RUHUSA YA MIKUTANO NGAWAIYA:

08Feb 2023
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe
RUHUSA YA MIKUTANO NGAWAIYA:
  • Upinzani ni kioo serikali ikitumie sasa kujitazama

TANGAZO la kuondoa zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, leo linatimiza siku 37, huku baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani waliokuwa uhamishoni wakiwa wamerejea nyumbani na wengine wako mbioni.

Thomas Ngawaiya (katikati), alipozungumzia ruhusa ya mikutano ya hadhara. Wengine ni wajumbe wa taasisi hiyo, Pricoline Mafoe (kulia) na Rahim Kibanda. PICHA: SABATO KASIKA

Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu, ni mmoja wao, alikuwa anaishi Ubelgiji karudi Tanzania Januari 25 mwezi uliopita.

Kuruhusiwa kwa mikutano hiyo kumeendelea kuwaibua wadau, mitazamo na fikra mbalimbali kurejea uamuzi huo wa Rais Samia Suluhu Hassan, anaoutoa Januari 3 mwaka huu.Miongoni mwa wadau hao, ni Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo Tanzania (CEGODETA), inayomsifia Rais kwa kufanya uamuzi mgumu bila kusikia minong'ono na kelele za wasiotaka utawala wa vyama, vingi ikisema ni ushindi kwa Samia.Mwenyekiti wa taasisi hiyo ya jijini Dar es Salaam, Thomas Ngawaiya anaiambia Nipashe kuwa Rais amesimama kwa miguu yake, na kwamba kama kiongozi wa nchi aliyekomaa kisiasa ameona mapungufu yaliyokuwa kwenye katazo hilo na kuyasahihisha."Amefanya hivyo bila kujali minong'ono, anasema hapana, hatuwezi kuishi kwa kuogopana na kutaka vyama vingi virudi, kwani kwa miaka takribani saba ni kama havikuwepo.Amefanya jambo la kijasiri," anasifu Ngawaiya.Anafafanua kuwa uamuzi wa Rais ni faida kwa nchi na kwa serikali, kwa maelezo kwamba, vyama mbadala ni kama kioo kinachosaidia kuona kasoro na kuzirekebisha."Vyama vya upinzani ni kioo cha kujiangalia kama taifa. Sisi CEGODETA tunaona ni faida kwa nchi na kwa demokrasia ya vyama vingi Tanzania. Huo ndio uongozi. Kama mtawala hataki kujitazama katika kioo ambacho ni mawazo mbadala, basi atakuwa na tatizo," anaeleza.Kiongozi huyo anasema Rais anataka siasa za ushindani, ili hata mtu anapowania nafasi ashinde kihalali na si kupita bila kupingwa, na kwamba siasa za ushindani zitawaweka pembeni wale waliozoea ushindi wa kunyonga na wala si wa kuchinja na kuchuna kwa maana ya kufanyakazi kwa haki.

"Kwa uamuzi huu wa Rais wa kurejesha demokrasia ya vyama vya siasa, nadhani haitakuwa vigumu kumtangaza mgombea wa upinzani kama atakuwa ameshinda katika uchaguzi, kwani miaka kadhaa iliyopita vyama vya upinzani vilichukuliwa kama maadui," anasema.ANGALIZO KWA VYAMAMwenyekiti huyo anasema pamoja na mikutano ya hadhara, viongozi wa vyama vya siasa hawana budi kuzingatia kufanya siasa za kistaarabu, ili kuepusha msuguano kati yao na serikali."Watumie sheria ya vyama vingi vya siasa ya mwaka 1992, kuendesha shughuli zao za kisiasa, kwani inaelezea namna ya kufanya siasa kwa kurejea mwongozo," anasema.Anaongeza kuwa kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria, hakuna mwanasiasa anayetafuta uongozi kwa kumchafua mwenzake na kuwashauri wanasiasa kuachana na mihemko ya kisiasa."Kufunguliwa kwa mikutano ya hadhara sasa kumeenda kuwafikirisha wanasiasa kuanza kujipanga upya namna ya kujibu hoja zitakazoelekezwa kwao katika mazingira ya kujenga hoja muhimu kwa taifa," anasema.Ngawaiya anasema, iwapo wanasiasa watajenga hoja zenye mashiko kwa taifa, kuna uhakika hakutakuwa mmoja atakayefungua kinywa kwa matusi bali kukosoa na kushauri kistaarabu.Anasema CEGODETA wadau wakuu wa utawala bora, wamefurahia hatua ya kuruhusu mikutano ya hadhara na kuongeza kuwa taifa linajengwa na Watanzania wote, bila kuegemea kwenye itikadi za vyama vya siasa."Rais amewahi kusema, kwenye kujenga Tanzania bora anatamani kujenga jamii yenye maridhiano na maelewano, umoja pasipo kujali tofauti zetu za kisiasa, kidini, kikabila na nyingine zote," anakumbusha.Katika ufafanuzi, anasema Rais hakuishia hapo, bali alibainisha kuwa hilo litawezekana kwa kujenga jamii inayopata haki sawa mbele ya sheria, isiyobaguana na inayotoa fursa sawa za kiuchumi kwa wote."Anawaambia Watanzania kuwa anaamini maridhiano hayawezi kupatikana penye ubaguzi na pale ambapo kuna wanaokosa fursa na haki zao za kiuchumi na kiraia. Kauli hiyo inaendelea kupokelewa na wapenda maridhiano,"anasema.Januari 3 mwaka huu, imeweka alama kwa vyama vya upinzani vitaikumbuka, kwani ndio ambayo Rais Samia alitangaza kuondoa zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, huku Chama cha Wananchi (CUF) kikiwa cha kwanza kufungua pazia la mikutano hiyo.CUF ilifanya mkutano Januari 9, katika viwanja vya Bakhresa Manzese Dar es Salaam ulioandaliwa na chama hicho Wilaya ya Kinondoni, na kuhutubiwa ma  Mwenyekiti wa chama taifa, Profesa Ibrahim Lipumba.Baada ya CUF, CHADEMA nao wakazindua mkutano Januari 21 mwaka huu, jijini Mwanza ukihutubiwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freema Mbowe, na kufuatiwa na mingine iliyofanyika Dar es Salaam, Mwembe Yanga, akirindima Makamu Mwenyekiti Lissu ,aidha, mingine imeendelea kufanyika Musoma na Tarime.

Mkutano wa Lissu ulifanyika muda mfupi baada ya kutua siku hiyo akitokea uhamishoni nchini Ubelgiji nao pia unaandika historia.Wakati Lissu akiwa amerejea, mwanachama mwingine wa CHADEMA Godbless Lema, naye ametangaza kuwa yuko mbioni, ambapo taarifa zake zilizopo katika mitandao ya kijamii zinaelezea kuwa atatua Machi mosi mwaka huu.Taarifa hizo zinaelezea kuwa atatua katika Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kwenda moja kwa moja katika mkutano wa hadhara utakaofanyika jijini Arusha, ambako amewahi kuwa mbunge.mwisho