IONE HATARI HII

07Feb 2023
Pankras Luoga
DAR ES SALAAM
Nipashe
IONE HATARI HII
  • Mabegi makubwa, mazito kwa mwanafunzi ni kumwandaa… *Kusagika pingili mgongoni, ubovu wa mabega, shingo, kiuno na miguu

NI mwanzo wa mwaka wa masomo, shule zimefunguliwa mwezi mmoja sasa. Mambo mengi yanayowasumbua wanafunzi wanaokwenda shuleni kutembea umbali mrefu kuifikia shule na kurudi nyumbani, njaa shuleni hakuna chakula hata maji ya kunywa.

 

 

Wanaoishi mijini tatizo la usafiri kwenye mabasi ya daladala na mwendokasi ni changamoto. Lakini pamoja na hayo upo mzigo mgongoni unaowasumbua wanafunzi wa msingi na sekondari ni mabegi makubwa na mazito wanayokukuruka nayo kila siku waendapo shuleni.

Ni mazito na makubwa kama vile wamebeba mawe au vyuma vizito. Tukumbuke bado ni watoto hasa wa shule za msingi ambao wana umri wa chini ya miaka 15, kwa umri wao bado miili yao haijawa imara na kuwa na uwezo wa kunyumbuka na kuhimili mizigo mizito ya kiasi hicho cha kilo hata 15.

Hivyo suala hili linawafanya baadhi ya wanafunzi hao kupata madhara ya kiafya muda mwingine pengine bila hata wao kujua, kwa sababu madhara yake hayatokei kwa siku moja ila baada ya muda mrefu wa kuendelea kubeba mizigo hiyo mikubwa kuliko umri na uwezo wa mwili.

Jamii imekuwa ikishuhudia hayo yote yakitokea katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja njiani, barabarani, stendi za mabasi, ya daladala na mwendo kasi jijini Dar Es Salaam lakini bila kuchukua hatua kukabili na changamoto hiyo hasa kwenye mikutano ya wazazi, walezi na uongozi wa shule.

MADHARA WANAYOPATA

Mabegi hayo yanabeba daftari zote, karatasi, vitabu, kalamu, mikebe, rangi za kuchorea na kwa baadhi ya wanafunzi yana vyakula na vinywaji. Wengine huweka nguo hasa sweta na viatu na sare za michezo.

Nini madhara ya watoto wadogo kubeba mabegi makubwa na mazito kila siku? Athari zipo nyingi hasa kwa watoto wadogo wenye miaka chini ya 18.

Baadhi ya athari ni pamoja na kuleta matatizo mbalimbali ya kiafya yanazoweza kujitokeza na kuanza kuonekana katika kipindi kifupi japo nyingi ni baada ya muda mrefu.

Kwa mfano, kupata uchovu wa mwili mzima, kuumwa na mgongo, kusagika kwa pingili za uti wa mgongo, maumivu ya mabega, shingo, kiuno na miguu, kushindwa kusimama vizuri na kupinda mgongo, tatizo la mfumo wa upumuaji, mishipa ya fahamu na kupata matatizo ya msongo wa mawazo.

Madhara haya makubwa ya kiafya yanayotokana na kubeba mizigo mizito mara nyingi si rahisi kutibika.

Pia hutumia muda mwingi sana kuyatibu na fedha nyingi na kuongeza mzigo kwa familia na serikali katika kutoa huduma za kiafya kwa wananchi.

Aidha, watoto hawa hupata usumbufu mkubwa kutokana na kuwa na mizigo mizito muda wote kuanzia nyumbani, kwenye daladala mpaka darasani. Wote ni mashahidi jinsi wanafunzi wenye mabegi makubwa wanavyopata shida kwenye nyombo vya usafiri. Iwe ni kwenye daladala au magari ya mwendo kasi ya lifti na hata kwenye pikipiki. Wakienda darasani nako bado wanaendelea kuteseka na mabegi yao makubwa na mazito.

Zaidi ya hayo yote, utafiti uliofanywa na daktari Muhammad Mushtaq mwaka 2012 kuhusu madhara ya ubebaji wa mabegi mazito kwa wanafunzi wa shule za msingi nchini Pakistani, unaonyesha athari hizo na unataja wanafunzi kufanya vibaya kwenye masomo yao.

Anasema ni kutokana na kushindwa kusikiliza na kufuatilia masomo vizuri darasani kwa sababu za uchovu, kuumwa na mgongo na mabega na msongo wa mawazo ambavyo hufanya mwanafunzi washindwe kutulia.

UFUMBUZI

Kwanza anashauri kuwa jamii lazima ikubali kuwa mabegi makubwa na mazito kwa watoto ni hatari kwa afya zao sasa na baadaye. Baada ya kulitambua hilo lazima wazazi, jamii, walezi na shule zichukue hatua ya kusaidia watoto hawa dhidi ya changamoto hiyo.

Jamii iwasaidie kwa kuongea na walimu waweke ratiba za masomo ya kila siku ili wanafunzi wachukue daftari chache kulingana na masomo ya siku hiyo.

Aidha, ujenzi wa madarasa uangalie kuweka vyumba vya kutunza daftari za wanafunzi kwa kila darasa jipya.

Hili litasaidia wanafunzi kuchukua daftari chache kila siku kuliko iliyo sasa kubeba daftari nyingi kuliko yale yanayohitajika kutumiwa kwa siku hiyo.

Pili wazazi, walezi na familia waongee na watoto wao ambao wanasoma wawafahamishe madhara ya kiafya ya kubeba mizigo kila siku.

Na kukagua mabegi ya watoto wao ili kuona nini wamebeba na kama kinatakiwa kubebwa kwa muda au siku hiyo.

Pia kuwasaidia watoto wao kwa kufuatilia ratiba za masomo ili waweze kuchukua daftari zitazotumika kwa siku hiyo pekee.

Daftari nyingine zisizotumika kwa siku ziachwe nyumbani mpaka siku ya somo itakapofika na kuhitajika, pengine, utaratibu huu unaweza kuwa mgeni na mgumu kwa watoto kuufuata kutokana na mazoea ya hapo awali ila ufuatiliaji wa wazazi na walezi ukiendelea kwa muda mrefu basi wanafunzi watauzoea na kuutekeleza bila shida.

Watoto hawa wanatakiwa kujifunza mambo mema ya kubeba daftari na vitabu vichache hasa vile vinavyohitajika kwa siku ili kuepuka kubeba kila kitu na wakati mwingine vitabu huchanika na kuharibika.

Hivyo kuwa na mabegi makubwa na mazito kila siku waendapo shuleni ambayo huathiri afya zao sasa au hapo baadaye si jambo jema.

ANGALIZO MUHIMU

Wito wangu kwa jamii ni kuwa ianze sasa kuwasaidia watoto wanaokwenda shuleni kuachana na mizigo kila siku kulinda afya zao.

Hii itasaidia sana kuwalinda watoto na wanafunzi dhidi ya matatizo ya kiafya yanayoweza kuwapata mfano, upumuaji, kuumwa mgongo na tatizo la kusagika kwa pingili za uti wa mgongo, maumivu ya mabega, shingo, kiuno na miguu na matatizo mengine mengi.

Na mwisho watoto hawa hushindwa kufanya vizuri katika masomo yao kwa kuwa inakuwa vigumu kuwa na utulivu na kusikiliza walimu.

Wazazi na walezi lazima wawasaidie watoto kutambua kuwa kuna madhara makubwa ya kiafya yanayoweza kuwapata kutokana na kubeba mizigo hiyo mizito.

Kwa mfano, kama ratiba ya masomo inaonyesha kutakuwa na vipindi vinne kwa siku basi mtoto achukue daftari za masomo manne na sio zote 12 na vitabu ambayo havitumika kwa siku husika.

 Jamii nzima kuanzia walimu, wazazi na walezi, wanasiasa Wizara ya Elimu na ya Afya zijitahidi kuwaelekeza na kuwasaidia watoto ili kuachana na mazoea hayo.

Tukumbuke watoto ambao ni wanafunzi wa leo ni taifa la kesho hivyo lazima tujitahidi kuwaandaa na pia kuwalinda kiafya ili waweze kuja kutoa mchango wao katika ujenzi wa taifa muda wao ukifika.