Biashara United ambayo ilishuka daraja msimu uliopita iliambulia kipigo hicho kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora na kuifanya kushika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi ya Championship, ikiwafanya wapinzani wao kukaa kwenye nafasi ya pili wakiwa na pointi 49.
Timu hiyo ambayo msimu uliopita ilicheza Kombe la Shirikisho barani Afrika, ina pointi 23, ikipoteza kabisa matumanini ya kurejea Ligi Kuu kwani imecheza mechi tatu mfululizo bila kushinda, ikitoka suluhu dhidi ya Mbuni, akachapwa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa, kabla ya kukutana na kipigo kingine juzi.
Wakati Biashara ikipoteza matumaini hayo, ni mechi chache tu zimebakia kabla ya JKT Tanzania haijatangazwa kurejea Ligi Kuu, baada ya juzi kushinda kwa mara nyingine tena bao 1-0 dhidi ya Transit Camp, mechi ikichezwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, kwa bao pekee lililofungwa na Martin Kiggi.
Ni ushindi unaoifanya kufikisha pointi 56 ikiendelea kuwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, na kuonekana hakuna tena wa kuizuia kurejea kwenye Ligi Kuu msimu ujao, baada ya kuteremka msimu wa 2020/21.
Katika matokeo mengine ya ligi hiyo juzi, timu ya Fountain Gate ililazimishwa suluhu dhidi ya Pan African, Uwanja wa CCM Gairo Morogoro, Mashujaa ikaichapa Copco bao 1-0, Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, African Sports ikalazimishwa suluhu nyumbani Mkwakwani dhidi ya KenGold na Green Warriors ikabamizwa mabao 2-1 nyumbani Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam dhidi ya Pamba FC.










