Miaka 59 ushindi wa Mapinduzi

11Jan 2023
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Miaka 59 ushindi wa Mapinduzi

KESHO Tanzania inaadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar, hongera kwa kila Mtanzania na Mzanzibari anayesimama na kutetea uhuru wa taifa hili kuanzia ule uliopatikana mwaka 1961 kwa upande wa Tanganyika na wa mwaka 1964 ambayo  ni Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoifanya kuwa Jamhuri huru.

Katika juhudi za kumwenzi mfalme wa Mapinduzi ya Zanzibar, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), kilieleza nia yake ya kuanzisha Kiti cha Utafiti (University Research Chair) ambacho kitakuwa cha kwanza kuanzishwa katika historia ya SUZA, kumuenzi Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Abeid Amani Karume.

 Kiti hiki cha utafiti kinalenga kumuenzi Karume na kuyaenzi mawazo na fikra zake kwa kuwa miongoni mwa wanaharakati na wanamapinduzi wakubwa waliopambana kwa nguvu zote kuhakikisha Zanzibar na Afrika inakuwa huru ili kujiletea maendeleo kiuchumi, kisiasa, teknolojia na sekta zote za maisha.

Kama kilivyo Kigoda cha Mwalimu Nyerere, cha Karume, kitahifadhi, kuenzi na kendeleza mawazo na fikra zake katika kuleta ukombozi na maendeleo ya Zanzibar, Tanzania na  Afrika kupitia utafiti na mijadala mbalimbali ya kisomi kutoka kwa wadau na wataalamu wa utafiti wa kada mbalimbali.

Ni jambo jema kuenzi kazi kubwa za wanamapinduzi ambao walitoa maisha yao kwa ajili ya Watanzania wa Tanganyika na Zanzibar.

Ujio wa Kigoda ni muhimu kwenye kuzienzi, kuzifahamisha na kuzieneza fikra na mawazo ya Karume kwa vijana na jumuiya ya Watanzania hasa zama hizi ambazo ni kama fikra na duru za kizalendo, ukereketwa na mapendo kwa taifa yanaondoka.

Ni nadra kuona vijana wakijitoa muhanga kwa ajili ya nchi yao, tofauti na walivyofanya waasisi wa Tanganyika na Zanzibar, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Karume. Wapo vijana leo,  wataisifu na kuizungumzia timu ya mpira ya Ulaya au  Afrika kwa sifa zote lakini ni nadra kukuta vijana hao  wakiwazungumzia na kuwasifia waasisi Karume na Nyerere.

Si kwa kingine, ila kwa namna walivyofanya mambo makubwa na kuanzisha fikra na mawazo ya utaifa, umoja, udugu na kulifikisha taifa hapa lilipo leo.

Karume ni mkombozi na mwana maendeleo anayeishi ni mshiriki mkubwa wa kutaka Zanzibar isiyo na umaskini, akijiunga na viongozi wenzake kuwapa Wazanzibari ardhi, kuwajengea nyumba Michenzani, Makunduchi na Gamba Unguja, wakati  Pemba zipo Micheweni, Mkoani, Wete na Chake.

Pamoja na hayo anawapatia wananchi maskini ardhi na kuwataka kila kaya kuwa na ardhi ya kulima karafuu ili kujiongezea kipato na kuwa na maisha bora.

Karume ni shujaa wa ukombozi na maendeleo ya nchi hii na Afrika. Karume aliamini kuwaelimisha watu kuwa kila raia apate elimu na kuanzisha utaratibu wa  elimu bila malipo, ni mambo ambayo hata sasa yanaishi na vijana wanatakiwa kuyafahamu na kuyaenzi kwa kusoma na kufanikisha ustawi wa taifa kupitia elimu kuanzia ngazi za awali hadi za juu.

Karume amefanya mambo mengi ambayo hata sasa yanaendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na ujasiri wa kutetea wanyonye. Leo Serikali ya Zanzibar na ya Muungano zinaendelea, kupambana na umaskini, kutumia rasilimali kama Bahari ya Hindi  kuwekeza kwenye uchumi wa buluu kuwainua watu.

Ni maono ya Karume yanayoonekana sasa SMZ, ikiendelea kupambana na rushwa, kutokuwajibika na matumizi mbaya ya rasilimali za nchi ili kuboresha maisha ya wananchi kwa ubunifu na juhudi kubwa kama walivyofanya viongozi waasisi walioondoa wakoloni na usultan.

Karume wakati wa mapinduzi alifanya mambo yote kwa juhudi kubwa kuondoa wakoloni na usultani, hivyo ni jukumu la Watanzania leo kuendelea kujenga msingi aliouweka kwa kutumia rasilimali zilizoko na kuwainua wananchi kutoka kwenye umaskini na kufikia uhuru kamili na maendeleo.