Ni juhudi za serikali za kugharamia elimu msingi sekondari na hata kuwarejesha shuleni wale walioanguka kutokana na matatizo mbalimbali iwe ujauzito, kukosa ada, maradhi na ugumu wa maisha ya familia. Hivyo itakuwa ngumu kueleza kwanini bado wewe ni mbumbumbu.
Rais Samia anapoelekea kufunga miaka miwili, tangu alipoapishwa kushika nafasi hiyo, Machi 19 mwaka 2021 baada ya kifo cha mtangulizi wake, Hayati Dk. John Magufuli.Tangu wakati huo aliposhikia madaraka, yapo mengi ambayo serikali yake imeyafanya, katika sekta mbalimbali, kwa lengo la kutaka nchi inazidi kupiga hatua kwenda mbele kwenye maendeleo.Miongoni mwa sekta hizo, ni ya elimu ambapo katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake, amehakikisha wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo mimba, wanarudi shuleni kuendelea na masomo.Hadi kufikia Januari mwaka huu tangu Rais alipotoa maelekezo mwaka juzi, wanafunzi 1,692 walikuwa wamerudi shuleni, kuendelea na masomo katika shule mbalimbali za sekondari ni kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga.
Anatoa ufafanuzi huo bungeni jijini Dodoma mwaka huu na kuongeza kuwa wizara inaendelea kukusanya takwimu za shule za msingi na huenda wanafunzi waliorejea madarasani wakawa wengi zaidi na hiyo ni kazi kubwa ya kuwainua wanawake na mabinti.Aidha, anasema ili kumaliza tatizo hilo la mimba shuleni, serikali imeweka mikakati minne ukiwamo wa Rais Samia kuridhia kujengwa shule 26 za sekondari za wasichana ambapo kila mkoa utakuwa na moja,Kipanga anataja mkakati mwingine wa serikali kuwa ni kuanzisha vitengo vya elimu ya unasihi na ushauri, katika shule mbalimbali, ili kuhakikisha vitendo vya unyanyasaji visijitokeze."Pamoja na hiyo, mkakati mwingine wa serikali ni kuchukua hatua kwa wale wote wanaohusika, katika vitendo vya kunyanyasa wanafunzi, ili wachukuliwe hatua za kinidhamu," anasema Kipanga.Wakati Rais akiendelea na juhudi za kukomboa mtoto wa kike kielimu, sakata la mimba shuleni linaendelea kujitokeza, baada ya kuwapo kwa idadi kubwa wanafunzi kupata ujazito, katika kipindi cha mwaka 2021/2022.Kwa mujibu wa Naibu Waziri akiwa bungeni jijini Dodoma Januari mwaka huu, katika kipindi cha mwaka 2021 na 2022 wanafunzi 9,011 za shule za msingi na sekondari walipata mimba.Anafafanua kuwa wanafunzi 1,554 ni wa shule za msingi na 7,457 wa shule za sekondari walipata ujauzito, ambapo takwimu hizo zinamshtua Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson na kuitaka wizara kuandaa takwimu za idadi ya walioshtakiwa kwa kupatikana na hatia ya kuwapa ujauzito wanafunzi.Katika maelekezo yake, Dk. Tulia anasema takwimu kuhusu wanaume wenye hatia ni muhimu, ili kusaidia kuona kama sheria ya kuwalinda watoto dhidi ya vitendo viovu inafanya kazi na kuleta matokeo chanya.SAMIA SCHOLARSHIPNchi nyingi duniani zinazoendelea ni zile ambazo zimejikita katika ubunifu, kwenye utafutaji maendeleo ya wananchi wake, kutokana na ukweli kwamba, ubunifu ni nguzo kuu ya kufanikisha maendeleo.Kwa kuzingatia hilo, Rais Samia naye ameamua kuelekeza nguvu zake huko, kwa kuanzisha ufadhili wa masomo ya sayansi kupitia programu iitwayo (SAMIA SCHOLARSHIP 2022/2023), kwa wanafunzi wenye ufaulu mzuri.Tayari serikali ilishatenga Sh. bilioni 3, kwa ajili ya programu hiyo ya kuwasomesha wanafunzi waliopata ufaulu wa juu, katika masomo ya sayansi kwenye mitihani yao ya kidato cha sita.Vilevile, majina 640 ya wanafunzi wanaokidhi vigezo vya kuomba ufadhili huo yalishatangazwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na na Teknolojia, Profesa Aldof Mkenda jijini Dodoma Septemba mwaka jana."Wote ambao watahitimu chini ya Samia Scholarship watakuwa na uwezo wa kuomba mkopo na watapatiwa, ili kujiendeleza kimasomo. Ubunifu ni nguzo muhimu, Rais ameamua kuwekeza huko," Prof. Mkenda anasema.Kwa hatua hiyo, ni wazi kwamba katika kipindi chake cha miaka miwili madarakani, Rais amedhamiria kuhakikisha elimu inaimarika zaidi ikiendana na teknolojia na ubunifu wa vitu mbalimbali.Serikali imekuwa ikikutana na wataalamu wa elimu kutoka sehemu mbalimbali ili kubadilishana ujuzi na maoni ya jinsi ya kuangalia mitaala ili iendane na soko la ajira kidunia na pia kuhakikisha elimu inatoa ujuzi kwa wahitimu.UBORESHAJI SHULETangu aingie madarakani, Rais amejitahidi kuboresha miundombinu ya shule kuanzia ujenzi wa madarasa, uongezaji wa madawati katika shule za msingi na sekondari ili kuepusha wanafunzi kukaa chini au kusomea chini ya miti.Katika mwaka wa fedha 2021/2022, serikali kupitia fedha za UVIKO- 19 ilielekeza Sh. bilioni 300, kwa ajili ya kujenga madarasa 12,000 katika shule za sekondari na madarasa 3,000 kwa shule shikizi.Aidha, serikali ilitoa Sh. bilioni 160, kujenga madarasa 8,000 nchi nzima, huku kupitia mradi wa kuimarisha elimu ya sekondari nchini (Sequip) zikitolewa Sh. trilioni 1.2 ambapo Sh. bilioni 143.47 zilikuwa zimeshatumika katika ujenzi wa shule 232 katika mwaka wa fedha 2021/22.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angela Kairuki ndiye anayesema hayo na kufafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23 serikali itajenga shule 184 za sekondari katika halmashauri zote."Kila shule itagharimu shilingi milioni 600, lengo la serikali ni kutaka kuhakikisha hakuna kata ambayo itakuwa haina shule ya sekondari. Tunamshukru Rais Samia kwa kuchagiza maendeleo kwenye sekta ya elimu," anasema Angela.Pamoja na hayo anasema kwa miaka mitano ijayo, serikali itajenga shule 1,026 kupitia mradi wa Sequip na kupitia mradi wa kuboresha elimu ya awali na msingi itaboresha madarasa zaidi ya 9,000 yenye thamani ya Shilingi bilioni 250.9.Kwa ujumla ni kwamba, miaka miwili ya Rais Samia madarakani, serikali imejitahidi kuhakikisha inaboresha elimu katika ngazi mbalimbali kuanzia elimu ya awali hadi vyuoni.










