Samia: Nguzo kuu imeondoka

15May 2023
Halfani Chusi
DAR ES SALAAM
Nipashe
Samia: Nguzo kuu imeondoka

RAIS Samia Suluhu Hassan ameongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliyefariki Mei 12 mwaka huu baada ya kuugua kwa muda mfupi, akisisitiza "nguzo kuu imeanguka".

Rais Samia Suluhu Hassan akiaga mwili wa aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, katika Viwanja vya Karimjee Dar es Salaam jana. PICHA: IKULU

Akitoa salamu za rambirambi jana jijini Dar es Salaam wakati wa kuuaga mwili wa Membe, Rais Samia alimtaja alikuwa 'kaka wa karibu' aliyependa kufundisha na kutoa maarifa yake kwa wengine, muungwana, mchapakazi na aliyependa maendeleo ya nchi na wananchi wake, kwa taifa lake na mataifa mengine.

Rais Samia alisema amepokea kwa huzuni na mshtuko mkubwa msiba huo, akieleza "...mimi na familia yangu tunaungana na Watanzania wote kutoa salamu za pole na rambirambi kwa mjane wa marehemu, watoto, ndugu jamaa na wana-Lindi."

Alisema alifanya kazi na Membe katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Nne, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa muda mrefu. 

"Katika mambo ambayo mwanadamu hawezi kujipangia, ni siku ya kuzaliwa na hata kama utakuja kwa njia yoyote ya upasuaji na kwamba daktari atapanga tarehe ya kufanyiwa upasuaji, kama Mungu hakuitaka litatokea jambo utakuja kwa tarehe nyingine. Vilevile, siku ya kufa binadamu hatuwezi kujipangia," alisema.

Alisema kifo hicho kimewagusa wengi ndani na nje ya mipaka kwa kuwa Membe alikuwa mtu mashuhuri na mwanadiplomasia mahiri.

"Ninaelewa machungu ya wanafamilia kufuatia msiba huu, ila msiba huu sio wenu peke yenu. Ni msiba wetu sote ingawa athari na machungu yatakuwa upande wenu kwa kuwa mmeondokewa na mpendwa wenu. Kwa hakika nguzo kuu imeondoka. Ninamwomba Mungu awape subira.

"Kifo chake kimeacha pengo kubwa sio tu katika familia yake, bali kwa Tanzania na mataifa aliyoyafanyia kazi katika kulinda utu na heshima ya mtu. Hakuna anayependa kuondokewa na mpendwa wake, lakini Mungu huchukua amana yake kwa jinsi inavyompendeza," alisema.

 

ZITTO AFUNGUKA

Akiwasilisha salamu za pole kwa niaba ya wafuasi na wanachama wa Chama cha ACT-Wazalendo, Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, alisema Membe alikuwa mwanasiasa na mwanamikakati wa mfano wa kuigwa.

Alisema alimfahamu mara ya kwanza kwa sifa hiyo mwaka 2005 alipokuwa anapambana kwa ajili ya kupata mgombea atakayemrithi Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

"Kulikuwa na maneno na minong’ono ya chini ya kapeti kuwa mgombea wenu asingeteuliwa mngejiunga nasi tuliokuwa upande wa upinzani. Ni hali ya kawaida kuwa na maneno ya namna hii kila nyakati za uchaguzi.

"Wakati mwingine maneno ya namna hii huwa kweli na wakati mwingine haitokei. Wakati wenu huo haikutokea. Ninadhani kwa sababu mgombea wenu alishinda.

"Kitendo chako (Membe) kuja kupaki gari lako mbele ya ofisi ya makao makuu ya chama changu cha wakati huo, na kuzungumza na mmoja wa waliokuwa wabunge wa chama hicho na kumpa salamu za kumletea mwenyekiti wetu, 'kwamba tujiandae mnakwenda Dodoma, demokrasia ikikanyagwa tuwapokee', kilikuwa ni kitendo cha kimkakati mno.

"Hii ni kutokana na ukweli kuwa ulikifanya mchana hadharani, ukijua kuwa ni lazima macho mengi yalikuwa yanakuona. Lengo ni kutengeneza mazingira ya wakubwa wa chama chako kupata ujumbe mahususi uliokusudia.

"Tukio hili kwangu lilikuwa ni mafunzo ya mwanzo ya uanademokrasia na uanamikakati wako. Ni wanasiasa wachache sana wana kipaji cha kukusanya kwa wakati mmoja uanasiasa na uanamipango ya kisiasa. Wewe uliweza kuwa nazo hizo sifa zote."

Kwa mujibu wa Zitto, Membe alikuwa mstari wa mbele kutetea haki za Watanzania wote. Alisema kuwa mwaka 2006 aliisaidia familia iliyoonewa na kupelekwa DRC kwa madai siyo raia hadi wakarejeshwa nchini. Alijali haki za watu zaidi kuliko maslahi finyu ya kisiasa.

Zitto alisema Membe alikuwa mtu mwenye msimamo, hakuogopa kusema lile uliloliamini, ilikuwa fahari kutokubali kutii mambo kwa sababu tu mkubwa kataka na hakujali madhara ya kusimamia hayo.

"Wakati mgumu sana wa maisha yako kisiasa ulikuwa ndio wakati mgumu sana wa kisiasa nchini. Ulisimama na watetezi wa demokrasia na watetezi wa haki za binadamu bila kupepesa macho.

"Ulikuwa nasi kila tulipopata maswahibu kiasi cha kukuingiza wewe mwenyewe kwenye maswahibu uliyokabiliana nayo kwa namna unayojua wewe mwenyewe.

"Mpaka umauti unakufika hukuacha kulionyesha taifa na dunia namna tunapaswa kuhusiana hata kama tunapingana kimawazo na mirengo ya kisiasa," Zitto alifafanua.

Kwa mujibu wa Zitto, Membe alipambana kulinda heshima yake dhidi ya watu waoga ambao badala ya kukabili hoja zake, waliamua kutuma mtu kumchafua pamoja na wote waliokuwa na mawazo mbadala kwa lengo la kuwanyamazisha.

"Kesi yako kupinga kuchafuliwa ulitusemea na sisi wenzako wote. Ulitupigania sisi wote dhidi ya tabia ya ovyo kabisa iliyojitokeza katika nchi yetu. Tabia ya watu wenye mamlaka kutuma wahuni kutukana viongozi wenzao.

"Tabia ya vyombo vya dola, vingine vyombo vya usalama, kuendekeza upuuzi na hata kuwezesha tabia hiyo chafu kabisa. Ni aibu kuwa mitambo ya baadhi ya vyombo vyetu ilitumika kuchapisha mambo ya namna ile.

"Wapo hapa watu ambao walifadhili na kushabikia upuuzi uliopigana kuupinga mpaka mahakamani na ukashinda. Nao eti wanakulilia. Nao eti wanakuaga.

"Ninaamini kifo chako hiki na mazishi yako haya yatazika tabia zile ambazo hukukubali kamwe ziwe sehemu ya utamaduni wetu wa kisiasa. Ninataraji hata katika mioyo yao watu wale watajuta na kukuomba radhi ukiwa kwenye umauti.

"Nilipenda utaratibu uliotumia kujiunga nasi, ukituandikia barua ya kueleza kwa kina kwanini umeichagua ACT Wazalendo, pamoja na mengine, ukituhimiza tusiache kutengeneza mazingira ya kutoa fursa wa kila mwathirika wa siasa na demokrasia kupata nafasi ya kuendelea kufanya siasa kupitia ACT Wazalendo. Tukio hili lilikuwa kilele cha uanademokrasia wako.

"Ulikaa nasi katika ACT Wazalendo kwa muda mfupi sana wa maisha yako ya kisiasa. Lakini muda huo mfupi ulikuwa na mafunzo makubwa sana kwetu. Ucheshi wako uliamsha ari zetu za kazi. Kila jambo lililokuwa linatokea ulikuwa hukosi mfano wa kutupatia kulinganisha mazingira ya sasa na wakati ukiwa ama serikalini au katika majukumu yako ya nje ya nchi."

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Stergomena Tax alisema, Membe alikuwa mtu muhimu katika safari yake ya kugombea nafasi ya kuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

"Binafsi Membe alinitia ujasiri sana wakati taifa langu liliponiteua kwenda kuwania nafasi ya kuwa Katibu Mtendaji wa SADC. Wizara iliyokuwa inatoa mapendekezo ya kuratibu shughuli hii ilikuwa ni ya Mambo ya Nje.

"Tanzania ilionekana kama ni nchi pekee ambayo ingeweza kushika nafasi hii, lakini katika mchakato wa kuwania walijitokeza wahitaji wengi kutoka nchi mbalimbali lakini yeye alisimama akasema 'hatuogopi ushindani',” alisema.

Waziri huyo alisema kuwa Membe alimwita na kumwambia "tuko nyuma yako, nenda kagombee utashinda". Pia alimsaidia kutekeleza majukumu mengi ya kimataifa kutokana na uzoefu mkubwa aliokuwa nao.

CHONGOLO

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo alisema Membe alikuwa mtu mahiri. Chama kimepoteza mtu muhimu aliyekuwa anagusa maslahi ya nchi kwa ujumla.

Alisema Membe hakuwa mchoyo wa maarifa pale alipohitajika kuyatoa. Maisha yake ya uongozi ndani ya chama na serikali ameacha mengi mazuri yanayostahili sifa.

Akizungumza kwa niaba ya familia ya Membe, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambaye ni Mbunge wa Mtama anakotokea Membe, Nape Nnauye, alimshukuru Rais Samia kwa mchango mkubwa, ikiwa ni pamoja na kusaidia gharama za kusafirisha mwili.

"Familia inawashukuru wote walioguswa, Wizara ya Mambo ya Nje, uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuungana pamoja tangu alipofikwa na umauti kaka yangu. Pia ninawashukuru madaktari wa Hospitali ya Kairuki kwa jitihada za kujaribu kuokoa maisha yake.

Membe alifariki dunia Mei 12, mwaka huu katika Hospitali ya Kairuki mkoani Dar es Salaam alikokwenda kupata matibabu. Mwili wake unatarajiwa kuzikwa kesho katika Kijiji cha Rondo mkoani Lindi.