Baada ya vitambulisho sasa kwenye stika!

24Feb 2023
Joseph Kulangwa
DAR ES SALAAM
Nipashe
Baada ya vitambulisho sasa kwenye stika!

SERIKALI imekuja kivingine hakika kwa kutangaza kuondoa ukomo wa muda wa matumizi ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambavyo zamani vilikuwa na muda maalumu.

Awali vitambulisho hivyo vilikuwa vinakufa baada ya miaka 10 ya matumizi yake, lakini sasa kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Masauni Yusuf Masauni, ni tumia daima unavyotaka.

Hiyo maana yake ni kwamba utabadilisha kitambulisho chako pale tu kitakapokuwa kimeharibiwa kwa sababu moja au nyingine, na kama kitakuwa kimepotea, utapatiwa kingine.

Pamoja na hoja mbalimbali zinazotolewa na wadau zikiwamo za picha kubadilishwa kutokana na mmiliki kuzeeka na kubadilika sura na ile ya utambulisho kimataifa, kutokana na kusalia na tarehe za muda kumalizika kwenye vitambulisho, lakini uamuzi ni mzuri.

Uamuzi ni mzuri kama alivyobainisha Masauni, kwamba utapunguza kama si kuondoa kero ya kufuatilia kubadilisha, hasa kutokana na mchakato wenyewe wa kuvipata ambao umechukua miaka kadhaa, na mpaka sasa kuna watu hawana, licha ya kuingia kwenye mchakato.

Hakika, uamuzi huu hautofautiani sana na ule mwingine maarufu alioutoa Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni, wa kuondoa zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa nchini.

Hivi sasa wanasiasa hususan wa Upinzani wanajikamua hoja nzito nzito majukwaani kufahamisha wananchi nini kilitokea katika miaka saba iliyopita, wengine wakiita ya giza, huku baadhi wakijishajihisha na nini wanapanga kuwafanyia Watanzania endapo watawapa ridhaa na kuwakabidhi nchi kuongoza.

Yote kwa yote,Serikali hii imeonesha nia na dhamira ya dhati ya kuliweka sawa Taifa hili katika utulivu,amani na maridhiano yanayowafanya Watanzania kujisikia kuwa wamoja na kuacha dhana ya kubaguana kiitikadi, kama ilivyokuwa imeanza kukita mizizi huko nyuma.

Haishangazi, kwamba katika miaka hiyo saba iliyopita, Watanzania walibaguana waziwazi kiitikadi,huku wapinzani wakionekana kama wahamiaji haramu wasiotakiwa katika nchi yao ya kuzaliwa.

Rais Samia ameyakataa hayo yote na sasa anakaribisha kila Mtanzania kutoa ushauri, kukosoa na kuisema Serikali,lakini kwa hoja zenye staha na zisizochafua wengine, ilimradi ni kwa mustakabali  mwema wa nchi hii.

Wakati nikipongeza hatua hiyo ya Serikali, namwomba Waziri Masauni ageukie kero nyingine hii ambayo nayo hujitokeza kila mwaka ya Wiki ya Nenda kwa Usalama, ambayo madereva au wenye magari hutakiwa kupeleka magari kufanyiwa ukaguzi ili kuthibitisha usalama wao.

Hili ni jambo jema, linalojali usalama wa raia na mali zao,  kwamba gari salama lina uhakika wa usalama kwa dereva wake na lenyewe,kwani halitasababisha ajali barabarani.

Hatahivyo,ukaguzi huu wa magari nao umekuwa kama kero tu, kwa sababu kwanza hakuna maeneo mahususi ya kufanyia ukaguzi huo,lakini pia hakuna askari wa ukaguzi wa kutosha maarufuk ama ‘maveko (vehicle inspectors)’ wa kuifanya shughuli hiyo.

Kutokana na hilo, jambo hilo limekuwa likiachwa mikononi mwa askari wa usalama barabarani, wanaotembea na stika na kuziuza kwa madereva hata ambao magari yao hayajakaguliwa na matokeo yake kugeuka kitega uchumi binafsi.

Si kweli,kwamba magari yanapofanyiwa ukaguzi huo, hayawezi kusababisha au kupata ajali,hapana, ajali zipo na zitaendelea kutokea kutoka na na sababu mbalimbali ukiwamo ubovu wa magari, lakini madereva wazembe na ubovu wa miondombinu.

Pengine kama tuko makini na jambo hilo, basi kipindi hicho pia kingetumika kuwapima akili madereva wote, ili kuona kama wako timamu nah ivyo hawawezi kusababisha ajali wanapokuwa barabarani.

Kusimamisha gari na kumuuzia dereva stika ili aonekane gari lake limekaguliwa, si dawa ya kumaliza au kukomesha ajali za barabarani, ilani kujidanganya,na ni kero kusimamishana barabarani kwa kitu kama hicho, huku shughuli za kimaendeleo zikicheleweshwa.

Hivyo, nadhani Serikali kupitia kwa Masauni, ielewe kuwa kukusanya magari eneo moja kufanyiwa ukaguzi ni jambo lisilowezekana,zaidi ya kusababisha kazi za uzalishaji kiuchumi kuchelewa.

Bora ukaguzi wa kawaida barabarani ukaendelea kama ilivyo hivi sasa, lakini si kwa kusimamishana bila sababu.

Kufanya hivyo kutakuwa kumeongeza sifa ya nchi kukabiliana na usumbufu, malalamiko na lawama kwa watu wake,kama ilivyo kuwa kwenye mikutano ya hadhara na vitambulisho vya NIDA. Alamsiki!