Simba yatangaziwa vita na Azam FC

19Feb 2023
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Simba yatangaziwa vita na Azam FC

WAKATI jana usiku ilicheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablanca, Simba imetangaziwa vita na Azam FC ambavyo ipo kwenye maandalizi kabambe ya mechi ya Ligi Kuu dhidi ya timu hiyo inayotarajiwa kuchezwa Jumanne kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kaimu Ofisa Habari wa Azam FC, Hasheem Ibwe.

Azam tayari imecheza mechi mbili za kirafiki kwenye Uwanja wa Azam Complex, dhidi ya KMKM na kushinda bao 1-0, likifungwa na Prince Dube, pia Mlandege Jumatano iliyopita ambapo ilishinda mabao 3-0 yaliyofungwa na Abdul Selemani 'Sopu', Prince Dube na Cleophace Mkandala.

Kaimu Ofisa Habari wa Azam FC, Hasheem Ibwe amesema kama kuna timu ambayo Azam hupenda sana kucheza nayo basi ni Simba.

"Kama kuna timu ambayo tunapenda kucheza nayo hata kesho ni Simba, tena hii ambayo itakuwa imetoka kucheza mechi za kimataifa,” alisema Ibwe kwa majigambo.

“Najua Simba ni timu nzuri, tunaiheshimu sana na sisi kama Azam FC tunawatakia kila la kheri kwenye mechi zao zilizobaki za kimataifa, sisi ni baadhi ya wanufaika wa hizo nafasi. Sisi Azam tuna uhakika msimu ujao tutacheza mechi ya kimataifa kwa sababu yao. Siku zote huwezi kuthibitisha kuwa wewe ni timu kubwa kabla hujacheza na timu kubwa, na mara nyingi Simba na Azam huwa ni mechi nzuri sana ya kutazama," aliongeza.

Timu hizo zinakwenda kucheza mechi hiyo zikiwa kwenye mazingira tofauti, Simba ikiusaka ubingwa, Azam ikiisaka kwa udi na uvumba moja kati ya nafasi nne ambazo zitawafanya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao.

Simba ipo kwenye nafasi ya pili ikiwa na pointi 53, ikiwa imeshacheza mechi 22, huku Azam ikiwa kwenye nafasi ya nne kwa pointi zake 43, ikiwa imecheza mechi 22, juu yake ikiwapo Singida Big Stars ambayo ina pointi 44 kwa mechi 23 ambazo imecheza.