Taarifa ya kuanza kwa michezo hiyo ambayo inatambuliwa kama Polisi jamii cup imetolewa leo Machi 25 na kamanda wa polisi mkoani Manyara Kamishna Msaidizi wa Polisi George Katabazi katika uwanja wa Kwaraa uliopo Mjini Babati.
Katabazi amesema mashindano hayo yameanza kulindima leo Machi 25 yatahitimishwa Aprili 23 mwaka huu.
Aidha amesema lengo la kuanzisha mashindano hayo ni kutekeleza agizo la Mkuu wa Jeshi la Polisi ambalo alilitoa kwenye waraka Na. 2 wa mwaka huu ambapo waraka huo ulisisitiza kushirikisha vijana katika kupambana na uharifu.
"Tumeona tutumie michezo ili kupambana na uharifu kwa kuwa uharifu haulipi na siyo kitu kizuri," amesema Katabazi.
Katabazi amewataka vijana kukataa uharifu ambapo miongoni mwa uharifu unaofanywa ni kutumia dawa za kulevya na kuuza, unyang'anyi wa kutumia silaha, uvunjaji na kujichukulia sheria mkononi.
Aidha amesema mashindano hayo yatakuwa endelevu ambapo yatafanyika kila kata, wilaya na kwa mkoa yatakuwa yanafanyika kila mwaka.
Amesema katika mashindano hayo timu 72 za mkoa ndio zitashiriki na timu sita za Netiboli zitachuana.
Katabazi amesema kila Wilaya itatoa timu moja ili kumtafuta mshindi mmoja ambaye atashiriki robo fainali.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange amemshukru Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini(IGP) kwa kuwa na maono na kutoa waraka huo.









