

5. Ruud van Nistelrooy (mabao 56) – Uwiano wa 0.77 kwa mchezo

Ruud van Nistelrooy hakuwahi kunyanyua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini alishinda Kiatu cha Dhahabu akiwa na Manchester United msimu wa 2002-03 kwa kufunga mabao 12.

Mholanzi huyo pia anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao 40 kwa haraka zaidi, akifanikiwa kufunga katika mechi 45 pekee.

4. Cristiano Ronaldo (mabao 140) – Uwiano wa 0.77 kwa mchezo

Mafanikio ya Cristiano Ronaldo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya hayana kifani. Yeye ni mshindi mara tano, mfungaji bora wa rekodi akiongoza kwa asisti (40).

Mchezaji huyo alifunga mabao 17 msimu wa 2013-14 - wakati Real Madrid iliposhinda - bado ni idadi kubwa zaidi kuwahi kufungwa na mchezaji katika msimu mmoja.

3. Lionel Messi (mabao 129) – Uwiano wa 0.79 kwa mchezo

Lionel Messi amekuwa mchezaji wa kudumu katika Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu alipoanza mwaka 2005 na anashika nafasi ya tatu kwenye orodha ya wachezaji waliocheza mechi nyingi zaidi (mechi 163) nyuma ya Ronaldo na Iker Casillas.

Msimu uliofanikiwa zaidi kwa mshindi huyo wa Kombe la Dunia ulikuwa ule wa 2011-12 akiwa Barcelona, ambapo alifunga mabao 14 katika mechi 11 alizocheza.

2. Robert Lewandowski (mabao 91) – Uwiano wa 0.82 kwa mchezo

Robert Lewandowski aliiongoza Bayern Muni kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa msimu wa 2020-21 kwa kufunga mabao 15, idadi yake kubwa zaidi katika msimu mmoja.

Raia huyo wa Poland kabla ya hapo aligonga vichwa vya habari kwenye michuano hiyo akiwa Borussia Dortmund, pia, akiandikisha ushindi wa mabao manne katika nusu fainali ya 2012-13 dhidi ya Real Madrid.

1. Erling Haaland (mabao 35) – Uwiano wa 1.20 kwa mchezo

Ikiwa Haaland atadumisha kiwango chake cha kushambulia na kuepuka majeraha mabaya, atavuka rekodi ya Ronaldo ya mabao 140.

Raia huyo wa Norway ni mmoja wa wachezaji watatu pekee waliofunga mara tano kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa - wengine wawili wakiwa Messi na Luiz Adriano.