Ukaguzi umebainisha wanafunzi hao 785 hewa, wamewekwa katika orodha ya malipo ya fedha za mkakati wa elimu bure katika shule.
Wanafunzi hao hewa wamegundulika kuingizwa, siku chache baada ya Rais Magufuli alipohitimisha ziara yake mkoani Mwanza.
Akiwa mkoani humo alisema anafahamu kuna walimu wakuu ambao wanaingiza majina hewa kwenye orodha ya shule zao ili kupata fedha nyingi zaidi kutoka serikalini kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa elimu bure.
Kubainika kwa wanafunzi hewa hao kulitangazwa juzi katika majiji ya Dar es Salaam na Arusha kwenye mikutano baina ya maofisa wa wilaya hizo na vyombo vya habari.
Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, alisema kutokana na ugunduzi huo, Manispaa ya Kinondoni imewaagiza katibu tawala na mkurugenzi wa manispaa hiyo, kuwavua madaraka walimu wakuu wapatao 90 waliohusika na upotevu wa Sh. milioni 70 baada ya kuwanufaisha ruzuku ya elimu bure ya wanafunzi 5,996.
Walimu hao ambao ni wa shule za sekondari 68 na msingi 22, wametakiwa kuzilipa fedha zote ambazo zimeisababishia hasara Serikali kwa kipindi cha Januari hadi Julai mwaka huu na kuwa walionufaika na ruzuku hiyo ni 3,462 kwa sekondari na 2,534 kwa msingi.
Jijini Arusha, wakuu 33 wa shule za msingi na sekondari wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za kuchomekea wanafunzi hewa katika orodha ya shule hizo kwenda serikalini. Waliosimamishwa ni wa shule za msingi 11 na wa sekondari 12 ambazo zimegundulika kuwa na jumla ya wanafunzi hewa 1,849.
Uchunguzi huo umebaini madudu mengi, lakini itoshe kusema kuwa ni vitendo vinavyodhihirisha kwamba sekta ya elimu bado inakabiliwa na changamoto kubwa.
Kinachosikitisha ni madudu yaliyobainika katika ukaguzi huo katika shule za msingi na sekondari kufanana na udanganyifu wa kutumia wanafunzi hewa uliobainika katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini na kuisababishia serikali hasara ya mamilioni ya fedha.
Kibaya ni kwamba udanganyifu uliobainika Dar es Salaam na Arusha umefanyika katika siku za mwanzoni tangu utekelezaji wa mpango wa kutoa elimu bure ulipoanza.
Lengo la utoaji wa elimu bure ni kuwawezesha watoto wengi hususani wa familia maskini wanapata elimu ya msingi na sekondari kwa kuwa ada ndiyo iliyokuwa ikiwakwaza kupata elimu.
Kama Serikali imeacha kutekeleza vipaumbele vingine na kuamua kujikita kuwasomesha bure watoto wote kwa kutumia fedha nyingi za walipakodi, jamii isikubali mpango huo ukwame kwa kuwa watoto wa maskini ndio watakaoathirika kwa kukosa fursa ya elimu ambayo ndio msingi wa maendeleo.
Walimu wote waliohusika katika matukio ya Dar es Salaam na Arusha wachukuliwe hatua za kisheria na kinidhamu ili liwe fundisho kwa wengine.
Tunashauri kamati za shule zihusishwe katika mchakato mzima wa uhakiki wa wanafunzi wanaoandikishwa katika shule za msingi pamoja na uhakiki wa wale wanaofaulu kuingia sekondari katika shule wanazopangiwa, lengo likiwa kudhibiti uingizaji wa wanafunzi hewa ili wakuu wa shule wajipatie fedha za Serikali kwa njia za udanganyifu.
Tusikubali mpango huu kukwama kwa kuwa umeonyesha mafanikio katika hatua ya awali kutokana na idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa shule za msingi kuongezeka mara dufu.










