Ubabaishaji usipewe nafasi Ligi Kuu Bara msimu 2016/17

20Aug 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ubabaishaji usipewe nafasi Ligi Kuu Bara msimu 2016/17

PAZIA la Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara kwa msimu wa mwaka 2016/17, linafunguliwa rasmi leo kwa kushirikisha timu 16 kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Timu zinazoshiriki ligi hiyo, ambayo bingwa wake ataiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa mwaka 2018/19 ni pamoja na mabingwa watetezi Yanga, Azam FC, Simba na African Lyon zote za Dar es Salaam.

Klabu nyingine ni Mtibwa Sugar ya Morogoro, Kagera Sugar (Kagera), Majimaji (Ruvuma), Mbeya City na Tanzania Prisons (Mbeya), Mbao FC na Toto Africa (Mwanza), Mwadui FC na Stand United (Shinyanga), Ndanda FC (Mtwara), Ruvu Shooting na JKT Ruvu za Pwani.

Kutokana na kuanza kwa kindumbwendumbwe cha michuano hiyo, ambayo huvuta hisia za mamilioni ya Watanzania, mashabiki wa soka nchini wanatarajia kushuhudia ushindani miongoni mwa timu zitakazoshiriki.

Wakati michuano hiyo ikianza kwenye viwanja mbalimbali, kumbukumbu za wapenda soka nchini juu ya mambo yaliyojiri katika msimu uliopita, bado zinagonga vichwani mwao.

Miongoni mwa mambo yaliyojitokeza, mbali na ushindani, ni usalama mbovu, hali duni ya viwanja, uamuzi mbovu kwa baadhi ya marefu uliosababisha baadhi kuambulia vipigo na uzalendo uliokithiri katika baadhi ya maeneo.

Mengine ni usimamizi mbovu kutoka Bodi ya Ligi, upanguaji na upangaji mbovu wa ratiba na baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuonyesha upendeleo wa waziwazi kwa baadhi ya timu kutokana na mahaba waliyo nayo kwa timu husika.

Mambo hayo yalisababisha kwa kiasi kikubwa kuvurugwa kwa ligi na hata msisimko wa mchezo huo na ushindani kukosekana, hivyo michuano hiyo kugubikwa na kasoro nyingi na hata kupoteza uhondo uliokusudiwa.

Kutokana na kuwapo kwa mambo hayo, TFF kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi, inapaswa kuhakikisha kasoro hizo zinapatiwa dawa ili kuhakikisha michuano inaendeshwa kwa kufuata kanuni na si mapenzi ya baadhi ya watu.

Tayari yamejitokeza malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadau kwamba bodi ya ligi, yenye dhamana ya kuendesha michuano hiyo mikubwa ya soka nchini, imeanza kuyumba baada ya kubadilishwa ratiba hata kabla ya ligi kuanza.

Ni wazi kwamba kuwapo kwa upendeleo kwa baadhi ya timu na uamuzi mbovu husababisha hata mshindi wakati mwingine kupatikana kwa njia zisizo halali au kwa maneno mengine, mshindi kupatikana nje ya uwanja. Hali hiyo, kwa kiwango kikubwa, husababisha kupata wawakilishi wabovu katika michuano ya kimataifa.

Kwa upande wa timu zinazoshiriki, pia kumekuwa na matatizo kwani baadhi ya mashabiki wamekuwa wakifanya fujo viwanjani huku hata baadhi ya wachezaji wakionyesha vitendo vya utovu wa nidhamu uwanjani.

Kutokana na kasoro hiyo, viongozi wa klabu na mabenchi ya ufundi wanapaswa kuwaelimisha wanachama, mashabiki na wapenzi pamoja na wachezaji juu ya umuhimu wa kufuata na kuheshimu sheria zinazoongoza soka. Haiingii akilini kuona mchezaji akibishana na mwamuzi au kumtendea mchezaji mwenzake vitendo vya aibu pamoja na kuonyesha ishara za matusi. Kwa ujumla, vitendo hivyo havikubaliki.

Ili kuhakikisha ligi kuu ya msimu huu inakuwa na mwamko pamoja na ushindani, jambo la kwanza linalopaswa kufanyika ni kwa wasimamizi kutenda haki kuanzia upangaji wa ratiba hadi waamuzi wanaochezesha mechi husika. Litakuwa jambo la kushangaza kuona viongozi wa TFF na Bodi ya Ligi wanabadilisha ratiba au waamuzi kwa utashi wao ili kuzipendelea baadhi ya timu na wakati mwingine bila sababu za kuridhisha.

Kwa ujumla, wadau wote wa soka nchini hasa wanaohusika moja kwa moja na ligi kuu, wanapaswa kuheshimu na kufuata sheria na kanuni ili kuhakikisha michuano ya msimu wa 2016/17 inaendeshwa bila kupindishwa kwa namna yoyote.

Ni imani yetu kwamba iwapo kila mhusika atatekeleza wajibu wake kwa kusimamia na kuzingatia haki, michuano hii itakuwa na ubora wa hali ya juu na kuleta msisimko mkubwa na ushindani miongoni mwa timu husika.

Kasoro zilizojitokeza katika ligi ya msimu uliopita, ziwe changamoto kwa wadau wote kuzifanyia kazi ili kuboresha michuano inayoanza leo kwa manufaa ya maendeleo ya soka na taifa kwa ujumla.

www.guardian.co.tz/circulation