Imeweka wazi kuwa tayari imeshaanza mchakato wa kufanya usajili wa wachezaji bora na wenye uwezo zaidi barani Afrika ambao wanawazidi hawa waliopo, baada ya misimu mitano ya kuishia hatua ya robo fainali, huku ikishindwa kuvuka hatua hiyo mara tatu Ligi ya Mabingwa Afrika na mara moja Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema kwa sasa wanasaka wachezaji watakaoweza kuwasaidia kuvuka kwenye hatua ya robo fainali na hata kutwaa ubingwa wa Afrika ili waje kuungana na hawa waliopo ambao ni wanarobo fainali.
Amekiri kuwa kwa kiasi kikubwa usajili wa msimu huu haukuwaridhisha viongozi wa klabu hiyo, hivyo kwa sasa wamejifunga vibwebwe kuhakikisha kiu ya wanachama na mashabiki wa Simba inaisha.
"Usajili mkubwa ambao tumeufanya msimu huu asilimia kubwa haujaenda vile ambavyo Simba tulihitaji na ndiyo maana tumeishia pale pale kwenye robo fainali. Kwa hiyo viongozi wetu wameliona hilo na wao wanaumizwa na mgando huu tulionao na sasa wanapambana kuona kwamba tunatafuta wachezaji waliokuwa bora zaidi waweze kutupeleka katika hatua ambayo Wanasimba tunaihitaji.
"Tutafanya kila linalowezekana ili kutoka hapa tunapoishia kwa miaka mitano sasa. Tunafanya usajili uliokuwa bora, tutatafuta wachezaji watakaoweza kutusaidia kutoka hapa kwenda kwenye hatua inayofuata, wachezaji tuliokuwa nao hivi sasa pasi na shaka yoyote wanaweza kutufikisha robo fainali, hata Ligi ya Mabingwa ikianza hii leo,
"Tuna uwezo wa kucheza robo fainali, sasa nini kinatakiwa? Ni kusajili na kupata nyota wengine wapya wenye viwango bora na vya juu, kuja kuungana na hawa wanarobo fainali kuja kutupeleka nusu fainali na hata fainali," alisema Ahmed.
Alisema kwenye dirisha hili la usajili walifanya usajili wakiamini utakwenda kuwasaidia, lakini kwa bahati mbaya usajili siku zote ni kamari.
"Viongozi wetu wameliona na kulijua hilo na kwenye dirisha hili la usajili ndicho tunachoenda kufanya. Msimu huu tulifanya usajili tukiamini ya kwamba utakuja kutusaidia kutupeleka huko ambako tulikuwa tunakusudia, lakini nyote mnafahamu usajili ni kamari, unaweza kutoa mtu kwao ni mzuri tu na uwezo mkubwa, lakini akija hapa mambo yanamkataa," alisema Ahmed.
Mwaka 2019 Simba ilitolewa kwenye hatua kama hiyo Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ikifungwa ugenini mabao 4-1, baada ya suluhu ya nyumbani na 2021, ilichapwa mabao 4-0 dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, licha ya ushindi wa mabao 3-0 nyumbani haikutosha kuwapeleka nusu fainali na msimu huu imetolewa na Mabingwa Watetezi, Wydad Athletic Club ya Casablabca nchini Morocco kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya kila timu kushinda bao 1-0 nyumbani.
Mwaka jana, Simba pia iliishia robo fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika ilipotolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3 na Orlando Pirates ya Afrika Kusini, baada ya kila kitu kushinda bao 1-0 nyumbani.










