OLENGURUMWA URAIS 2025

29Mar 2023
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe
OLENGURUMWA URAIS 2025
  • Aambiwa ni mtizamo wa ki-AZAKI si wa wanasiasa wanaotamani dola *Atetewa ana haki ya maoni yake, wengine ni kampeni, anatumiwa

MWAKA ujao ni wa uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa, kisha utafuata mwingine 2025 wa urais, wabunge na madiwani, hivyo ndani ya miaka miwili mfululizo, Watanzania watakuwa wanachagua viongozi kwa mujibu wa katiba.

 

Wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi huo, kumekuwapo na maoni tofauti yanayotolewa na wadau wa siasa yakiwamo ya kuvitaka vyama vya upinzani kumwachia Rais Samia Suluhu Hassan uongozi uchaguzi wa mwaka 2025, wanasiasa wengine wajipange kwa kazi 2030.Vinashauriwa kuwaweka wagombea wa serikali za mitaa na madiwani na ubunge lakini katika uchaguzi mkuu wamwachie Rais Samia amalizie muhula wa pili.Ni Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa, anayetoa ushauri huo, akieleza sababu zake kuwa ni kutamani kuona nafasi ya urais ikiwaniwa na Rais Samia.

MARIDHIANO SI KUACHIANA

Kutokana na ushauri wa mwanaharataki huyo, Nipashe imekutana na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzaani na wachambuzi wa siasa na kuzungumzia suala hilo ili kupata mtazamo wa ushauri wake.

Inaanza na Makamu Mwenyekiti wa ACT -Wazalendo Bara, Dorothy Semu, anayesema, mawazo ya mratibu huyo ni ya ki Asasi za Kiraia (AZAKI) na kwamba wao ni chama cha siasa na lengo lao ni kushika dola si kufanya siasa za vyama visivyo vya kiserikali.

“Tumemsikia Olengurumwa, tunajua mawazo yake, yeye ni mtu wa AZAKI, amekuja na fikra za ki-AZAKI, lakini lengo letu ni kushika dola, tutaweka wagombea katika ngazi zote bila kujali nini kimetokea, yale ni mawazo yake, lakini kama chama cha siasa tutaendelea na harakati zetu, tukiwa na mawazo kama yake, tutaelekea kuwa taasisi za kiraia," anasema Dorothy.Anafafanua kuwa nia njema aliyoonyesha Rais, ni muhimu kwa kuwa ndiye kiongozi wa nchi, na kwamba hawaendi kwenye maridhiano ili kuachiana nafasi bali kuweka mambo sawa, kwa ajili ya manufaa na mustakabali wa taifa.Anaongeza kuwa Rais kukutana na vyama ni sehemu ya majukumu yake kama kiongozi wa nchi, ili kuiponya na majeraha, kuweka njia bora ya kulisaidia kusonga mbele, na kwamba hatua hiyo si kigezo cha kuachiana nafasi."Chama ambacho hakiko tayari kushika dola, ni chama chenye mawazo ya ki-AZAKI, si ACT- Wazalendo kwa vile tuna malengo hasa kukamata madaraka, yaani mamlaka kamili ya nchi, hivyo si rahisi kuachiana nafasi." Anasisitiza Dorothy.

KATIBA INARUHUSUMchambuzi wa siasa, Gwandumi Mwakatobe, anasema jambo la kwanza kuzingatia ni kuheshimu maoni ya mtu kwa kuwa katiba ya Tanzania inaruhusu uhuru wa  kutoa maoni."Kwa mantiki hiyo, ninaheshimu maoni yake au mtazamo wake, lakini ni muhimu kutambua kuwa katika suala la uchaguzi, wanaoamua wamchague nani ni wapigakura kwenye karatasi na boksi la kura, hakuna mgombea anayejichagua," anasema Mwakatobe.Anafafanua kuwa ushauri wa kuwataka wapinzani waache nafasi moja, kwa ajili ya mgombea fulani si sahihi, kwa madai kwamba hajichagui, badala yake waachiwe wananchi au wapigakura waamue wanamtaka nani na lini si kazi ya mtu mmoja.

"Nimeeleza kuwa ninaheshimu maoni na mtazamo wa mtu, kwani katiba imempa raia uhuru wa kufanya hivyo, lakini ni vyema pia tujiulize kama mtu akiachiwa nafasi anaweza kujichagua mwenyewe? Anahoji.Mchambuzi huyo anasema ushauri wa Olengurumwa unaweza kuzingatiwa, lakini wapigakura wakawa hawautaki au wakaukubali na kwamba waokwenda kupigakura ndiyo wanaotakiwa kuachwa waamue nani wanamtaka awaongoze."Niseme tu kwamba, kila mtu ana haki ya kutoa maoni, lakini si lazima maoni hayo yakubaliwe au kukataliwa, ila mkazo wangu ni kwamba, mwenye uamuzi wa mwisho amchague nani ni Mtanzania atakayeweka kura ya ndiyo au hapana wakati ukifika," anasema.AU KAMPENI MAALUMMwenyekiti wa Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo Tanzania (CEGODETA), Thomas Ngawaiya, anasema huenda baadhi ya wapinzani wamepitia kwa Olengurumwa kufanya kampeni baada ya kuona mambo makubwa ambayo amewafanyia kama njia ya kurudisha shukrani na heshima kwa Rais Samia."Unakumbuka miaka kadhaa iliyopita vyama vya upinzani vilikuwa na wakati mgumu hadi vikakosa madiwani na wabunge vikasahaulika. Chini ya Mama vimeibuka upya, hivyo si vibaya kurudisha shukrani," anasema Ngawaiya.Anaongeza kuwa pamoja na hayo, lakini dhana ya vyama vingi, ni kuwa na mtu mwenye uwezo zaidi wa kuongoza bila kujali chama anachotoka, kwa kuwa anayeshinda anakuwa kiongozi wa nchi si wa chama."Hivyo inaonyesha Mama Samia ameonekana ni bora zaidi katika nafasi hiyo, ndiyo maana zimeanza kampeni kama hizo, na kama wapinzani wenyewe wamo kwa mlango wa nyuma ni wazi wameona nuru kwa Mama Samia,"anasema.

WAPINZANI JIBUNIAidha, Ngawaiya anawashauri wapinzani kujitokeza hadharani kujadili maoni ya Olengurumwa, ili Watanzania wajue msimamo wao kama wanaungana na mwanaharakati huyo au wanapingana."Lakini kwa hali ilivyo ni wazi wameshaona Mama Samia ni bora zaidi. Ninashauri hata katika udiwani na ubunge, wachaguliwe wagombea bora bila kujali vyama wanavyotoka, kwani lengo ni kujenga Tanzania,"anasema.Olengurumwa, anatoa ushauri huo akisema kutokana na Rais Samia kuonyesha nia ya maridhiano na upinzani, huku vyama vya siasa vikianza kurejea kazini baada ya kuwekwa rumande kwa miaka saba ni vyema kumwachia.

Anasema ni vyema ili kukuza utawala bora na kuongeza utekelezaji wa yale yaliyofikiwa na kuazimiwa.Mratibu huyo anashauri vyama viwekeze kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa na kwa uchaguzi wa mwaka 2025, wasimamishe madiwani na wabunge na kuachana na nafasi ya urais.

Akikaririwa na vyombo vya habari anashauri vyama vya upinzani kutosimamisha wagombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, akiwa na sababu kadhaa.Anasema kutokana na Rais Samia kuonyesha nia ya majadiliano na upinzani, huku vyama vya siasa vikianza kurejea tangu kufungiwa shughuli zao kwa takribani miaka saba, ni vyema vikaacha nafasi hiyo, ili kukuza utawala bora.Mratibu huyo anashauri vyama viwekeze kwa ajili ya uchaguzi unaokuja wa serikali za mitaa , madiwani na ubunge, lakini nafasi ya urais waiache.Olengurumwa anashauri wafanye hivyo ili angalau wapate theluthi ya wabunge, ya madiwani na wenyeviti wa vijiji kwa uchaguzi unaokuja wa mitaa na mkuu 2025."Uchaguzi wa mwaka 2030 waweke wagombea urais, lakini wa 2025 ukiwa wa haki, wapinzani watapata viti vya ubunge, udiwani, hivyo waingie makubaliano na Rais katika uchaguzi huru na haki,"anasema Olengurumwa.Anafafanua kuwa ili kuwa mgombea urais unahitaji pesa, na akidai wapinzani wana tatizo hilo na kuwataka wawekeze kwa wagombea udiwani na ubunge, huku akiongeza kuwa kwa mtazamo Rais aliyeko madarakani anatekeleza misingi ya wapinzani ikiwamo kuruhusu shughuli za kisiasa.