Wawili hao walizungumza vema sana kuhusu umuhimu wa hatua hiyo, wakisema kwanza inaokoa muda, pia inaimarisha uhusiano baina ya pande mbili zilizo kwenye mgogoro.
Wakasema, usuluhishi unapotumika kabla ya kufikishana mahakamani, uhusiano baina ya walio kwenye mgogoro hubaki ulivyo, kwani huhifadhiana siri, kuliko inavyokuwa mahakamani kila kitu kuanikwa.
Katika kuliimarisha hilo, Rais akaunda Tume ya Haki Jinai itakayofuatilia taasisi mbalimbali za kutenda haki kuona zinavyotenda, pamoja na changamoto zilizomo, ili zitatuliwe ili taasisi hizo zitende haki itakiwavyo.
Hata hivyo, usuluhishi hufanyika katika migogoro ya madai na si ya jinai, hivyo ni vizuri ikaitwa haki madai badala ya haki jinai, katika suala zima la utekelezaji wa usuluhishi katika migogoro ya kijamii.
Mara nyingi usuluhishi umekuwa ukifanyika katika masuala ya madai, kwani jinai mara zote hutatuliwa mahakamani ambako upelelezi hufanyika na ushahidi kutolewa na hatimaye hukumu.
Uzuri mwingine wa usuluhishi kwa mujibu wa viongozi hao wa kitaifa ni kwamba hapatikani mshindi ambaye husababisha mwingine kushindwa na hivyo kuibua chuki baina yao. Kwenye usuluhishi hufikiwa makubaliano na maisha kuendelea.
Watu wengi hujikuta zaidi katika usuluhishi ni katika ajira ambako kuna mwajiriwa na mwajiri na mara nyingi haya hujitokeza pale ajira inapokoma, kwa sababu yeyote, lakini yenye mwelekeo wa uonevu.
Waajiriwa wanaokuwa wameachishwa kazi na kuhisi kuonewa, ndio hukimbilia kwenye tume za usuluhishi (CMAs), ambako kwanza wasimamizi huomba pande mbili za mgogoro kusuluhisha na kwa mazungumzo nje ya mahakama.
Inaposhindikana, ndipo sasa shauri huingia mahakamani na kesi kuanza kama kesi zingine, ambako ushahidi na vielelezo hutakiwa, ili kuthibitisha madai dhidi ya mdaiwa.
Lakini, mara nyingi waajiri ambao ndio huonekana kushika mpini, hukataa usuluhishi na kuamua kusonga mbele kwa shauri kusikilizwa, kwa imani kwamba wanaweza kushindana kuwaacha wadai bila kitu.
Hilo hutokana na waajiri wengi wenye misuli kiuchumi, kuamini kwamba wanaweza kutumia fedha zao kufanya lolote na kushinda, hasa shauri linapokuwa mbele ya wasimamizi wenye uchu wa fedha na hivyo kushindwa kutenda haki.
Kama walivyotanabaisha viongozi wetu hao wawili wa kitaifa endapo usuluhishi utatumika muda utapungua, lakini gharama zitapungua ambazo ni za nauli, chakula, malazi na hata kumlipa mwakilishi (wakili).
Hata hivyo, mawakili wengi hawapendelei usuluhishi, kwa sababu wanajua shauri likimalizika mapema, nao hukosa kipato kwani wapo wanaolipwa kila wakionekana kwenye shauri, hivyo kumalizika mapema ni kukata mrija wa kipato.
Tamaa hii ndiyo imekuwa ikisababisha mashauri kulundikana katika tume hizo na mahakamani, lakini kuchelewesha haki ambako ni sawa na kunyima haki kwa walalamikaji au wadai, katika kesi au shauri husika.
Kama ilivyopendekezwa na baadhi ya wadau, Idara ya Mahakama nchini isimamie hili na kutunga sheria inayolazimisha usuluhishi wa mashauri, badala ya kukimbilia mahakamani, ili kuondoa changamoto hiyo ambayo si tu inaligharimu taifa pekee, ni mateso kwa wananchi.
Ukitaka kuona jinsi Watanzania wanavyoteseka hususan waliokuwa waajiriwa, nenda kwenye tume za usuluhishi na Mahakama ya Kazi, ndipo utaona jinsi watu wanavyohangaikia haki zao, pale wanapokuwa wameondoshwa kazini isivyo halali.
Kwa kuwa mashauri haya ya madai hayahitaji upelelezi kama ilivyo kwa mashauri ya jinai, ni vema usuluhishi ukawa wa lazima, ili kuondokana na kupoteza muda na kama wadaiwa watakuwa wanafanya jeuri kwa kutanguliza misuli ya kiuchumi, basi wanaposhindwa kesi walipe na riba.
Hiyo itakuwa sawa, kwa sababu mara nyingi waajiriwa hudai haki zao ambazo ni mishahara na haki zingine za kifedha, hivyo itokeapo mwajiri akabainika anafanya jeuri hiyo, basi ikionekana ni haki ya wadai wa kulipwa, ukokotoaji wa riba ufanyike ili ilipwe. Alamsiki!










