Kwa mfano Bonde la Ihefu awali lilikuwa na ukubwa wa skwea kilomita 83 lakini kutokana na kuvamiwa na shughuli za binadamu ikiwemo kilimo cha umwagiliaji na ufugaji zimebaki skwea kilomita 10 tu mpaka kufikia mwaka huu.Kwa mfano uchunguzi unaonyesha kwamba leo ni siku ya 136 mto Ruaha ukiwa haujatiririsha maji jambo ambalo si la kawaida kuwahi kutokea kwa miongo mingi iliyopita.Hii inatoa ishara mbaya sana kwa vizazi vijavyo kwamba iwapo serikali haitachukua hatua za dharura kuokoa hali hii kuna uwezekano vizazi vijavyo vikakosa huduma muhimu ya maji ambayo yanategemewa kwenye shughuli mbalimbali za uzalishaji hususan viwandani.Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, waandishi wa habari wameamua kuonyesha uzalendo kwa kuanzisha kampeni ya kuokoa bonde la Ihefu na Mto Ruaha ili liweze kutiririsha maji kama ilivyokuwa zamani.
Waandishi wameaanzisha Chama cha Kutetea Mazingira na Rasilimali (MERICA), ambacho kiliandaa kongamano la mazingira mkoani Iringa lililofunguliwa na Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango mapema wiki hii.Miongoni mwa aliyoyasema Dk. Mpango wakati wa ufunguzi wa mkutano huo ni kuhusika kwa baadhi ya viongozi kwenye uharibifu wa mazingira hali inayowafanya wapate kigugumizi kutekeleza maagizo ya serikali.Alisema ametoa maagizo mara kadhaa kuhusu utekelezaji wa maagizo ya kuokoa bonde la Ihefu na Mto Ruaha lakini kwa muda mrefu hakuna kinachotekelezeka.“Bahati mbaya sana kuna kundi la baadhi ya viongozi ambao kwa maslahi binafsi wanachangia sana kwenye uharibifu wa mazingira, mimi siamini kwamba wale wanaoswaga ng’ombe wamevaa matairi ndio wenye ng’ombe 3,000 na kuendelea.“Wala siamini kwamba wakulima maskini ninaowajua kwamba ndio wenye mashamba makubwa wenye matrekta yanayoziba mito yetu na kupeleka kwenye mashamba yao, hawa ndio watu ninaosema wanywe sumu wakaue maslahi yao binafsi ili mazingira ya taifa letu yapone,” anasema Dk. Mpango.Anasema lazima iwepo mikakati ya kuokoa mito yote hususan ile ya kimkakati kama Ruaha Mkuu na kuongeza kuwa mazingira yameshaharibiwa na yenyewe yameamua kulipa kisasi na ndiyo sababu hivi sasa nchi inahangaika na uhaba wa mvua na maji.Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Deodatus Balile, anasema mwaka 1974 bakuli la ardhi oevu la Ihefu lilikuwa na ukubwa wa skwea kilomita 83 lakini mpaka sasa limepungua zimebakia skwea kilomita 10.Anasema limepungua kutokana na shughuli za kilimo na ufugaji ambapo wakulima hao na wafugaji wameendelea kulizingira na kufanya shughuli zao kama kawaida.“Ng’ombe mmoja akikamatwa faini yake ni Sh 100,000 lakini ikitolewa namba ya malipo mtu anaweza kulipa ndani ya sekunde 20 hata yangekuwa mamilioni lakini ng’ombe wakikamatwa wakisema wawanadi wahusika wanakamatwa na unakuta Naibu Waziri anapiga simu ng’ombe waachiwe,” alisema Balile“Hawa ng’ombe wakikanyaga bonde la Ihefu inamaana ile ardhi oevu wanaikandamiza inakuwa ngumu kama bati na mvua ikinyesha maji hayaingii ardhini na badala yake yanapita zake kwa hiyo bonde hili ambalo linapokea maji kwenye mito 26 na kutiririsha maji kwenda Ruaha Mkuu linakosa sehemu ya kuhifadhi maji,” alisemaAnasema kwa mara ya kwanza mto Ruaha ulikauka mwaka 1994 na mwaka 1995 ukatokea mgao wa umeme hali iliyosababisha serikali kuanza kununua Megawati 100 kutoka kampuni binafsi ya uzalisha umeme ya IPTL.Anasema mwaka 2005 mto huo ulikauka kwa mara ya pili na 2006 serikali iliamua kuanza kununua umeme kwenye makampuni binafsi ya Dowans na Richmond hali ambayo ilisababisha kashfa kubwa ndani ya serikali.“Mwaka 2008 serikali iliamua kutoa notisi ya serikali namba 28 kwamba iongeze mbuga ya Ruaha kulinda vyanzo vya maji na kweli maji yalianza kuongezeka na vigingi havikuwekwa kwa miaka 14 na mwaka huu ndipo vimeanza kuwekwa vimefikia 45,” anasema Balile.“Kwa masikitiko makubwa kuna Ranchi ya Usangu ambayo ukiuliza watu wanasema hawajui nani anaimiliki lakini sisi tunafanya habari za uchunguzi inamilikiwa na familia 12 wakiwemo vigogo serikalini na majina tunayo tutakukabidhi,” alisemaGodwell Ole Meleing’ati ambaye ni Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Kamanda wa Uhifadhi Ruaha, alisema changamoto ya matumizi mbalimbali yaliyokinzana na yasiyo rafiki kwa mazingira yaliathiri na kusababisha kukauka kwa mto Ruaha.Anasema mwaka 1994 Mto Great Ruaha ulikauka kabisa na kwa mara ya kwanza tangu kuwepo kwake na mwaka 1995- hali ilizidi kuwa mbaya na kuathiri uzalishaji wa umeme na mwaka 1998 – Serikali iliingilia kati na kuamua kuweka eneo la usangu mashariki kuwa sehemu ya pori la akiba la Usangu ,wavuvi na wafugaji waliondolewa eneo hilo.Anasema mwaka 2006 hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya wafugaji na kilimo kushamiri Serikali ilifanya operesheni ya kuhamisha mifugo yote kutoka Usangu kwenda kwenye maeneo mengine na mwaka 2008- Pori la akiba la Usangu na baadhi ya maeneo ya vijiji yaliongezwa kuwa sehemu ya Hifadhi ya Ruaha, ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji za ardhi oevu ya Usangu na Mto Great Ruaha.Anasema Bonde la Usangu lina zaidi ya maeneo ya umwagiliaji 408 na kati ya hayo 2.7% zimeboreshwa, asilimia 18 zimeboreshwa kidogo, 23.3% ni maeneo ya umwagiliaji wa asili/kienyeji na 55.4% ya maeneo hayo hayana vibali vya matumizi ya maji.Kuhusu nini kifanyike kuokoa hali hiyo anasema lazima kukamilisha zoezi la mipaka ya Hifadhi ya Ruaha kwa kuweka alama, tathmini ya mali, malipo ya fidia, kuhama, kuondoa wavamizi wanaofanya shughuli ndani ya Hifadhi ya Ruaha kulingana na notisi ya serikali namba na marekebisho, kuondolewa kwa idadi kubwa ya mifugo katika Bonde la Usangu, mifugo imezidi katika bonde la Usangu (Zaidi ya 300,000), uwezo wa bonde ni mifugo 65,000.Anasema kuna umuhimu wa kutekeleza mkakati ya usimamizi wa vyanzo vya maji vya MtoRuaha Mkuu, kutambua vyanzo vyote vya maji, kusitisha uchepushaji wa maji , kubomoa kuta na kuondoa mabanio, kusitisha kilimo kiholela, tathmini ya matumizi ya maji kwenye mashamba makubwa, upandaji wa miti, kuandaa na kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi, kujenga miundombinu ya kuwezesha wanyama kupata maji na mbinu bora za kuwezesha Mto Great Ruaha kutiririsha maji, ujenzi wa kingo Ngiriama na mabwawa na visima vifupi na virefu.










