Ikumbukwe kabla ya kupata uhuru na baada ya kujitawala hadi miaka ya 1990, ungeweza kusema kipindi hicho ni ‘majira ya zamani’, lakini kuanzia miaka ya 1990 hadi leo 2023 kukiita kipindi cha majira ya sasa ni sahihi.
Iwe zamani au sasa masuala ya sayansi na teknolojia; mila, desturi, utamaduni, siasa na mazingira hususan mabadiliko ya tabianchi hayakwepeki kwa kumaanisha kwamba ni mambo yanayojitokeza katika vipindi vyote viwili utofauti ni kiwango cha kasi yanayokuja nayo,
Mathalani, sayansi na teknolojia hata zamani vitu hivyo vilikuwapo ila kiwango cha mabadiliko kimeonekana kushika kasi zaidi katika miongo mitatu iliyopita au zama hizi ama majira ya sasa.
Kadhalika kwenye masuala ya kijamii, utamaduni, mila na desturi nazo zina mabadiliko makubwa, mfano, mambo ya mila potofu na kandamizi hasa kwa wanawake na watoto zimeendelea kutoweka.
Masuala machache kama ‘ukeketaji’ na baadhi ya wazazi kutopenda watoto wao wapate elimu pamoja na serikali kuamua watoto wasome bure mpaka kidato cha sita, lakini hali bado ni ‘kizungumkuti’. Katika siasa pia kumekuwapo na mapya vipo vyama vingi. Zamani, msingi ulikuwa wa chama kimoja pamoja na falsafa na itikadi za Ujamaa na Kujitegemea zilijengwa kwenye msingi wa binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja na kuzingatia ‘utu’ na ‘heshima’ kwa binadamu wote bila ya kuwapo kubaguana.
Hali ya mazingira ukilinganisha zamani na sasa kasi ya kubadilika imekuwa kubwa nyakati hizi masuala mengine yameibuka na kutishia heshima ya binadamu.
Mathalani, mihemko na kushabikia, kwa kiasi kikubwa, uhusiano hata ndoa za jinsia moja.
Mambo kama haya yanasababisha kutokuelewana katika familia nyingi, jamii na taifa kwa ujumla kwa sababu yanagusa zaidi imani, maadili na misingi ya uumbaji wa wanadamu ambao ni mume na mke. Inafika mahali wengi wanajiuliza kulikoni katika majira haya ya sasa, wanaume kuoana?
Kwa miongo miwili iliyopita suala hili limekuwa likipigiwa gitaa kwa sauti kubwa ili wahusika kujinafasi wapendavyo. Katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu; Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam (1981) inabainisha kuwa ‘shoga’ ni jina linalotumiwa na wanawake walio-marafiki sana wakati wa kuitana au kujulishana kwa wengine.
Mfano, fulani ni shoga yangu kwa kumaanisha rafiki yake wa karibu neno likitumiwa zaidi mijini na kuzoeleka kwa kuhusishwa na kinamama walioshibana.
Vilevile, kamusi hiyo inabainisha kuwa ‘shoga’ ni aina ya mwanamume anayefanya mambo ya kike au kuashiria ni mwanamume asiye na uwezo wa kufanya tendo la ndoa.
Kadhalika, kamusi ya Kiingereza: inamtaja mwanamume anayefanya mambo ya kike kuwa ni ‘gay’ kumaanisha wanaume ambao wanavutiwa kufanya mapenzi ya jinsia moja.
Kwa lugha hiyo mwanamke anajulikana ni ‘lesbian’ hivyo, ‘gay’ na ‘lesbian’ ni wanaume na wanawake wanaohangaika na uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja na kwa pamoja kujulikana kama ‘homosexuals’.
Hii ni hali au dhana inayopingana na mahusiano ya watu wa jinsi tofauti yaani ‘mume’ na ‘mke’ kama ilivyoainishwa tangu kuumbwa kwa binadamu wa kwanza, Adam na Hawa au Eva.
Tangu uumbaji urafiki kwa watu wa jinsi moja ulikuwapo na kwamba watu wapendane, kama Mungu mwenyewe anavyowapenda. Hivyo, kulikuwa na upendo na hata sasa inatakiwa iwe hivyo kutokana na agizo la kupendana kama ndugu ambao ni sehemu ya uzao wa Adam na Hawa.
Sasa dunia imechafuka yanayozuka sasa yanaashiria hali ilivyo ya machafuko na yeye asili ya kishetani, kinachoshangaza ni chimbuko la machafuko haya kutokana na mataifa yenye maendeleo makubwa ya elimu, sayansi na teknolojia na utandawazi wa hali ya juu.
Mataifa kama Tanzania yanakazana kujiletea maendeleo (kwa kurejea yaliyofanyika katika nchi zilizoendelea sana).
Kimsingi, baadhi ya mataifa hayo yametawala Bara la Afrika, katika harakati za kutawala, wakaanzisha shule ili kuwe na elimu na kuongeza maarifa. Kadhalika, wakaanza kujenga baadhi ya miundombinu kama Reli ya Kati: Dar-es-Salaam mpaka Mwanza na Kigoma pia mpaka Mpanda mkoni Katavi. Vilevile, wakajenga bandari, barabara na huduma za afya mfano, hospitali na vituo vya afya na zahanati.
Juhudi hizo zililenga kuandaa Watanzania wakati ule Watanganyika na Wazanzibari, kuweza kumudu maisha kwa kuwa na afya njema, akili na maarifa na kufanya maamuzi sahihi.
Haikupita muda mrefu, Wamisionari kutoka mataifa yaliyoendelea wakafika nchini zaidi ya miaka 100 iliyopita kwa kusudi za kueneza injili ambayo ni habari njema kwa watu wote.
Kutokana na hatua hiyo, watu wakamjua Mungu wa kweli na kuachana na maagano au ibada za kijadi na kimila. Katika kumjua Mungu wa kweli, ndipo pia tulipofahamu kuwa alimuumba binadamu kwa mfano na sura yake:
Akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia pumzi ya uhai baada ya kumuumba Adam, Mungu akaona amekuwa mpweke; akasema ‘si vema huyo ‘mtu’ awe peke-yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye’.
Ndipo Bwana Mungu akamletea Adam usingizi mzito, kisha akatwaa ubavu wake mmoja akafunika nyama mahali pake na ule ubavu alioutwaa katika Adamu, akaufanya mwanamke akamleta kwa Adam. Hivyo, Mungu akaumba jinsia mbili ya kiume na kike na Adam akawa mzaliwa wa kwanza wakati huo msaidizi wake akawa mzaliwa wa pili.
Mungu akawabariki akawaambia zaeni mwongezeke na kuijaza nchi: mzaliwa wa kwanza Adam’ akapewa amri ya kumiliki na kutawala na kuisimamia familia yake ipasavyo wakati huo mzaliwa wa pili Hawa akiwa msaidizi wake halisi.
NI HAPANA USHOGA
Kwa msingi huo Mwenyezi Mungu ndiye asili na msingi wa familia zote; mwanamume aishi na mwanamke na wazae na kuongezeka zawadi ya watoto kutoka kwa muumbaji wao.
Kwa kuwa Hawa alitwaliwa katika mwanamume, hivyo mwanamume atawaacha wazazi wake baba na mama, naye ataambatana na mkewe na watakuwa mwili mmoja. Sasa taswira za mwanamume kumuoa ‘mwanamume’ au mwanamke kumuoa mwanamke zinatoka wapi? Hilo ni vyema lisikubalike. Dunia itakuwa jangwa kukowapi kuzaa na kuongezeka kama Mungu alivyowaagiza? Binadamu na Watanzania tafakarini njia zenu.










