Baadhi ya madhara yake ni kupotea kwa baadhi ya viumbe bahari, wakiwamo kobe wanaokufa kwa kujeruhiwa katika harakati za kujiokoa, baada ya kunaswa na nyavu.
Uvuvi wa nyavu za plastiki ulishapigwa marufuku nchini chini ya Sheria ya Uvuvi Mwaka 2003 na adhabu zake zinajulikana ni faini isiyopungua Sh.200,000 na isiyozidi Sh.milioni 15,000,000 au jela miaka isiyopungua miwili na isiyozidi miaka 10.
Nipashe limebaini kwamba, kukithiri vitendo hivyo katika ukanda wa Pwani ikiwamo mwalo wa samaki wa Kunduchi, jijini Dar es Salaam, unakinzana na kazi kubwa ya serikali kunusuru baioanuai hiyo.Mvuvi Ibrahimu Ng'eve, anasema nyavu hizo huletwa na wafanyabiashara kutoka nchi jirani na wanaowauzia wavuvi wa nchini.
"Kwenye nchi za wenzetu wameruhusu kutumia zile nyavu, lakini kwetu hapa sisi sheria hairuhusu, kwa sababu zina madhara makubwa sana kwa samaki,” anasema Ng’eve.
Hilo linafafanuliwa na Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Kinondoni, Godfrey Mrosso, anayesema baadhi ya wavuvi wanazitengeneza kwa kutumia mishipi ya ndoano za kuvulia samaki, ingawa shughuli hiyo inatumia muda mrefu.
"Zile nyavu ni zile za mshipi ambazo wanatumia wale wanaotumia ndoano kujipatia samaki, lakini inawezekana wakawapo watu wanaonunua hizo nyavu halafu wakaenda kusuka nyavu za kuvulia samaki, japo kufuma nyavu ni kazi… wapo wanaoweza, ingawa wanafanya hivyo kwa kujificha,” anasema .
Mvuvi, Sadiki Chale, anasema wavuvi wanapenda kutumia nyavu hizo, kutokana na uwezo wake wa kukaa kwenye maji muda mrefu bila ya kuharibika na kukamata samaki wengi, jambo ambalo nyavu za kawaida haziwezi kufanya.
“Wenzetu hao wanasumbuliwa na tamaa ya kupata samaki wengi na kusahau maisha ya baadaye, kwa sababu zile nyavu zinanasa samaki wengi hadi wenyewe wanashindwa kuwabeba wote. Wengine wanawaacha wanakufa, madhara yake mazalia ya samaki yanazidi kupungua” anasema Sadiki.
Anaeleza kuwapo wavuvi wanaozipaka sumu nyavu hizo, ili samaki anayenasa asitoke na hata wale wanaonusurika kwa hatimaye wanakufa kutokana na sumu wanayokutana nayo, zao lake ni samaki wapo hatarini kupungua.
Ripoti iliyotolewa na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) mwaka 2022 inayoitwa ‘Stop Ghost Gear’, inaonyesha matumizi ya vifaa vya uvuvi hatari, yanadhuru kwa kiasi kikubwa viumbe bahari.Ina ufafanuzi kwamba vifaa hivyo hudhuru asilimia 66 jamii ya viumbe bahari kwa aina ya saba au viumbe bahari, wakiwamo ndege na kasa wa baharini, wakisababishiwa vifo vya taratibu.
MADHARA YANAYOTAWALA
Mtaaluma, Prof. Philip Bwathondi, anasema uvuvi wa kutumia nyavu za plastiki huchangia samaki wengi kufa bila sababu za msingi, kutokana nyavu zile kunasa samaki wengi kuzidi uwezo wa wavuvi.
Anasema, samaki wengi wananasa kwenye mtego wa nyavu kiurahisi zinapokuwa majini, kutokana na rangi yake kufanana na maji.
Mwanazuoni huyo anafafanua kwamba, huwa wana kawaida ya kuziacha nyavu katikati ya bahari, kwa kuhofia watakamatwa nazo.“Wanapoziacha kwenye bahari, samaki wengi wananaswa na hivyo wanapokuja kesho yake, wanakuta samaki wengi wamenaswa na wengine wamekufa. Hivyo, wanawachukua kiasi wanachotaka na kuacha wengine wakiendelea kufa,” anasema.Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, nyavu hizo ni plastiki haziozi zinapoachwa bahari zimetelekezwa, inasababisha madhara kwa samaki wengine, akirejea mfano pia na kiumbe kobe kusababishiwa majeraha au kifo.Lingine analolitaja ni kwamba, nyavu hizo zina matundu madogo yanayonasa hadi samaki wachanga, ambao hawajakomaa kwa ajili ya kuliwa, hivyo inaathiri vizazi vyao katika viumbe bahari.
“Ukienda huko katikati ya bahari kama kuna eneo ambalo nyavu hizo zimetelekezwa, utakuta mamia ya samaki wamekufa baada ya kunaswa,” anasema.
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO linakadiria uvuvi haramu usioripotiwa na usiodhibitiwa, husababisha kupotezwa tani milioni 11 hadi 26 za samaki kila mwaka, huku hasara za kiuchumi ni kati ya Dola za Marekani bilioni 10 hadi 23, sawa na Sh. trilioni 23.37 hadi Sh. trilioni 53.751.
SERIKALI INAVYOPAMBANA
Ofisa Uvuvi Mrosso, anasema serikali kwa kushirikiana na viongozi wa mialo ya samaki, wanaendelea kuwasaka wavuvi wote wanaofanya kazi hiyo kinyume na sheria ya uvuvi na adhabu inatolewa kwa wakosaji wanaokamtwa na kuthibitika; faini au jela.
“Tuliwakamata wavuvi wanaotumia nyavu hizo kama mwaka mmoja au miwili iliyopita, baada ya hapo tukawapeleka polisi wakachukuliwa hatua za kisheria. Kwa hivi karibuni, hatujafanikiwa kuwakamata, lakini inawezekana wapo wanaofanya kwa siri na sisi hatutochoka kuwasaka,” anasema
Pia, anasema huwa wanatoa elimu ya madhara ya uvuvi haramu kwa jamii, viumbe bahari, mazingira, akiamini inatoa mwamko wamekuwa wakitoa taarifa, pale wanapomnasa mvuvi mwenzao akifanya vitendo hivyo.
Msimamizi wa Mazingira ya Bahari na Fukwe, anayeshughulika na masuala ya takwimu Msasani, Justine Ndola, anasema huwa wanafanya doria za usiku na pindi wanapogundua dalili za vikundi vya wavuvi haramu, wanatoa taarifa kwa polisi majini, wanaofuatilia na ikibainika uhalifu wanawakamata.
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Wanamaji Tanzania, Moshi Sokoro, anasema shida yao kubwa ni namna ya kuwakamata, kwa kuwa nyavu wanaziacha baharini.
“Hizo nyavu wamekuwa wakiziacha ndani ya bahari, kwa sababu zenyewe haziozi tofauti na nyavu za kawaida. Kwa hiyo, kuwakamata inahitaji uwe na mbinu mbadala au mmojawapo wa wavuvi waliokuwa wanafanya nao kazi awageuke na kutoa taarifa,” anasema
Aidha Msimamizi Mazingira, Andola anataja changamoto nyingine inayowakabili ni kukosekana vifaa vya kuwafuatilia, ikiwamo vya usafiri.
"Tuliwahi kupanga doria ya kuwasaka tukawakamata wavuvi kama unaenda kwa Nyerere (Msasani), walipotuona wakakimbia, sisi tukachukua nyavu na mitumbwi yao tukazileta hapa ofisini, baadae tukawapigia watu kutoka Ofisi ya Ofisa Uvuvi Kinondoni, wakaja kuzichukua," anabainisha.
NINI KIFANYIKIE
Mvuvi Ibrahimu Ng'eve, anasema serikali inapaswa kujenga utamaduni wa kupitia kila mara maeneo kunakofanyika uvuvi, na kushirikiana na wavuvi kuwabaini watu hao, kwa sababu wanafahamika.
Mkurugenzi wa shirika la Aqua Farm Organisation (AFO) linalojishughulisha na usalama wa viumbe bahari, anasema kuna haja ya serikali kutoa elimu inayojitosheleza kwa wavuvi na madhara ya kutumia neti hizo.
“Kikubwa hawa wavuvi bado elimu haijawaingia vizuri, kwa sababu mpaka sasa hawaelewi kuwa ule uvuvi una athari kubwa kwa uchumi wao hapo baadaye, serikali iwaeleze hili na ninaamini watabadilika,” anasema.
Hadi sasa kuna wito wa kimataifa, kwamba kuundwe mkataba wa kimataifa utakaozuia uchafuzi wa bahari unaotokana na taka za plastiki, ikiwamo neti haramu na kuhamasisha nchi kuunga mkono mkakati wa kuzuia utumiaji vifaa hatarishi baharini.










