Ndivyo Chongolo alivyowapa raha wanachama , wananchi

08Feb 2023
Mary Geofrey
MOROGORO
Nipashe
Ndivyo Chongolo alivyowapa raha wanachama , wananchi

KATIBU Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, anahitimisha ziara mkoani Morogoro, akitatua kero zinazoibuliwa na wananchi na kutoa maelekezo kwa watendeji na wanasiasa wakiwamo mawaziri kumaliza changamoto zinazolalamikiwa.

Katibu Mkuu, Daniel Chongolo, akisikiliza na kutafutia majibu kero za maji wakati wa ziara yake Morogoro. PICHA: MARY GEOFREY

Anakutana na kero vijijini hadi mikoani katika sekta za maji, umeme, barabara, afya, elimu, ardhi na kilimo, kwenye ziara ambayo anaongozana na Katibu wa Uenezi, Sophia Mjema na Katibu wa Oganaizesheni, Issa Gavu, kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM na uhai wa chama, kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Katibu baada ya kusikiliza kero anazokutana nazo, anawasimamisha watendaji wa serikali wakiwamo wa vijiji, kata, wilaya, mkoa na wizara kutoa maelezo.

"CCM ndiyo yenye dhamana ya kuongoza nchini, ndiye mmiliki wa duka, tuna haki ya kuhoji, kuagiza na kuchukua hatua, kwenye mambo ambayo hayaendi sawa," anawaeleza viongozi na wanachama na wananchi.

Akiwa kijijini Mikese, anakuta kituo cha afya cha Mikese, ambacho baadhi ya majengo yamekaa zaidi ya miaka mitatu bila kutumika kwa kukosa vifaa licha ya kukamilika.

Anachukizwa na hali hiyo na kuihoji  Halmashauri ya Morogoro Vijijini, ambayo imeshindwa kutumia milioni 50 fedha za ndani, kununua vifaa vichache ili jengo la wazazi lianze kutoa huduma, wakisubiri vifaa kutoka serikalini.

Katibu Mkuu anashangazwa na halmashauri hiyo, kuwa na akiba ya bilioni 2.5 kwenye bajeti ya mwaka wa fedha uliopita na kusema.

"Hatuwezi kwenda namna hii, nitazungumza na Waziri wa TAMISEMI aje mwenyewe hapa ndani ya siku 14, aone fedha zilizowekwa hapa kwa ajili ya kujenga majengo haya lakini hayatumiki, inakuwaje”?

Hata tukiwaleta watumishi wa afya waliopangwa hapa nadhani wanatushangaa maana hawana kazi ya kufanya, madaktari nao hawana kazi wanatamani vifaa, anasema Chongolo.

"Na sisi tukija hapa tunasema kidumu Chama Cha Mapinduzi, kitadumu kama mambo yatanyooka, kama wenyewe tunajihujumu, haiwezekani ….."

BARABARA KUSUASUA

Akiwa Ifakara wilayani Kilombero, ujenzi wa barabara ya Kidatu hadi Ifakara yenye urefu wa Kilomita 66.9 kwa kiwango cha lami, anaambiwa umedorora.

Anamuagiza Meneja wa Wakala waTaifa wa Barabara (TANROADS), Morogoro Lazack Kyamba, kumsimamia kikamilifu mkandarasi ifikapo Oktoba 15 mwaka huu, awe amemaliza.

Anaeleza kuwa fedha zilishatengwa na kuwaonya wasimamizi watakao kaidi maelekezo hayo ya chama.

Akiwa katika Kijiji cha Melela, wilayani Mvomero, wananchi wanaibua kero ya kutolipwa fidia ya mashamba 2005 yaliyovamiwa na tembo.

Katika uvamizi huo, anaelezwa kuwa, wanavijiji 30 walipoteza maisha, na kusema changamoto haijibiwi kwa maneno mengi.

“Kama tembo walivamia maeneo ya watu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Pindi Chana au watendaji wa wizara na kuna mamlaka zake zilizopewa majukumu, ndani ya siku saba wafike hapa kuwaona wananchi," anaagiza.

"Tembo wamekula mazao, watu walipwe fidia, kinachotakiwa fedha ilipwe kwa walioharibiwa mashamba yao, waje hapa mpate haki yenu."

VIJIJI 68 GIZANI

Chongolo akiwa nyumbani kwa Katibu wa Shina namba 10 la chama hicho, Zainabu Ajili Kijiji cha Dumila Juu, anasalimiwa kwa kilio cha wananchi wa vijiji 68 kukosa umeme.

Aidha, wanalalamikia kuunganishiwa kwa Sh. 310,000 badala ya Sh. 27,000 iliyopangwa na serikali kwa maeneo ya vijijini.

Anawaahidi wananchi hao kuwa, Aprili mwaka huu, ataongozana na Waziri wa Nishati, January Makamba, kuwasha umeme katika vijiji vyote vya wilaya hiyo ambavyo havina huduma ilihali serikali imetoa fedha za kuwawekea umeme.

Chongolo anamtaka Meneja wa TANESCO, Fadhili Chilombe, kujibu kero hiyo. Akijibu anasema tatizo limetokana na kukosekana mawasiliano sahihi hapo awali.

"Kulikuwa kuna tatizo la mawasiliano ndio sababu ya kutozwa kiasi hicho, lakini kuanzia sasa watatozwa Sh. 27,000 badala ya 310,000."

KUPUNJWA MIWA

Kero ya wakulima wa miwa kupunjwa malipo ya utamu wa miwa na kiwanda cha Sukari cha Kilombero, inaibuka akiwa wilayani Kilombero.

Katibu CCM Tawi la Sanje- Kidatu, Timotheo Kihanji, anawasilisha kero hiyo, kwa niaba ya wakulima ,wanaodai kupunjwa kwa maelezo kuwa miwa haina utamu unaokubalika na kiwanda hicho.

Akijibu, Chongolo, anamwagiza Mkuu wa Mkoa huo, Fatma Mwasa, kukaa na Vyama Vya Ushirika wa Kilimo na Biashara (AMCOS), kuteua mkulima mmoja katika kila chama, kwenda kufundishwa namna wanavyopima utamu wa miwa kiwandani.

“Wakifundishwa na kufahamu namna kiwango cha utamu wa miwa unavyopimwa, watatoa elimu kwa wakulima wenzao na kupunguza malalamiko ,” anasema.

MAWAZIRI KITIMOTO

Licha ya majibu waliyotoa kwa wananchi wakiwa katika vitongoji, vijiji na maeneo mbalimbali ya mkoa huo, Chongolo anaendelea kusaka suluhu ya kudumu kutoka kwa mawaziri.

Akihitimisha ziara yake mkoani Morogoro, anawaita mawaziri ambao wizara zao zinatakiwa kufuatilia, mfano TAMISEMI, Naibu Waziri, David Silinde, anatakiwa kujibu hoja ya mgawanyo wa walimu kwa usawa katika shule zote za serikali nchini, baada ya Chongolo kulalamikiwa kuwapo kwa upungufu wa walimu vijijini.

Silinde anasema baada ya agizo la Chongolo, tayari wameshatoa barua 545 za uhamisho kwa walimu wa mkoa huo na kutenga Sh. milioni 607 kwa ajili ya kazi hiyo.

"Tangu umetoa agizo la uhamisho, ndani ya siku saba tayari tumeanza kuwahamishia walimu katika shule ambazo hakuna walimu wa kutosha ikiwa ni awamu ya kwanza," anasema Silinde.

Kuhusu Shule ya Msingi Ngerengere, ambayo ilikuwa haijakamilika, anasema wamepokea maelekezo na Shilingi  milioni 100 kwa ajili ya kukamilisha ili wanafunzi waanze kusoma. Zimetengwa.

Akijibu vifaa vya matibabu katika zahanati na vituo vya afya mkoani humo, anasema serikali imetenga bilioni 95.7 na tayari vifaa vimeshaagizwa kwa ajili ya kufungwa na kutoa huduma ya matibabu.

"Kuhusu miradi ya barabara na mingine ya kimkakati ambayo imeshindwa kukamilika kwa wakati, Waziri wa TAMISEMI, Angela Kairuki, ataanza ziara wiki ijayo katika mkoa huu kwa ajili ya kuanza utekelezaji," anasisitiza.

SHIDA YA MAJI

Chongolo anamtaka Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi, kujibu hoja ya tatizo la kukosekana maji katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo ambayo yalilalamikiwa na wananchi katika ziara yake.

Maryprisca anasema, wizara inafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wanawake wanapata huduma ya maji nchini ili kuokoa ndoa zao zilizopata shida kutokana na foleni ya kutafuta maji.

Anasema umbali wa kupata huduma ya maji hautakuwa zaidi ya mita 400 katika maeneo yote nchini.