Uhalifu unaweza kudhibitiwa ushirikiano ukiwapo kwa jamii

29Dec 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Uhalifu unaweza kudhibitiwa ushirikiano ukiwapo kwa jamii

MARA kwa mara katika siku za sikukuu kunaripotiwa vitendo vingi vya uhalifu, ikiwamo wizi, watu kupigwa au kuporwa vitu vyao.

Lakini katika kipindi hiki cha Sikukuu ya Krismasi, matukio hayo hayajasikika kwa wingi kama ilivyotokea katika miaka ya nyuma.

Kamanda wa wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alitaja sababu ya matukio hayo kutoripotiwa kwa wingi ni jeshi lake kufanikiwa kudhibiti vikundi vya kihalifu maarufu panya road, pamoja kupunguza ajali za mwisho wa mwaka kutokana na ushiriki wa wananchi katika kufichua vitendo hivyo.

Hata kwenye mitaa kwa sasa watu wanaishi na kulala kwa amani kwa sababu wananchi wameona umuhimu wa kuwa na ulinzi shirikishi ambapo kila mwisho wa mwezi huchangishana kuwezesha wanaofanya kazi hiyo.

Pia sasa hivi ukipita mitaa mingi utakuta wameweka vizuizi vya kuzuia magari na watu wasiofahamika kupita bila kujitambulisha wanakwenda nyumba ipi.

Kwa kweli wananchi wakishirikiana na Jeshi la Polisi kufichua watu wanaofanya uhalifu kwenye mitaa yao, hakuna lisilowezekana na wizi na uhalifu hautakuwapo.

Kamanda Muliro alipozungumza na gazeti hili alifafanua kuwa jamii inapaswa kufuta dhana ya kuamini kila mwisho wa mwaka lazima yatokee matukio ya kihalifu na ajali nyingi.

"Tangu Septemba mwaka huu nilisema mambo ya kusema kila ikifika mwisho wa mwaka kuna ajali nyingi au matukio ya kihalifu sasa limefika mwisho, Jeshi la Polisi halitaki watu kuongea mambo ya kufikirika mimi ukiniambia kuna ajali nyingi nitakuuliza hizo ajali ziko wapi? Ukisema uhalifu nitakuuliza hao wahalifu wako wapi?

"Hata wale wanaokunywa pombe na kuingia barabarani hawatofika mbali kwa sababu askari wa usalama barabarani wamejipanga kila kona kitendo cha kusema kila mwisho wa mwaka lazima uhalifu utokee hilo halikubaliki."

Kamanda Muliro anaasa jamii kuwa inaposema hivyo maana yake inahalalisha kwamba lazima matukio hayo yatokee, mambo hayo Jeshi la Polisi haliyataki na hivyo vyanzo ameahidi kushughulika navyo kuhakikisha ulinzi wa raia na mali zake unaimarika.

Kadhalika, amekemea vitendo vya wananchi wenye tabia ya kutoa rushwa kwa askari akisisitiza kuwa wao ndiyo wanao washawishi askari kujiingiza kwenye tamaa hiyo.

“Mtu asipotoa rushwa askari atapokea nini? Kuna askari wetu wengine ndiyo wametoka mafunzo bado wadogo na wao ni binadamu unapo mshawishi kumpa rushwa maana yake unatuharibia askari wetu na sisi tukikukamata tutakuchukulia hatua za kisheria.”

Ameonya ikitokea umeombwa rushwa na askari ni bora uende kutoa taarifa kituo cha polisi. Asisitiza jamii kubadili mitazamo na kwamba mtu wa kwanza kabisa mbaya ni mtoa rushwa ndiyo maana jeshi hilo limegawa namba mbalimbali za kutoa taarifa ili mtu anapoombwa rushwa awaseme na pia wale wanaotoa ili vitendo vya kutoa na kupokea rushwa vikomeshwe.

Alichokisema Kamanda Muliro ni muhimu kikazingatiwa kwa sababu wananchi ndiyo walinzi wa kwanza wa wenzao na wao ndiyo wanaowafahamu wahalifu kwa kuwa wanaishi nao kama si jirani zao kwenye mtaa anaoishi. Umoja ni nguvu na ushirikiano huleta maendeleo na kutatua matatizo mengi.