Zao lake, ni tishio la eneo hilo kutokea jangwa, kutokana na uharibifu wa mazingira unaotokana na kukata miti ovyo.
Jamii mbalimbali huvuna mazao ya misitu wilayani hapa wakiegemea madai ya kujikwamua kiuchumi, pasipo kupewa uzito athari za uharibifu, zikiwamo zinazosababisha ukame.
Inatajwa hadi sasa kuna shehena nyingi za mazao hayo husafirishwa kwenda mkoani Dar es Salaam, ambako wako wanunuzi wengi, ikizingatiwa ni wilaya iliyo jirani na mkoa mkuu wa kibiashara kitaifa.
Kinachofanyika kutoka Kisarawe, ni kwamba wavunaji hukusanya mazao yao na kisha wachuuzi wanayafuata huko huko misituni. Hapo zinatajwa bidhaa kama kuni, mbao, mkaa na magogo, wanayasomba kwa magari na pikipiki na wakati mwingine huyasogeza kando ya barabara yakibebwa na mabasi ya abiria.
Uzoefu unaonyesha ni hali inayozua hoja kinzani, baadhi ya abiria wa mabasi wakisikika kulalamika wanachafuliwa na vumbi la mkaa yanayobebwa kwenye mabasi. Kwa kifupi, si hali rafiki kwa usafiri wa umma.
Mkaa huo unaopakiwa kwenye magunia, maarufu viroba, huingizwa na kufichwa ama chini ya viti vya abiria au kwenye sehemu ya kuweka mizigo ya abiria na hupita kwenye vituo vya ukaguzi, pasipo kukaguliwa na mamlaka husika.
Sasa kuna kikundi kilichojitokeza kukagua walakini huo unajitokeza kwenye huduma tajwa. Abdallah Mijayo na Seifu Mkali na wezao wengine wameanzisha Shirika la Maendeleo la Utunzaji wa Mazingira Tanzania (CMT) Wilaya Kisarawe.
Mijayo, ambaye ni mwenyekiti wa shirika hilo, anasema uharibifu wa misitu wilayani humo, umeshamiri kiasi cha kuwalazimisha wao kujitokeza kujinusuru na hali hiyo, kwa njia mbadala ya nishati.
Anasema, mtazamo ni haja ya watu wabadilike ili kuepukana na uharibifu unaotishia jangwa wilayani humo.
Mijayo anasema, hofu ya uharibifu huo imezidi kupanda kutokana na ushuhuda wa shehena za magunia ya mkaa, kuni, magogo na milunda kusombwa kuelekea Dar es salaam.
Anasema kwamba, hilo linawalazimisha kuanzisha shirika hilo, ili kuwahamasisha watu kuacha matumizi ya mkaa na kuni, badala yake wabadilike na kuanza kutumia nishati safi ya gesi.
OFISA MISITU
Kaimu Ofisa Misitu wilayani Kisarawe, Waziri Mkumbwa, anasema mwaka jana zaidi ya magunia 121,000 sawa na tani 60,000 za mkaa, pia kuni mita za ujazo 51,000; pamoja na ujazo wa mita 770 za magogo; na mita 10,000 za milunda, vyote vilibebwa kwenda jijini Dar es slaam.
Aidha, inatajwa kwamba kuna wastani wa pikipiki 150 zinazobeba magunia matatu makubwa kila moja kutoka wilayani hapa kila siku, kwenda Dar es Saaam.
Mkumbwa anaeleza kwamba, ni mazao yanayoongoza kwa kulipatia kipato kwa asiimia 68 wilaya hiyo, licha ya kwamba yanaharibu mazingira husika.
SEMINA KUWANOA
Hivi karibuni, shirika hilo la utunzaji mazingira liliitisha semina ya siku moja mjini Kisarawe, kujadili utunzaji wa mazingira kwa wakata mkaa na watengenezaji wa majiko ya mkaa.
Ni kazi ya kitaaluma iliyoandaliwa na shirika hilo likishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Shule Kuu ya Uchumi, ambako washiriki wakaiomba serikali kupunguza bei ya gesi, ili kuongeza idadi ya watumiaji wake, hali inayowapunguza watumiaji kuni na mkaa.
Pia, wakaiomba serikali kutoa elimu ya matumizi ya gesi kwenye shule na kwenye makazi ya watu, ili kuepukana na ajali zinazoweza kusababishwa na matumizi ya nishati hiyo.
Maombi hayo wameyatoa, baada ya mwezeshaji wa semina kuutaka umma ubadilike kwa kutumia nishati safi na salama.
Mtaalamu mwezeshaji, Dk. Onesmo Selejio, anatoa angalizo kwamba matumizi ya kuni na mkaa ni hatari kwa afya ya mtumiaji, kwani moshi wa mkaa una sumu na zinazidi kuwapo kila matumizi ya mkaa na kuni, zinavyoongezeka.
Kitaifa inaelezwa, hadi sasa asilimia 64 ni watumiaji mkaa; asilimia 26 wanatumia kuni; asilimia tano wako kwenye gesi; asilimia tatu umeme; wakati asilimia mbili zilizobaki ziko katika nishati nyinginezo.
Dk. Selejio anatahadharisha kuwa, afya ya wananchi itakuwa salama, endapo umma utabadilika kwa kutumia nishati safi, ikiwamo ya gesi.
” Mkaa na kuni zina sumu hivyo hakuna usalama kwa watumiaji,” anasisitiza.










