Wachezaji wa5 wanaotumia miguu yote kwa ubora sawa

13Mar 2023
Na Mwandishi Wetu
UINGEREZA
Nipashe
Wachezaji wa5 wanaotumia miguu yote kwa ubora sawa

KATIKA mpira wa miguu mchezaji kutumia miguu yote kwa ustadi na usahihi ni nadra sana. Ni ubora unaoweza kumpa mchezaji faida kubwa dhidi ya wapinzani wake.

Mchezaji mwenye uwezo wa kutumia miguu yote miwili anaweza kubadili mwelekeo wa kucheza chenga kwa urahisi, kupiga mashuti kutoka pembeni na nafasi tofauti na kupasisha mpira kwa usahihi na kasi akitumia mguu wowote.

Ustadi huu unaweza kuleta mkanganyiko kwa mabeki ambao huenda wasijue mchezaji atapita njia gani au atatumia mguu gani. Mchezaji wa miguu miwili pia anaweza kuwa fiti zaidi na kubadilika kwa nafasi tofauti uwanjani.

Kwa mfano, winga ambaye yuko na furaha kutumia miguu yote miwili anaweza kuwa na ufanisi sawa katika pande zote za uwanja, hivyo kufanya iwe vigumu kwa mabeki kuziweka alama. Kwa ujumla, uchezaji wa miguu miwili ni ustadi unaothaminiwa sana katika soka ambao unaweza kumfanya mchezaji kuwa bora zaidi na wa thamani kwa timu yake.

Hapa tunawaangalia wachezaji watano bora wenye uwezo wa kutumia miguu yote miwili dimbani, haya sasa...

 

#5 Son Heung-Min (Tottenham Hotspur)

Son Heung-Min ni mmoja wa washambuliaji bora wa kizazi chake. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Korea Kusini, amekuwa mtu muhimu pale Tottenham Hotspur tangu ajiunge na klabu hiyo mwaka 2015. Alishinda kwa pamoja Kiatu cha Dhahabu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu England na Mohamed Salah.

Ni mchezaji mahiri na hodari ambaye anasifika kwa ustadi wake wa kucheza chenga na uwezo wa kupata bao kutoka kwa masafa marefu. Ana wepesi sawa kwa miguu yake yote miwili.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 msimu huu hajawa kwenye kiwango chake bora, amefunga mabao tisa na kutoa asisti tatu katika mechi 33 alizocheza kwenye mashindano yote akiwa na Tottenham kufikia sasa msimu huu.

 

#4 Sergej Milinković-Savić (Lazio)

Kiungo wa kati wa Lazio, Sergej Milinković-Savić anajulikana kwa sifa zake za kuvutia za kimwili na uwezo wa kiufundi. Ni kiungo mrefu na mwenye nguvu ambaye yuko vizuri kucheza kama kiungo mkabaji na kiungo mshambuliaji.

Zaidi ya hayo, ana uwezo wa kutumia miguu yote miwili, ambayo ina maana kwamba anaweza kutumia miguu yote kwa usawa, na kumfanya asitabirike kwa wapinzani wake.

Amefunga mabao sita na kutoa pasi nane za mabao katika mechi 31 alizocheza kwenye michuano yote akiwa na Lazio hadi sasa msimu huu.

 

#3 Neymar Jr (Paris Saint-Germain)

Neymar Jr. alikuwa katika kiwango kizuri mwanzoni mwa msimu. Mchezaji huyo wa Brazil anachukuliwa kuwa mmoja wa wachezaji mahiri wa kizazi chake. Uwezo na ubunifu ni vitu muhimu sana kwake.

Ustadi wa Neymar wa kupiga chenga unazingatiwa sana, na ana uwezo wa kuwashinda mabeki kwa urahisi. Sifa nyingine muhimu ya Neymar ni kuwa na uwezo wa kutumia miguu yote miwili. Uwezo huu unamfanya kuwa mgumu kutabiri na kumkaba, kwani anaweza kubadilisha mwelekeo haraka au kupiga shuti kwa mguu wowote.

Katika mechi 29 za michuano yote aliyoichezea Paris Saint-Germain hadi sasa, amefunga mabao 18 na kutoa asisti 17.

 

#2 Kevin De Bruyne (Manchester City)

Kevin De Bruyne anasifika kwa umahiri wake wa ufundi na anatajwa sana kuwa kiungo mshambuliaji bora wa kizazi chake. Ana udhibiti bora wa mpira, ustadi wake wa kupiga pasi na ni mahiri katika kutengeneza nafasi za kufunga mabao kwa wachezaji wenzake.

De Bruyne ni mchezaji wa miguu yote miwili. Anaweza kupiga pasi, kupiga shuti na hata kupiga chenga kwa miguu yote miwili na hii inafanya kuwa vigumu kwa mabeki kutarajia hatua yake inayofuata. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji ana uwezo wa kupiga shuti akiwa katika nafasi mbalimbali.

Ingawa anapendelea kutumia zaidi mguu wake wa kulia, De Bruyne amefunga mara nyingi kwa kutumia mguu wake wa kushoto. Katika mechi 32 katika michuano yote aliyoichezea Manchester City kufikia sasa msimu huu, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31, amefunga mabao matano na kutoa asisti 18.

 

#1 Ousmane Dembele (Barcelona)

Winga wa Barcelona, Ousmane Dembele, anasifika kwa uwezo wake wa kipekee wa kiufundi kwenye mpira. Ni fowadi hodari ambaye anaweza kucheza kama winga ama mshambuliaji. Ubora wa kuvutia zaidi wa Dembele ni uwezo wake wa kupiga chenga kwa miguu yote miwili, jambo linalomwezesha kuwapita mabeki kwa urahisi.

Pia ni mpigaji sahihi wa mpira na anaweza kutoa krosi kwa usahihi kwa kutumia miguu yote miwili. Zaidi ya hayo, Dembele ana mbinu bora kwa miguu yote, inayomruhusu kufunga mabao kutoka pembe tofauti.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25, amefunga mabao nane na kutoa asisti saba katika mechi 28 kwenye michuano yote hadi sasa msimu huu akiwa na Barcelona.