Kampuni digitali Korea Kusini yaingia ubia na Tume Tehama ‘kusafisha’

02May 2023
Beatrice Philemon
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kampuni digitali Korea Kusini yaingia ubia na Tume Tehama ‘kusafisha’

HIVI karibuni Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini, imeingia mkataba wa kisheria na kampuni ya Aron Group, ya Korea ikitarajiwa itaunganishwa na mifumo ya serikali.

Mkurugenzi Mkuu wa TEHAMA, Dk. Nkundwe Mwasaga, anasema ni hatua itakayoisaidia serikali nchini kuongeza pato la taifa na wakati huo huo, kusaidia wafanyabiashara wadogo na wa kati kuwa na historia nzuri ya biashara zao, hatimaye kupata mikopo kutoka kwenye benki au taasisi za kifedha.

Lingine linatajwa katika hoja hiyo, ni kwamba mkataba utaleta chachu kubwa katika sekta ya TEHEMA nchini, ikiboresha kutoka sekta isiyo rasmi kuwa sekta rasmi, vilevile kukiletwa teknolojia ya kisasa nchini, kutoka Korea Kusini.

Kampuni ya Aron Group ni kampuni, ina makao makuu nchini Korea Kusini na hivi sasa imefungua tawi nchini Tanzania kwa ajili ya kusaidia wafanyabiashara wadogo na kati kutumia njia ya kidigitali katika biashara zao hasa malipo na huduma nyingine.

Dk. Mwasaga anasema kuwa katika utekelezaj, kampuni ya Aron Group itaunganishwa na mifumo ya kiserikali, hapa akifafanua “itafanya kazi yao vizuri au kutoa huduma nzuri kwa wananchi wa Tanzania, itawavutia wawekezaji wengi zaidi kutoka Korea Kusini kuja kuwekeza nchini.”

Anasema, ili kuhakikisha Tanzania inakuwa shindani katika uchumi wa kidigitali, tume yake inahakikisha wanatoa huduma inayokidhi haja ya kusaidia serikali, kwa kupata kodi kupitia miamala ya simu.

“Lengo kuu la kuwezesha kampuni hizi tunataka zikue na kupeleka huduma nchi jirani, watoe ajira Tanzania na nchi jirani na pia tunataka Tanzania ijulikane ina uchumi wa kidigitali na isaidie kuleta teknolojia ya kisasa,” anasema.

Kwa mujibu wa bosi huyo wa Tume ya TEHAMA, kampuni hiyo mbia wa teknolojia, inalenga kuisaidia serikali kujua idadi ya wafanyabiashara walioko nchini, hata kukawapo takwimu sahihi kuhusu kiasi cha malipo (transactions) kinachofanyika kwa siku au mwezi kupitia mitandao ya simu.

“Sisi kama tume katika kukuza na kutafuta njia ya kuvutia watu na wawekezaji, pia tunashiriki kwenye makongamano makubwa nje ya nchi. Pia, Tanzania ina kongamano lake ambalo linakutanisha wadau mbalimbali waliopo kwenye sekta ya TEHEMA,” anafafanua.

Tume ya TEHAMA hadi sasa inaelezwa inatoa mafunzo ya muda mfupi kwa watalaamu wa sekta hiyo, pia wanawatafutia wadau wengine wanaoweza kutoa mafunzo ya muda mrefu, ili kutoa huduma nzuri ya fani hiyo, wataalamu wazuri wanaoaminika, pia kwenye kanzi data ya taifa.

Anasema, hadi sasa tume ya Tehama imefanikiwa kusajili kampuni zaidi ya 300 (Start-up companies) na zinatakiwa zitoe huduma katika nchi ya Tanzania, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ma Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC), mtazamo wa kiufundi ulioko ni kuwapo uchumi wa kidigitali nchi nzima.

HATUA ILIYOFIKIWA

Dk. Mwasaga anasema hadi Tume ya TEHAMA imeshafanikiwa kusajili wataalamu wake 1600 na sasa inaangalia uwezekano wa kufanya nao kazi, pia kuwapa mafunzo ya muda mfupi, akitaja msimamo wake kwa sasa ni kwamba, wanauunga mkono taasisi changa za TEHAMA zinazochipukia, ili ziwe chachu katika utoaji ajira kwa vijana na kurahisisha utoaji huduma nchini na mataifa jirani.

“Tutaendelea kuhakikisha upatikanaji huduma za kidigitali katika mifumo ya miamala ya pesa inakuwa ya uhakika na yenye kukidhi usalama wa pesa za mtumiaji," anasema

Anataja takwimu kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), ni kwamba kuna jumla ya kampuni ndogo milioni 30 zinazotoa huduma kwa ‘cash’ na hazina rekodi ya biashara wanazoifanya.

“Sisi kama tume (ya TEHAMA), tunapenda huduma zote zinazotolewa na kampuni hizi zianze kutolewa kwa njia ya mtandao, ili kuwasaidia kuwa na rekodi sahihi kuhusu biashara zao na malipo ya biashara zao,” anasema na kuongeza kuwa “kampuni nyingi zinaanzia watu wanne na kuendelea.”

Pia, anatoa rai kwa kampuni nyinginezo kuja kuwekeza Tanzania katika sekta ya TEHAMA kwa sabau serikali ya Tanzania kupitia tume ya tehema imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji .

ARON GROUP

Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa Aron Group, Leonce Mongi, akizungumza na Nipashe, anasema hadi sasa kampuni yake imetengeneza mfumo wa malipo unaoitwa ‘shake up’  na ‘digital payment solution’ zikiwa mahsusi  kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo na wa kati, kupokea malipo kutoka kwa wateja wao, kupitia simu za mkononi.

Kupitia mfumo huo wa ‘shake app’ anadems mfanyabiashara ataweza kutangaza biashara zake, pia mfumo huo utawasaidia wafanyabiashara kukusanya taarifa za mapato na matumizi kupitia mfumo huu, hivyo kuwa na historia nzuri ya miamala wanayofanya katika biashara zao au huduma wanazozitoa katika maeneo yao.

“Mfumo huu ni salama na rahisi kwa mtumiaji, imekidhi vigezo nawaomba watanzania hasa wafanyabiashara hapa nchini kutumia mfumo huu,” anausifu ubunifui huo.

Kwa mujibu wa Mongi, Aron Group hivi sasa imefungua ofisi zake Dar es Salaam, lakini baada ya miezi sita itapeleka huduma zake katika mikoa mbalimbali nchini.

“Tumeamua kujikita katika eneo hili baada ya kugundua kuwa wafanyabiashara wengi wametawaliwa na sekta isiyo rasmi, sisi kama kampuni tumekuja na mfumo huu kusaidia serikali kujua kuna wafanyabiashara wangapi hapa nchini, miamala mingapi inafanyika kwa siku, mwezi na tutaendelea kuwa pamoja na serikali na tunashukuru Tume ya Tehema kwa kusaini mkataba na sisi,” anasema.

 

Top of Form

Bottom of Form

Top of Form

Bottom of Form