Serikali yasisitiza matumizi sahihi chanjo mifugo kukuza soko

14May 2023
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Serikali yasisitiza matumizi sahihi chanjo mifugo kukuza soko

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe amewataka wafugaji nchini, kuacha kufuga kwa mazoea na kuzingatia matumizi sahihi ya chanjo za mifugo zinazozalishwa na serikali, ili kukuza soko la ndani na nje ya nchi.

Prof. Riziki Shemdoe (katikati) akipokea maelezo kwenye maabara.

Akizungumza  jana mara baada ya kutembelea Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), jijini Dar es Salaam, Prof. Shemdoe amesema lengo la la ziara ni kujionea shughuli mbalimbali za kimaabara.

“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa fedha ambazo amekuwa akizitoa hapa kuongeza vifaa na kuzifanya maabara zetu ziwe za kisasa zaidi, mimi kama Mtendaji Mkuu wa Wizara niahidi kuendelea kuuangalia Wakala kwa jicho tofauti,” amesema Prof. Shemdoe. 

“Hili ni eneo ambalo tukiimarika zaidi hata mifugo yetu itaimarika na mifugo ikiimarika tutapata masoko mengi ya nje ya nchi,” ameongeza.

Amesema kwamba kazi kubwa inayofanywa na wakala inasaidia nchi kutambua magonjwa ya mifugo ambayo yapo nchini, ili  kuyazuia au kuyaondoa kabisa na kusaidia isiambukizwe au kupata magonjwa mbalimbali.

Sambamba na hilo, Prof. Shemdoe  ameongeza kuwa kwa miaka michache iliyopita Tanzania ilikuwa inapeleka nyama nje ya nchi tani elfu 1,000 lakini mwaka huu wa fedha unaoisha limeshavukwa lengo.

“Nimependezwa na namna mlivyojitahidi kupata Ithibati ya vipimo muhimu 10 kwa ajili ya kuhudumia wanyama wetu mbalimbali ndani ya nchi, vilevile nimependezwa na kazi inayoendelea ya uzalishaji wa chanjo. Mnazo chanjo za aina saba,nimefurahishwa na jitahada zenu za kuendelea kutafuta Ithibati za chanjo hizo ili zianze kutumika kimataifa,” amesema Prof. Shemdoe.

Mtendaji Mkuu wa TVLA, Dk. Stella Bitanyi amemshukuru Prof. Shemdoe kwa kutenga muda wake kutembelea wakala huo, kufahamu kazi zinazofanywa na kujionea shughuli mbalimbali za kimaabara.