Mke kanikimbia bila hata kugombana

01May 2023
Flora Wingia
Nipashe
Maisha Ndivyo Yalivyo
Mke kanikimbia bila hata kugombana

KARIBU tena msomaji wangu tuendelee kuelimishana kuhusu mikiki mikiki ya maisha. Mengi yamejificha katika familia zetu, huku mengine tukiyashuhudia na kudhani kuwa Maisha Ndivyo Yalivyo kumbe ni shida!

Tena ndoa nyingi hivi sasa zinaanza mitikisiko miaka ya mwanzoni tofauti ya miaka kadhaa iliyopita ambapo tafrani huanza baada ya miaka mitano kuendelea.

Hapo wameshazaliwa watoto wawili au hata watatu, gari lipo na pengine ujenzi wa nyumba upo kwenye mchakato au tayari.

Wiki iliyopita tulimjadili kijana mmoja ambaye alioa binti ambaye hakuwahi kupata elimu kabisa. Akatamani sana kumuendeleza ili aweze kuendana na maisha yenye uelewa mpana kifikra.

Japokuwa alianza kumpatia mafunzo ya elimu ya msingi mwenyewe, alipotaka kumuinua zaidi kielimu binti akagoma. Pengine ni kutokana na kuona kwamba kwao wazazi hawakumsomesha na wapo wengi hawajasoma katika familia yao akajikatia tamaa.

Roho ya ujinga ama kwa hakika inatesa watu wengi, na ndilo lengo kuu la shetani kutesa wanadamu. Mungu anaweka bayana katika neno lake aliposema, “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitasahau watoto wako”.(Hosea 4:6).

Ujinga ni mbaya sana na ni kifungo kikubwa kinachosababisha matatizo kwa wengi. Kiwango cha ujinga alicho nacho mtu, ndicho shetani hukitumia kumdanganya.

Nilieleza wiki moja iliyopita kwamba yupo mama alimvuruga mumewe kiasi cha kufikia hatua mume akaihama nyumba yake na kwenda kuanzisha maisha kwingine.

Baada ya muda kupita, mama akili ikarudi akagundua alipokosea, akaanza kuwatumia watoto kumshawishi baba yao arudi nyumbani. Baba akakataa kwani alishaanzisha maisha yake, akajenga nyumba na kununua gari lake lingine na zaidi ya yote anayo amani tele.

Msomaji wetu mmoja alipoisoma makala ile akanitumie ujumbe kuelezea naye jinsi mkewe alivyokimbia ndoa na kutokomea kusikojulikana. Akaona ujumbe hautoshi akanipigia kabisa simu. Akasema kwa tukio hilo yeye alishangaa kwani hawakuwahi kugombana na mkewe mbali na kuchakarika kimaisha kwa pamoja.

Akasema kwamba yeye ni mfanyabiashara na mkewe alikuwa tu mama wa nyumbani huku akimshirikisha kwenye biashara kadhaa kuongeza kipato cha familia. Walibahatika kupata mtoto mmoja.

Mtoto huyo akiwa katika umri wa miaka minne, mama akaanza vituko mara anachelewa kurudi nyumbani. Akiulizwa ananuna au anajibu kwa ukali. Ilibidi nivumilie kwani nilikuwa nampenda mke wangu sikutaka kumuudhi.

Siku moja nikitoka kwenye shughuli zangu kufika nyumbani nikaona tofauti. Mke wangu na mtoto hawapo na hata sanduku lake halipo. Kuuliza majirani wakasema hawajamuona akitoka.

Tokea siku hiyo sijamuona tena mke wangu na hata nilipofuatilia kwa ndugu zake hawakunipa habari zake. Ni miaka mitano tokea aondoke. Anamalizia kusema mpendwa huyu.

Msomaji wangu, vituko vya wanandoa kuzikimbia ndoa zao ni vingi. Na inakuwa mbaya zaidi mama anapoikimbia nyumba yake baada ya yeye kuwa chanzo cha anguko. Ni wazi kuwa mwanamke mpumbavu ndiye anayebomoa nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe.

Niliwahi pia kueleza kwenye safu hii kwamba yupo mwanamke mmoja alichukuliwa kijijini na kuletwa mjini. Akaolewa na kijana mmoja aliyekuwa na kazi ya kuongoza watalii wanapokuwa katika ziara sehemu mbalimbali nchini.

Wakabahatika kupata mtoto mmoja. Baada ya miaka miwili bibie akabadilika akaanza kumwambia mumewe kuwa anahisi anaye mwanamke mwingine(hawara). Vinginevyo sharti aache kazi ili waishi. Mume akashangaa kwani kulikuwa hakuna kitu kama hicho. Na pia kwa nini aache kazi!

Mwanamke akaanza vituko, mara hali, mara hapiki, analala sebuleni. Siku moja narudi nyumbani nikakuta hayupo. Kumbe katoroka. Nikaenda kuripoti polisi.

Nikapiga simu kwao kijijini mama yake akanitukana kwamba nimemtesa binti yake na kwamba hatarudi tena kwangu. Nikabaki nashangaa.

Hata hivyo, nilizidi kufuatilia nikagundua alishaolewa na mtu mwingine. Cha ajabu aliishia kwenda kulima vibarua vya shamba kwa watu na mumewe mpya.

Mpenzi msomaji, wapo kinamama ambao sijui ni madudu gani huwaingia akilini na kutifukatifuka hadi kuchukua maamuzi yanayowapeleka kusiko. Hii ni roho ya ujinga inayopumbaza watu wengi inafanya kazi.

Wengi siyo wavumilivu katika ndoa na wanapokurupuka wanatengeneza majanga. Je, una kisa? Ujumbe 0715268581.