USHUHUDA WADAU, WANASIASA

22Mar 2023
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
USHUHUDA WADAU, WANASIASA
  • Anayoyafanya Rais yanaonekana mchana, hata gizani kwa ukamilifu *Kushirikiana na upinzani, shule nyingi ghorofa, kuimarika utulivu

VIONGOZI na wadau wa kisiasa Zanzibar wanayaelezea mafanikio ya miaka miwili ya Rais Samia Suluhu, hasa kuwa yanaonekana gizani na kwenye mwanga, si jambo la kutafuta au kusaka kwa bidii.

“Maendeleo tunayoyashuhudia CCM hatuna wasiwasi na jambo lolote na muelekeo wetu ni sawa na kula ngisi au pweza gizani, tuna mambo mengi ya maendeleo ya kuzungumza kwa wananchi bila kificho,”anasema Katibu wa Idara ya Itikadi, Uenezi na Habari wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis.

Anafafanua kuwa mafanikio hayo yanaonekana kwa wazi bila kizuizi, iwe mchana au usiku, kwa mgeni au mwenyeji, mtoto na kijana wanakitambua kinachoendelea visiwani humo.

Akizungumzia tathmini ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia, anasema amedhihirisha kasi ya kuleta maendeleo Bara na Visiwani na kuongeza:“Mungu ametupatia zawadi, Mama ameupiga mwingi na kila mwenye macho anashuhudia maendeleo yanayojitokeza.”

Khamis anasema barabara za kuunganisha mikoa zinajengwa kwa kasi lakini pia nguvu zinaelekezwa ujenzi wa miundombinu ya vijijini, ili kuimarisha huduma za usafiri kunufaisha sekta zote kuanzia wakulima, wafugaji na wafanyabiashara.

Mradi unaoendelea wa ujenzi wa reli ya treni ya umeme utakapokamilika utafungua mlango wa kiuchumi ndani na nchi jirani kama Rwanda,DRC na Burundi kwa kuimarika sekta ya usafirishaji zaidi, anaongeza.

Aidha, anasema fedha za UVIKO-19 zimefanikisha miradi mingi ya maendeleo sekta ya afya, elimu na Zanzibar imekuwa mnufaika mkubwa kutokana na shule za kisasa za ghorofa zilizojengwa na hospitali za wilaya Unguja na Pemba.

Anaongeza kuwa chini ya Rais Samia, uhusiano wa kimataifa unaendelea kuimarika pamoja na serikali kurejesha uhuru wa vyombo vya habari uliokuwa unazorota hapo awali,

Akizungumzia maendeleo yaliyopatikana Zanzibar katika uongozi wa Rais Dk Hussein Ali Mwinyi, akishirikiana na Rais Samia, anasema miradi mingi ya afya, elimu, uvuvi pamoja na kuweka misingi ya utawala bora, kukomesha ubadhirifu na ufisadi wa mali za umma imefanikiwa.

Anasema licha ya kujitokeza mfumko wa bei, Zanzibar ina uhakika wa chakula na kwamba umeanza kupungua baada ya mvua kunyesha Bara na yapo matumaini ya bei kushuka baada ya wakulima kuanza kuvuna.

 “Mfumuko wa bei Zanzibar ulisababishwa na ukame wa mwaka jana, mtikisiko wa uchumi duniani uliosababishwa na UVIKO-19 na vita vya Russia na Ukraine”anasema Khamis.

FEDHA ZA UVIKO-19

Aidha, Khamis anazungumzia fedha za UVIKO -19 akisema SMZ imezitumia kumaliza upungufu wa maji baada ya kuipatia mamlaka ya maji (ZAWA) Shilingi bilioni 34.5 kujenga matangi ya kuhifadhi lita 1,000,000 kutandaza  mabomba ya kusambaza maji na kuchimba visima 120 pamoja na kununua pampu 55 za huduma za dharura Unguja na Pemba.

Akizungumzia kuendeleza wajasiriamali, anasema wamejengewa masoko ya kisasa maeneo ya Mwanakwerekwe, Jumbi na Mbuzini ujenzi ambao unatarajiwa kukamilika mwakani.

Katibu Mkuu Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu Dk.Aboud Suleiman Jumbe, akizungumzia mafanikio anasema miaka miwili ya Rais Samia uchumi wa buluu unapata mafungamano bora ya uhusiano wa kidiplomasia ili kufanikiwa.

Anawasifu Rais Samia na Dk. Mwinyi kuwa ni mabingwa wa diplomasia na kwamba Mwinyi ndiye mwasisi wa dhana ya uchumi wa buluu ambao ni miongoni mwa kazi za ilani ya CCM  2020-2025.

“Niseme miaka miwili ya Rais Samia madarakani diplomasia ya kimataifa ya uchumi wa buluu imefunguka na kuna mapinduzi makubwa ya sera za taifa na kimataifa zinazowezesha fursa mbalimbali kuibuka,’’anasema Dk.Jumbe.

Aidha, anasema SMZ inatekeleza miradi ya uvuvi wa bahari kuu,nishati ya mafuta na gesi pamoja na ujenzi wa bandari za mizigo na ya kutengeneza vyombo vya baharini.

Jumbe aliyataja mashirika ya kimataifa pamoja na nchi zilizofunguwa milango ya kuisaidia Zanzibar katika sekta ya uchumi wa buluu ikiwemo Benki ya Dunia itakayotoa Dola milioni 120 kuendeleza mradi uliojikita katika kujenga miundombinu zikiwamo huduma mbalimbali za samaki, viwanda vya kusindika pamoja na kilimo cha mwani.

 

UHUSIANO KIMATAIFA

Aidha, anasema Benki ya Uwekezaji ya Ulaya imetoa Yuro milioni 540 kwa ajili ya mikopo katika maeneo mbalimbali ya wajasiriamali zikiwa na lengo la kuwanyanyua na kuwajengea uwezo kufanya miradi yao.

Rais Samia ameonesha uwezo mkubwa katika kulitumikia taifa na kuimarisha uhusiano wa kimataifa, anasema Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Hamad Masoud.

Anaeleza kuwa chini ya uongozi wake wananchi wameshuhudia miradi mikubwa katika sekta ya afya, elimu pamoja kupunguza gharama za pembejeo kwa wakulima jambo ambalo litaongeza uzalishaji na kubadili sekta ya kilimo.

Masoud anasema Rais Samia amefunguwa milango ya demokrasia na hivyo kujenga mazingira mazuri kwa wanasiasa kufanya shughuli zao za kisiasa kwa amani na utulivu.

''Ameanza vizuri miaka miwili ameifungua demokrasia iliyokuwa ikilalamikiwa na viongozi wa vyama vya siasa, anafahamu kuwa mikutano ya kisiasa ndiyo uhai wa vyama ''anasema.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib anaitaja miaka miwili ya Rais Samia kuwa imefungua zaidi demokrasia ya vyama vingi akilenga kusaidia serikali iliyopo madarakani kwa kuikumbusha mambo ya msingi kama ahadi zake kwa wapiga kura.

Khatib anamsifia Rais kwa kutumia zaidi busara na kuwa msikilizaji wa  changamoto za wanasiasa, ameunda kamati ya wanasiasa iliyokuja na maazimio ya nini kifanyike katika uendeshaji wa siasa za kistaarabu nchini.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chama Cha ACT-Wazalendo Salim Bimani, anasema Rais Samia katika kipindi hicho amekuwa karibu zaidi na wanasiasa kwa ajili ya kutafuta maridhiano ya kudumu yatakayoimarisha amani na utulivu wa taifa.

'' ACT-Wazalendo tumeingia maridhiano na CCM ambapo tunashukuru amani na utulivu vimeimarika katika kipindi cha miaka miwili huku tukimshuhudia Rais Samia akifuatilia maridhiano hayo,'' anasema.