Pamoja na maendeleo makubwa waliyoyapata shughuli za kiuchumi zimechangia kuiweka dunia ‘njiapanda’ kutokana na athari zilizojitokeza na kusababisha mabadiliko ya tabianchi.
Kabla ya ‘nchi’ kuathirika ilikuwa na ‘tabia nzuri’, watu waliishi maisha bora na ya amani. Mathalani, mvua ya kutosha ilikuwa inanyesha kwa wakati, kulikuwapo vijito, mito midogo na mikubwa ikitiririsha maji mwaka mzima. Uhakika wa kupata mavuno mengi na chakula cha kutosha ulikuwapo.
Ilikuwa nadra kuwapo mafuriko au kusikia madaraja yamezolewa na maji ya mvua au sehemu za makazi ya watu kujaa maji mpaka kuharibu maisha, nyumba na mali.
Hali ya hewa ya sasa inayojulikana kuwa ni mabadiliko ya tabianchi imesababisha kuwapo na ‘tabia mbaya’ kiasi cha kufanya maisha hasa katika mataifa yanayoinukia kimaendeleo kuwa ya mihangaiko makubwa kila kukicha.
Ingawa kanuni ya maisha inataka ‘kuacha kulaza-damu’ bali kuhangaikie maslahi kwa bidii ili kula chakula, kiuhalisia hali ya mazingira imekuwa ngumu kiasi cha binadamu katika mataifa yanayoendelea, kutokwa jasho kiasi cha kupindukia.
Ukame umezidi zaidi hasa kwa miongo miwili iliyopita. Kadhalika, mvua ikinyesha ni hatari kutokana na mafuriko na kusababisha maafa.
Hali imekuwa ngumu hata wanyamapori nao wanahangaika mno kutafuta chakula na maji mpaka kuvamia makazi ya watu na kusababisha taharuki kubwa.
Haya yote maana yake nini au yanaashiria kitu gani? Ni matokeo ya uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanyika bila kujali athari zake kwa viumbe wengine. Hii ndiyo hali tunayoishuhudia sasa.
Kimsingi hayo ni matokeo ya kutoitii sauti na maagizo ya Muumba na kukosa hekima na maarifa katika kuitawala ‘dunia na vyote vilivyomo’. Sasa binadamu wanahangaika sana kutokana na kufanya mambo kinyume na mapenzi ya Mungu.
Tujiulize iweje tuangamizwe kwa ugonjwa usioeleweka au maradhi yanayozuka bila kujua chanzo chake? Wakati mwingine kutokana na mahangaiko ya binadamu huwa nasikia watu wakisema “akili nyingi maarifa kidogo”.
Kauli hizo zinaashiria kwamba binadamu tunajiletea hali ya ‘kuangamizwa’ kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kukosa maarifa ya kutosha au kwa kupuuzia ukweli.
Maendeleo-endelevu tunayahitaji lakini inatakiwa tutumie mbinu za kisayansi na teknolojia zisizohatarishi kwa maisha yetu na kwa kuzingatia maisha ya vizazi vijavyo. Tusiwe na roho za uchoyo na ubinafsi uliokithiri kiasi cha kujilimbikizia mali na fedha nyingi wakati rasilimali hizo zingetumika kwa faida ya wengi bila kuathiri mazingira.
Kwa kuzingatia halihalisi kama ilivyoainishwa katika vifungu vilivyotangulia, suala la kukabiliana na ‘mabadiliko ya tabianchi’ halikwepeki. Hapa, tunahitaji mbinu na mipango-mikakati iliyo sahihi na endelevu kuweza kupambana na hali hiyo lakini pia kuweka mazingira rafiki kwa vizazi vitakavyofuata.
Mojawapo ya mipango-mikakati ni kuingiza “Elimu ya Mazingira” katika mitaala ya shule na vyuo hapa Tanzania ili kuwajengea uwezo vijana waweze kupambana na hali ya hewa isiyotabirika kirahisi lakini pia inayoathiri mihimili ya uhai kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira.
Hivyo, ni budi kutayarishwe ‘mitaala’ kuhusu elimu ya mazingira na iingizwe katika mifumo ya elimu nchini na yawe masomo kama yalivyo mengine na wanafunzi watahiniwe ipasavyo. Katika kuandaa ‘mitaala’ masuala ya ‘maliasili yazingatiwe ikiwamo umuhimu wa wanyamapori, utalii endelevu, rasilimali ardhi na maji.
Natambua kuna mikakati inayoendelea kufanikisha suala hili muhimu mfano, elimu ya misitu katika shule za sekondari na vyuo. Hata hivyo vyombo husika ikiwamo Wizara ya Elimu, TAMISEMI, Maliasili na Utalii, Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, vyuo kama Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam (UDSM).
Aidha, Chuo Kikuu Huria Taasisi za Elimu, mfano Elimu ya Watu Wazima, taasisi za utafiti mbalimbali kama TAFORI, TAWIRI, TAFIRI, pamoja na kilimo na mifugo na wadau wengine washirikishwe kikamilifu.
CHA KUFANYA
Elimu ya mazingira katika shule ianzie ngazi ya chini kabisa mfano, shule za awali na za msingi, watoto wazoeshwe picha mbalimbali au mifano halisi kama mimea na miti, misitu, wanyama, ili waanze kuuelewa uhusiano uliopo kati ya misitu, mvua na maji yanayotiririka kutoka katika maeneo yenye misitu kupitia chemichemi hadi mito.
Kadhalika, katika shule za msingi wanafunzi wazoezwe kuyatambua mazao mbalimbali na uhusiano wake katika matumizi bora ya ardhi, misitu na wanyamapori.
Katika shule za sekondari na vyuo mitaala iwawezeshe kujua namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwapa maarifa zaidi kuhusu hatua za kuchukua ili kupambana na changamoto zitokanazo na ‘mabadiliko husika’.
Elimu na maarifa watakavyovipata vizingatie uwezo wao kusaidia uongozi vijijini kuhifadhi ardhi na maliasili zilizoko pia namna ya kuzitumia kwa misingi endelevu ikiwa ni pamoja na kupitisha na kusimamia matumizi bora ya ardhi.
Wakulima na wafugaji wazingatie kilimo na ufugaji kijani, misitu ya asili itunzwe na kutumiwa kwa misingi endelevu. Wataalamu wa misitu, ufugaji nyuki, kilimo na afya wapunguze muda wa kukaa ofisini ili watumie zaidi wakiwaelimisha na kuwasaidia wakulima na wafugaji namna bora ya kukabiliana na mabadiliko hayo.
Wanafunzi waanze kufahamu na kuelewa vizuri nini maana ya vyanzo vya maji kama, misitu lindi maji, mito, mabwawa, maziwa na ukanda wa bahari. Wakifahamu tangu ujana jinsi ya kuvitunza na kuviendeleza tutapiga hatua kubwa katika kutunza mazingira.
Suala la kupanda na kuitunza miti na jinsi ya kuanzisha na kuendeleza bustani za miche ya miti na matunda lizingatiwe.
Katika maeneo ya shule na vyuo kuwepo sehemu ambazo wanafunzi wanaweza kufanya mazoezi ya namna ya kuhifadhi udongo kupitia shughuli za kilimo au ufugaji pamoja na kupanda miti ya matunda ya mbao na nguzo.










