Miongoni mwa hatua hizo ni kumwagiza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kuitisha kikao maalum cha Baraza la Vyama vya Siasa, ili kushirikisha wadau kufanya tathmini ya utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi.
Kikosi Kazi hicho ni kile alichounda na kukipa majukumu ya kuratibu maoni ya watu kuhusu demokrasia ya vyama vingi nchini, baada ya kilio cha muda mrefu cha wadau cha kuomba katiba mpya.
Mchakato wa kutaka kuwapo kwa katiba mpya, umepitia hatua mbalimbali ambapo sasa utahusisha pia kushughulikia marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusiana na uchaguzi.
Sheria zinazotajwa ni ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na ya Sheria ya Vyama vya Siasa, ingawa sheria hizo hazikutajwa sura na vifungu vyake, kuna pia vipaumbele katika mchakato huo vikiwa ni maboresho ya sheria za uchaguzi kuelekea uchaguzi ujao mwaka 2024 na wa mwaka 2025.
Binafsi ninachukulia uamuzi huo wa Rais kama njia ya kutelekeza nguzo nne ambazo ameshaweka wazi kwamba katika uongozi wake atazisimamia kwa ajili ya ustawi wa taifa hili na watu wake.
Nguzo hizo ambazo amewahi kuzitaja ni maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya Tanzania, na kwamba hizo ndizo zinazoweza kuunganisha Watanzania bila kujali tofauti zao za kisiasa.
Baada ya kuchukua nafasi hiyo ya juu katika nchi, ameendeleakusimamia nguzo hizo, kwa ajili ya kuijenga Tanzania mpya inayojali uhuru wa watu, demokrasia, usawa na haki za binadamu.
Kupitia njia hiyo, amefanikiwa kuwaleta Watanzania pamoja bila kujali tofauti zao za kisiasa na kuhakikisha utawala wa sheria, usawa, kutobaguliwa, fursa sawa kwa wote.
Sasa ameruhusu mchakato wa katiba mpya, ili kuhakikisha katika utawala wake, kila mtu anafurahia haki zake za msingi na kutekeleza majukumu yake kwa uhuru kwa mujibu wa sheria bila kubughudhiwa.
Hiyo ni kutokana na kwamba wananchi wamekuwa wakitaka katiba mpya ambayo itakuwa imewekwa haki zao zote za msingi na jinsi ya kuzilinda ili wafurahie matunda ya uhuru wa nchi yao.
Kwa kuwa tangu alipoingia madarakani kilio cha kwanza cha wanasiasa kwake kilikuwa ni katiba mpya hadi akaamua kuunda Kikosi Kazi, ninaamini kwa mchakato unaoendelea watakuwa nyuma yake.
Iwapo watajitokeza wengine kupinga mchakato unaoendelea, ni wazi wanaweza kusababisha ukakwama kama ilivyotokea baada ya Bunge Maalum la Katiba mwaka 2014.
Nimeelezea hayo kutokana na ukweli kwamba, vipo baadhi ya vyama vya siasa ambavyo havikubaliani na jinsi baraza hilo linavyoendeshwa, ambalo msajili ameelezwa kukutana nalo, kwa ajili ya mchakato huo.
Lakini kwa kuwa lengo la wadau wakiwamo hata CCM ni kuwapo katiba mpya, basi ingekuwa ni vyema wote watakuwa na lengo moja la kuhakikisha katiba hiyo inapatikana, kwa maslahi mapana ya umma.
Kimsingi, mageuzi yanayofanywa na Rais Samia, katika nyanja mbalimbali, yanalenga kuimarisha juhudi za kuelekea kuwa na jamii yenye haki, ustawi wa demokrasia na uchumi unaokuwa kwa faida ya Watanzania wote, hivyo haina budi kuungwa mkono na Watanzania kuanza kutekeleza na kushiriki kila hatua lile serikali inalopendekeza ili kufanikisha uwepo wa katiba mpya na kudumisha demokrasia.