Yanga ambayo mpinzania wake halisi kwenye mbio za ubingwa ni Simba, inahitaji ushindi kwenye mechi tano kati ya saba zilizobaki ili kuwa mabingwa wa Tanzania.
Kwa sasa Yanga imefikisha pointi 62, hivyo kama itacheza mechi tano na kushinda, itazoa pointi 15 na kufikisha jumla ya alama 77 ambazo hazitofikiwa na timu yoyote ikiwamo Simba.
Simba ambayo ina pointi 54 na imebakisha mechi saba ili imalize mechi zake zote 30 msimu huu, kama itashinda zote inazoa jumla ya pointi 21 ambazo ukizijumlisha na 54 ilizonazo unapata pointi 75, ambazo hazitoweza kuizuia Yanga kutwaa ubingwa.
Kimahesabu ni kwamba pointi 14 tu za Yanga zinatosha kuipa ubingwa kwani ukijumlisha na 62 ilizonazo unapata pointi 76, moja zaidi ya ambazo Simba itavuna ikishinda mechi zote.
Kwa takwimu na hesabu zote hizo, inaonyesha Yanga iko karibuni zaidi na ubingwa. Kitu pekee ambacho kinaweza kuchelewesha ubingwa huo ni kwamba kati ya mechi hizo tano ilizosalia, itacheza dhidi ya Simba inayoifukuza, mchezo unaotarajiwa kupigwa Aprili 6, mwaka huu.
Iwapo itashinda basi hesabu hizo zinaweza kutimia kwa asilimia 100, lakini kama itafungwa au kutoka sare, inabidi idadi inayotakiwa ya pointi itafutwe kwenye mechi zingine.
Hata hivyo, pamoja na mahesabu yote, lakini itategemea pia na matokeo ya mechi za Simba, ambapo kama kati ya hizo saba baadhi itapoteza au kutoa sare, itairahisishia njia zaidi Yanga.
Zifuatazo ni mechi tano ambazo kama ikichanga katara zake vizuri, basi itatawazwa kuwa mabingwa msimu wa 2022/23.
1. Yanga vs Geita Gold
Mechi hii imepangwa kuchezwa Machi 12, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Itacheza ikiwa imetoka kucheza mechi ya marudiano dhidi ya Real Bamako kutoka nchini Mali. Baada ya mechi ya kwanza iliyochezwa jana, timu hizo zitacheza tena Machi 8, ikiwa ni za Kombe la Shirikisho barani Afrika, lakini siku nne baadaye itacheza mechi hiyo dhidi ya Geita Gold.
Inaweza kuwa mechi ngumu, au rahisi kwa Yanga kwa sababu kadhaa. Ngumu kwa sababu itakuwa inacheza siku chache baada ya kucheza mechi kubwa zenye matumizi makubwa ya nguvu na akili na huenda ikawachosha baadhi ya wachezaji wake muhimu.
Urahisi inakuja kwa sababu Yanga wachezaji wake wanaokaa benchi, angalau wana viwango vya kupambana na kushinda mechi hasa za Ligi Kuu. Pia Geita Gold ambayo inashika nafasi ya tano, haipo kwenye msitari mwekundu wa timu zenye hatari ya kushuka daraja na kusema kuwa huenda wachezaji wao watapambana kufa kupona.
2. Yanga vs Kagera Sugar
Faida nyingine ya Yanga ni kwamba mechi hii pia wanachezea kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Ni uwanja ambao timu zinazoitwa au kujiita za mikoani zinapata tabu sana zinapocheza na Simba na Yanga.
Aprili 7, mwaka huu, Yanga inakwenda kucheza dhidi ya Kagera Sugar kwenye uwanja huo. Kama mechi ya kwanza.
Itakuwa ni siku tano, baada ya kucheza mechi dhidi ya TP Mazembe mjini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na hiyo itakuwa ni mechi ya mwisho ya Kombe la Shirikisho, Kundi D.
Ikiwa itafanikiwa kusonga mbele hatua ya robo fainali, itaongeza morali kwa viongozi, wachezaji na mashabiki wa timu hiyo kushinda mechi hiyo, bila kujali uchovu wa safari.
Lakini mechi inaweza kuwa ngumu kwa Yanga kama itashindwa kufuzu, kwani kisaikolojia wachezaji wa timu hiyo hawatokuwa vizuri.
3. Simba vs Yanga
Mechi ya watani wa jadi 'dabi' itapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Aprili 16, mwaka huu. Ni mechi inayosubiriwa na mashabiki wengi wa soka kwani wanaona huenda ikaamua hatima ya timu zote mbili kwenye kutwaa au kuukosa ubingwa.
Wachambuzi wa masuala ya soka wanasema huenda mechi hii ndiyo ikawa ngumu kwa Yanga kuliko zingine na kama ni kupoteza, basi inawezakana ikawa ni hii.
Hata hivyo, kama Yanga ikishinda, basi hakuna wa kuizuia tena kwani itakuwa imebakisha mechi nne za kumalizia na endapo itashinda mechi zote tatu ikiwamo hiyo, itakuwa imebakisha ushindi kwenye mechi mbili tu kutwaa ufalme.
4. Yanga vs Singida Big Stars
Yanga itacheza dhidi ya Singida Big Stars kwenye Uwanja wa Liti, Singida mechi ambayo mpaka sasa bado haijapangiwa tarehe.
Ni kwa sababu ya michuano ya Kombe la Shirikisho inayoendelea. Hata hivyo, wachambuzi na wadadisi wa masuala ya soka wanasema kutokana na ukaribu wa timu hizo mbili, huenda ikawa mechi nyepesi sana kwao, hasa nyakati hizi ambazo inahitaji kila pointi ili kutimiza azma ya kutwaa ubingwa.
Wengine wanadai mechi itakuwa ngumu kama Singida Big Stars itakuwa inasaka pointi za kumaliza nafasi ya tatu ambayo moja kwa moja itakuwa inapata nafasi ya kucheza mechi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika msimu ujao.
5. Yanga vs Dodoma Jiji
Ni mechi nyingine ya Yanga ambayo inatajwa ni rahisi kama kumsukuma mlevi kwenye utelezi. Dodoma Jiji haijawahi kuwa mbishi kwa Yanga tangu ipande Ligi Kuu. Tena kwa bahati nzuri itachezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kwenye tarehe ambayo nayo itapangwa baadaye.
Inawezekana kabisa hii ikawa ndiyo moja ya mechi ambayo Yanga inakwenda kutwaa ubingwa Tanzania Bara.
Hata hivyo, ugumu unaweza kuja pale ambapo Dodoma Jiji nayo itakuwa inalazimika kusaka pointi za kuiwezesha kubaki Ligi Kuu kwani ipo kwenye hali mbaya. Kwa sasa inashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 24.










