Kijana (jina tunalo) ni mhanga mwenye simulizi ya safari yake, alivyonasa hadi alivyochomoka, akinena alianza safari yake katika sura kwamba, baada ya kufariki baba yake akiwa na umri mdogo miaka 13, mwanafuzi wa darasa la sita, akawa anapenda sana kwenda kuangalia runinga usiku kwenye mabanda.
Ni kitendo ambacho hakukipendelea hata siku moja, mama yake akamchapa sana hadi akaamua kutoroka nyumbani, maeneo ya Mganza, Chato, kwenda mkoani Mwanza ambako dada yake alikuwa anaishi.
“Nilitafutiwa kazi za ndani na dada kwa rafiki yake kwa ahadi ya mshahara wa shilingi 8,000 ambako nilitumikishwa kazi nyingi, kwenye nyumba mbili na nilikaa miezi mitatu bila ya kupewa malipo, hali iliyosababisha niondoke na kurudi kwa dada ambaye alinifokea na nikaamua kuondoka.
Anasema, akaamua kuelekea visiwani, akipataja visiwa vya Yozu, Mchangani na Zilagula vilivyopo wilayani Ukerewe, ambako alikutana na marafiki wanaovuta bangi, sigara, kunywa pombe na ni wachezaji wa disko usiku.
Binti huyo anasema binafsi hakujua pa kuelekea, akaangukia kujiunga na vitendo hivyo na baada ya miezi sita alirudi jijini Mwanza.
“Nikiwa sehemu nilizokuwa naenda kununua bangi, nilipata mwanaume wa kuishi naye ambaye pasipo kujua tukiwa tunaendelea na uvutaji huo, kumbe alikuwa akinichanganyia bangi na dawa za kulevya akitaja aina ya Heroine, ambayo alijikuta akiingia kwenye uraibu wa matumizi ya dawa za kulevya,” anasema.
Anaeleza lengo la mwanaume huyo ilikuwa kumuingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya, ili aweze kumtumikisha kufanya biashara ya ngono na akawa anafanya hivyo kila siku, akikutana na wanaume wengi, kisha anampelekea pesa mwanaume huyo.
"Ililazimika nijiuze asubuhi, mchana na jioni ili nipate pesa ya kuvuta na kumvutisha huyo kijana na ilifika hatua nikakosa mtu wa kuniinua, nikaanza kuruka mageti kuiba kwenye nyumba za watu, ili kupata pesa ya kununua dawa za kulevya," anasema.
Kijana huyo anaendelea: “Mwaka 2013 nilipata mtoto na mwanaume tofauti na niliye kuwa nikiishi naye, ambaye alifariki siku chache baada ya kujifungua, kwani kutokana na matumizi ya dawa za kulevya, nilikuwa sihudhurii kiliniki kupata huduma za afya.”
Anaeleza kutumia dawa za kulevya na kutumikishwa kingono kwa miaka 10 kuanzia mwaka 2008 akiwa na umri miaka 14 hadi mwaka 2018, alipoacha kutumia dawa hizo, akaanza matibabu maalumu katika kituo husika kilichopo kwenye Hospitali ya Rufani Sekou Toure, jijini Mwanza.
"Kwa kweli dawa za kulevya zimenipotezea mwelekeo nikiwa na umri mdogo na nimeambukizwa virusi vya Ukimwi na homa ya ini, kutokana na mwenendo mbaya nilio kuwa nao," anatamka kwa kauli ya majuto.
WADAU KINGA
Godfrey Kirumbe, mkazi wa Nyegezi, jijini Mwanza, anakumbusha haja ya jamii kuwalinda vijana wasijiingize katika utumiaji dawa za kulevya, akisisitiza hoja inapaswa kutolewa kwa upana katika jamii, kuanzia ngazi za chini ya elimu, kuwawezesha watoto kukua wakiwa na uelewa sahihi wa namna ya kuepukana na matumizi hayo.
Anashauri serikali inapaswa kutafuta suluhisho la udhibiti dhidi ya kuingizwa nchini, pia uzalishaji wa dawa hizo kwa kuwachukulia hatua kali wote wanaobainika kujihusisha na biashara hiyo, hata kuangukia katika madhara mbalimbali ndani ya jamii inayoshindwa kutekeleza majukumu ya ujenzi wa taifa.
Dk. John Kahemele, ni Naibu Mkurugenzi Mkazi kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ICAP, anaitambulisha kuwa ni mshiriki mradi unaopambana na madhila hayo ya Ukimwi na dawa za kulevya, kupitia mpango wa dharura unaoitwa ‘Pepfar’ kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania.
Mkoani Mwanza, penye simulizi tajwa, wanatekeleza huduma ya tiba na matibabu kwa wanaoishi na virusi vya ukimwi, pia kusaidia mabinti rika balehe walio kwenye mazingira hatarashi ya kupata maambukizi ya magonjwa, kupitia kituo cha kusaidia waraibu wa dawa za kulevya.
Anafafanua kwamba, Mwanza inakadiriwa kuwa na takribani watu 145,000 wanaoishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi na hadi Desemba 2022, wamefanikiwa kuwafikia watu 121,000 wakiamini ni hatua nzuri katika udhibiti wa maambukizi mapya na vifo kufikia sifuri ifikapo mwaka 2030.
Anatoa wito kwa wote wenye tatizo la uraibu wa dawa za kulevya, kuepukana na hali hiyo huku akiwaasa wasichana wadogo wanaojiingiza kwenye biashara ya ngono, kwamba wanapata mbadala wa kujifunza ujuzi mbalimbali unaowapa mwelekeo wa maisha, wakajitegemee.
"Hakuna haja ya kujificha tena, dawa zipo na zinatolewa bure. Hakuna sababu ya mtu kujificha nyumbani ukijua una maambukizi ya virusi vya Ukimwi wakati huduma na matibabu inapatikana," anatamka Dk. Kahemele.
Hapo, Mkuu wa Kitengo cha Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, katika mradi huo, Eveline Maziku, anasema wanaendelea kuyafikia makundi mbalimbali yaliyo hatarini kupata maambukizi hayo, wakiwamo watumiaji wa dawa za kulevya na wanaofanya biashara za ngono na washiriki wa mapenzi ya jinsia moja.
Anaeleza watumiaji dawa za kulevya wako hatarini zaidi, virusi vya Ukimwi na homa ya ini, kwani wamekuwa wakichangia vitu vyenye ncha kali pasipo tahadhari, huku wakijiingiza kwenye ngono zembe.
Pia, anaeleza serikali inaendelea kufanya jitihada za kutoa elimu kwa makundi hayo, ikijumuisha kuanzisha vituo vya tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya, ambao wamekuwa wakijengewa uwezo wa stadi za maisha, ili wajitegemee na kuepukana na uwezekano wa kurejea katika matumizi ya dawa hizo.